Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TGNP yatoa madai ya Jumla katika Katiba Mpya

TGNP yatoa madai ya Jumla katika Katiba Mpya



Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jana katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TGNP, Bi. Lilian Liundi (kulia) akifafanua jambo kwa baadhi ya wahariri katika semina hiyo.
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevilli Meena (kushoto) akijadiliana jambo na Mratibu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TGNP, Bi. Lilian Liundi. Kulia ni mmoja wa maofisa wa TGNP kutoka kitengo cha Habari.
Picha ya pamoja kati ya wahariri mbalimbali walioshiriki katika semina hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya (wa kwanza kulia aliyechuchumaa).

Na Joachim Mushi,Dar es Salaam

MTANDO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umetoa maoni ya jumla ambayo wangependa yaingizwe kwenye mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya ya Tanzania. Maoni hayo yalitolewa na TGNP kwenye semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika semina hiyo, Mratibu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TGNP, Bi. Lilian Liundi alisema madaraka katika muhimili wa utawala wa sasa ni makubwa hivyo kushauri yapunguzwe na kuwe na utengano kati ya mihimili mikuu mitatu ya nchi.

Bi. Liundi pia ametaka uwepo wa uwiano sawa wa kijinsia (50/50) huku akitaka mawaziri wasiwe wabunge na uwepo wa utaratibu wa viongozi (wabunge, madiwani) kuwajibishwa katikati ya mihula tofauti na ilivyo sasa.

Aidha mambo mengine ambayo Bi. Liundi ameyatoa kama changamoto na kushauri yaingizwe kwenye mchakato wa Katiba Mpya ni pamoja na kufutwa kwa adhabu, uwepo wa uhuru wa kupinga matokeo ya urais baada ya kutangazwa na ukomo wa uongozi wa wabunge, madiwani na serikali za mitaa.

Amesema siasa za uliberali mamboleo zilizoletwa na mataifa ya nje katika nchi za kiafrika zimesababisha mtafaruku mkubwa katika siasa za kiafrika, hali ambayo imezua migomo na mapambano dhidi ya uporaji wa rasilimali, ubinafsishaji wa huduma za afya na kuzifanya kama bidhaa na uporaji mkubwa wa ardhi na madini.

“Harakati hizi zimesababisha makundi ya kijamii, vyama vya siasa na wanaharakati kuanza kudai mabadiliko ya katiba katika nchi zao. Mfano mzuri ni nchini Kenya 2007,” alisema.

Pamoja na hayo alisema licha ya mchango mkubwa unaotolewa na wanawake nchini Tanzania bado hakuna fursa sawa kimgawanyo wa masuala mbalimbali.

Asilimia 80 ya nguvu kazi vijijini ni wanawake na asilimia 60 yao ni wazalishaji wa chakula. Wanawake ambao hawana ajira ni asilimia 40.3 (2006) ukilinganisha na wanaume ambao walikuwa asilimia 19.2 ( 2006), asilimia 66 ya wanawake wanafanya kazi zisizokuwa na kipato (kazi za huduma)... asilimia 39.5 ya wanawake hawajasoma ukilinganisha na asilimia 25.3 ya wanaume...,”

Awali akitoa mada katika semina hiyo ya wahariri, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema licha ya uwepo wa maendeleo kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka ya nyuma, bado kuna mifumo kandamizi inayoikabili jamii ya kipato cha chini.

Alisema maendeleo ya huduma za jamii katika maeneo mbalimbali kwa kiasi kikubwa yanawanufaisha zaidi wenye nacho (matajiri) na si masikini. “Huduma za jamii zimeongezeka ndiyo lakini wanaonufaika zaidi na huduma hizo ni wachache...ukiangalia utaona Serikali inawajibika zaidi kwa wafadhili na si wananchi wake...,” alisema Bi. Mallya.

Alioneza kwa sasa hata tabaka la wasionacho na walionacho ni kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma huku jukumu la kuihudumia jamii likirudi kwa familia zenyewe (majumbani) na si Serikali walioiweka madarakani kuwahudumia wananchi wake

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa