Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » KUWEPO KWA MUUNGANOMIAKA 50 NI JAMBO LA MIHIMU

KUWEPO KWA MUUNGANOMIAKA 50 NI JAMBO LA MIHIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAFANIKIO makubwa ya Muungano nchini ni kudumu kwa muundo huo kwa miaka 50, imeelezwa. Hayo yamesemwa na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu Dar es Salaam juzi, katika mahojiano na TBC 1, yaliyohudhuriwa pia na waandishi wa habari wa vyombo vingine.
Alisema nchi kadhaa duniani, ziliwahi kujaribu kuungana, lakini zilishindwa na alitaja baadhi ya nchi hizo ni Syria, Libya, Ghana, Guinea, Senegal na Gambia.
“Tuliungana nchi mbili na Muungano umedumu miaka 50. Haya ni mafanikio makubwa,” alisema.
Alisema mafanikio ya pili ni katika sekta ya uchumi, ambapo Pato la Taifa, limeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa mfano, wakati nchi inapata Uhuru mwaka 1961, pato la wastani la Mtanzania lilikuwa dola za Marekani 35, lakini sasa ni dola za Marekani 674.
Alisema uchumi wa Tanzania ni moja ya uchumi unaokua kwa kasi duniani, ambapo katika miaka 10 hadi 15 iliyopita, uchumi umekua kwa wastani wa asilimia 7.
“Uchumi unaelekea vizuri na ifikapo mwaka 2025 Tanzania itakuwa nchi ya uchumi wa kati,” alisema.
Hata hivyo, alisema kasi ya kukua kwa uchumi, hakuendani na kiwango cha kupungua kwa umasikini kwa sababu umasikini umekuwa ukipungua kwa asilimia 2 tu kwa mwaka wakati uchumi unakua kwa asilimia 7.
Alieleza kuwa asilimia 34 ya Watanzania, bado wapo kwenye kundi la watu masikini sana na hiyo ndiyo changamoto kubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Alisema sababu kubwa ya kuendelea kwa umasikini nchini ni kilimo kushindwa kukua vizuri vijijini, ambako asilimia 70 ya Watanzania wanaishi huko.
Alisema kilimo kinakua kwa asilimia 4.4 kwa mwaka, wakati sekta zingine za kiuchumi, kama vile simu, madini, viwanda na ujenzi, zinakua kwa kasi. Kuhusu changamoto za Muungano, alisema Muungano umekuwa na mitihani na misukosuko mingi.
Alisema busara za viongozi, ndizo zilizonusuru Muungano ikiwemo Tume ya Shelukindo iliyobainisha kero 31 za Muungano na Kamati ya Pamoja na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar, ambayo ilizipatia majibu baadhi ya kero hizo 31.
Rais alisema alipoingia madarakani mwaka 2005, kero zilizobaki zilikuwa 13, ambapo kero 9 zimepatiwa majibu na zimebakia nne, hivyo ukiongeza na nyingine mbili mpya, kwa sasa zilizosalia ni sita.
Kero zilizosalia ni suala la hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu, ajira ya Wazanzibari katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, suala la mafuta na gesi, ushiriki wa Zanzibar katika vyombo vya kimataifa, na usajili ya vyombo vya moto ambapo vimekuwa vikisajili Zanzibar na pia Bara Kero nyingine ni Zanzibar inataka fursa ya kujiunga na mashirika ambayo ina maslahi nayo, yanayoweza kuwapa mikopo na misaada.
“Changamoto kubwa iliyopo ni mjadala wa muundo gani wa muungano ni bora - serikali mbili au tatu.Mchakato wa Katiba mpya una fursa kubwa ya kubadili mambo mengi na kuipa Katiba yetu na Muungano wetu sura mpya. Wajumbe wa Bunge la Katiba watatupatia jawabu la kero zilizopo,” alisema Rais.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa