Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » WATATU MBARONI KWA KUHUJUMU ZOEZI LA VITAMBULISHO VYA TAIFA

WATATU MBARONI KWA KUHUJUMU ZOEZI LA VITAMBULISHO VYA TAIFA


Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imewakamata watu watatu na kuwafikisha polisi kutokana na makosa ya kuomba fedha kwa watu wanaokwenda kujiandikisha vitambulisho vya utaifa.

Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Habari wa Mamlaka hiyo, Thomas William, alisema watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, yakiwemo Bunju, Mabwepande na Yombo Kilakala.

“Hawa watu wamefanya mambo ya kihuni…tumewakamata na tumewafikisha kwenye vituo vya Polisi, tunataka sheria ichukue mkondo wake. Hawa watu tumewakamata baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi, naomba wananchi waendelee kutupa taarifa kwani bila wao hatutajua uchafu unaofanyika katika vituo vya kujiandikishia,” alisema William.

Akizungumzia suala la msongamano kwenye vituo vya kujiandikishia, William alisema wameamua kuongeza idadi ya maofisa usajili katika vituo.

“Tumeongeza idadi ya maofisa usajili katika maeneo ..tumeongeza jumla ya wasajili 240…lakini pia mtu anayejua kusoma na kuandika atapewa fursa ya kujisajili mwenyewe kwa kupewa fomu, lengo ikiwa ni kupunguza foleni,” alisema William.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kuongeza muda wa kujiandikisha, alisema hivi sasa hawawezi kusema kama wataongeza muda hadi zoezi hili, litakapofika mwisho.

“Kwa sasa ni mapema kusema kama tutaongeza muda, tutakapofika tarehe ya mwisho ndiyo tutaona…lengo ni kuandikisha wananchi wote, kwa hiyo tutaona ifikapo mwisho,” alisema William.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dickson Maimu, alisema mamlaka ina vituo 451 na watendaji 2,279 na wataendelea kuongeza pale itakapohitajika.

“Tuna vituo 451 Dar es Salaam, huku watendaji wakiwa 2,279, lakini NIDA tumeongeza watendaji wengine 240 wiki hii na kufanya idadi hiyo kuwa ya kutosha kwenye vituo vyetu,” alisema Maimu.

Kwa mujibu wa Maimu, zoezi la uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa, limelenga kutengeneza daftari kuu la kudumu la utambuzi wa watu.

Hata hivyo, Mjumbe wa Serikali za Mtaa Sinza C, Fredriki Kapufi, amesema licha ya kuwa na mwamko mzuri wa wananchi, lakini kuna watu wengi bado hawajafikiwa.

Aliishauri Serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa vitambulisho vya taifa, kwani bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi.

Habari hii imeandikwa na Elizabeth Mjatta, Otilia Paulinus na Mariam Kibondei

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa