Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Alazwa kwa kupigwa risasi na polisi

Alazwa kwa kupigwa risasi na polisi


na Abdallah Khamis, Dar es Salaam
MKAZI wa Mbezi kwa Yusuph, Calvin Muro, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi na askari polisi wa kituo cha Mbezi Luis.
Akizungumza na Tanzania Daima hospitalini hapo jana Muro alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1.00 usiku wakati askari hao wakiwa katika harakati za kulikimbiza lori la mchanga.
Alisema awali aliwaona askari hao wakiwa katika gari aina ya Defender wakilikimbiza lori hilo lililoegeshwa Kimara B na dereva wake ambaye hakufahamika kukimbilia kwenye nyumba moja ya kulala wageni kisha askari hao kumfuata na walipompata walimpiga ngumi na mateke.
“Mwanzoni tulishangaa tukajua ni jambazi lakini tulipoona wanaanza kumpiga ilitubidi tusogee kujua kinachoendelea ambapo tulimsikia yule dereva akilalamika na kusema sina pesa na ninatakiwa nipeleke hesabu nyie mmezoea kutuonea,” alisema Muro.
Alisema baada ya wananchi kusikia kauli hiyo walianza kuwazomea askari hao ambao waliondoka na baada ya muda wakarudi na kuanza kufyatua risasi hovyo ndipo moja ikampata yeye chini ya makalio sehemu ya paja la kushoto na kutokezea kwa mbele.
“Sikuusikia mlio wa risasi bali nilijihisi kama navuja maji na nilisogea katika mwanga nikaona tundu kubwa limejitokeza mbele ya paja langu huku damu ikinivuja kwa wingi ndipo wenzangu waliponichukua na kunipeleka polisi kisha Hospitali Teule ya Tumbi Kibaha ambao nao walinihamishia hapa Muhimbili saa nane usiku,” alisema.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo (jina linahifadhiwa) aliieleza Tanzania Daima kwamba askari waliotenda unyama huo walikuwa wakitumia gari la polisi lenye namba PT 1412.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Kimara aliyefahamika kwa jina moja la Papalika alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikataa kuzungumza na kutaka atafuatwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela.
Hata hivyo juhudi za kumpata kamanda Kenyela ziligonga mwamba baada ya simu zake za kiganjani kutopatikana kwa muda mrefu.
Chanzo: Tanzania Daima

1 comments:

Tulinagwe said...

Hivi wananchi wa Tanzania tutaendelea kuonewa na kujeruhiwa hivi na police mpaka lini?na usikute hao police hata hatua wasichukuliwe.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa