Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KWA
mara nyingine tangu kuanza mjadala wa kujadili sura ya kwanza na ya sita
ya Rasimu ya Katiba kuhusu muundo wa Serikali, Mjumbe Maalum wa Bunge
la Katiba, Tundu Lissu, ameendelea kutikisa Bunge hilo kutokana na hoja
kuhusiana na uhalali wa Muungano.
Mbunge huyo alienda mbali zaidi na
kusema kuwa hati za Muungano ambazo Serikali imeonesha saini za Abeid
Aman Karume, zimeghushiwa na kutaka hati hiyo ipelekwe bungeni ili
wabunge walinganishe saini hizo.
Lissu alitoa kauli hiyo mjini
Dodoma wakati akichangia mjadala kuhusu sura ya kwanza na ya sita ya
rasimu ya Katiba. Lissu alianza kuchangia akisema;
"Acha nijibu
vioja kuwa Tundu Lissu amemtukana Baba wa Taifa, sasa mwaka 1995 Baba wa
Taifa alihutubia mkutano wa Mei Mosi mkoani Mbeya na baadaye aliandika
kitabu chake alichokiita 'TUJISAHIHISHE' na katika kijitabu chake
alisema asiyekubali kukosolewa hawezi kuwa kiongozi bora."
"Baba wa
Taifa aliyekuwa Mwenyekiti na mwanzilishi wa CCM alisema CCM si mama
yangu hivyo Baba wa Taifa alikuwa binadamu, hakuwa Mungu hakuwa malaika
na hajawa mtakatifu bado kwa hiyo tunaposema makosa yake tunathibitisha
ubinadamu wake na Baba wa Taifa mwenyewe angekuwa wa kwanza kukubali
kuwa alikuwa binadamu na si Mungu na kama binadamu alikuwa anakosea."
Alisema
kwa wasiofahamu Baba wa Taifa aliwahi kuunga mkono vita ya Jamhuri ya
Biafra iliyokuwa inataka kujitenga na Nigeria alikosea hakuwa Mungu;
"Tunaposema alikosea hatumdhalilishi bali tunathibitisha ubinadamu
wake," alisema.
Alisema, “kuna watu ambao wako humu ndani bungeni
wakati wa uhai wake walikimbia chama chake na kujiunga na chama cha
NCCR-Mageuzi na wakasubiri Mwalimu amefariki wamerudi CCM na leo hii
ndiyo wanaojifanya kuwa watetezi wakubwa wa Baba wa Taifa.”
HATI ZA MUUNGANO
Akizungumzia
hati za Muungano, Lissu alisema; "Kioja cha pili ni kuhusu hati ya
makubaliano ya Muungano kuwa ipo au haipo kwani tumeoneshwa kitu hivi na
kuna sahihi kwenye mitandao mlinganishe sahihi ya Sheikh Karume iliyoko
kwenye hati ya Muungano katika sheria ya mabadiliko ya kwanza ya Katiba
ya mpito ya mwaka 1965.
"Leteni hiyo hati mnayodai kuwa ina saini
ya Karume tuwaoneshe hapa mlivyo waongo na kama hati hiyo ni halali
iliwahi kutungiwa sheria ya kuithibitisha Zanzibar?
“Je na hiyo
sheria ipo wapi na kwa mujibu wa Profesa Shivji kuwa Zanzibar haijawahi
kuridhia Muungano hadi kesho kutwa, hivyo basi kama masharti
hayakutimizwa kwa miaka 50 hiyo hati si halali."
Alisema hoja za
msingi kwa mahali tulipofikia sasa kikatiba na kisiasa na kwa mujibu wa
Dkt. Mwakyembe aliwahi kuandika kwenye kitabu chake kuwa muundo wa
shirikisho wa Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji
Nyalali, Kisanga, Warioba na wananchi ndiyo njia pekee ya kutatua
matatizo ya Muungano.
"Nathibitisha ukweli wa maneno ya Dkt.
Mwakyembe kwa katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
ile Katiba ya Zanzibar ambazo ni halali na ukisoma kama utaona kama vile
unasoma katiba za nchi mbili tofauti kumbe ni nchi moja," alisema Tundu
Lissu.
Alisema Rais Kikwete sio Mkuu wa nchi ya Zanzibar kwa Ibara
ya 26 (1) ya Katiba ya Zanzibar inasema; "Rais wa Zanzibar atakuwa Mkuu
wa nchi ya Zanzibar, hivyo Rais Kikwete si Amiri Jeshi Mkuu wa Zanzibar
na ibara ya 123 ya katiba hiyo inasema Rais wa Zanzibar ndiye Amiri
Jeshi Mkuu wa Vikosi vya ulinzi maana yake ni jeshi, hivyo tayari tuna
nchi mbili tofauti," alisema Lissu.
Alisema Ibara ya 9 inasema
kutakuwa na Mzanzibar yaani inazungumzia Mzanzibar na si Mtanzania;
"Hivyo hakuna ambaye atasimama hapa na kusema sisi ni nchi moja... nani
anayeweza kumbishia Dkt. Mwakyembe kuwa suluhisho la tatizo la Muungano
ni Serikali tatu?" Alihoji Lissu.
Alisema hata kiprotokali Rais
Kikwete, anapokuwa kwenye sherehe za Mapinduzi anapanga foleni kule
Zanzibar na anayepigiwa mizinga 21 ni Dkt. Shein.
"Hauwezi kuwa na
wakuu wa nchi wawili mmoja anaishi Magogoni na mwingine Mnazi Mmoja
wakipishana kauli hali itakuwaje," alihoji Lissu.
Alisema baada ya
miaka 50 tutengeneze utaratibu mpya na bila kuchukua hatua za haraka
mbele ni giza na watakaoleta vita si wale wanaotaka kufanya marekebisho
bali ni wale wanaofumbia macho wanaokwenda kuangukia kwenye vitindi
virefu.
Kwa upande wake mjumbe mwingine wa Bunge hilo Maalum Bernad
Membe, alisema yeye anaunga mkono msimamo wa chama chake wa kutetea
Serikali mbili.
Alimshukia, Lissu akisema hakuna nchi yoyote duniani
inayotukana viongozi wake na Bunge litakuwa la mwisho kufanya dhihaka
kwa viongozi na waasisi wa Taifa hili wanaheshimika duniani kote.
Kuhusu
hati ya Muungano, Membe alisema ameiona ni halali na ndio iliyokwenda
Umoja wa Mataifa. Alisema Tume ya Jaji Warioba itakuja kulaaniwa kwa
mauaji yatakayotokea kutokana na kubariki muundo wa Serikali tatu.
"Bunge
hili litakuja kulaaniwa kwa kubariki mauaji," alisema Membe. Naye
Mjumbe wa Bunge hilo, Zitto Kabwe, alisema Muungano ni imani hivyo
muundo wowote wa Muungano unavunja Muungano kama hakuna mwafaka
utavunjika.
"Tuwe wa Serikali mbili au moja au tatu kama hakuna
mwafaka lazima utavunjika tu na mfano mzuri ni wa Serikali ya shirikisho
ya Somalia, Ethiopia na Malaysia zilivunjika," alisema.
"Mchakato
huu ulipaswa kutengeneza maridhiano katika nchi yetu, unajenga chuki,
kutengana na majibizano ambayo wananchi huko nje wanatushangaa sana na
tumesikia lugha kali sana za kibaguzi humu ndani na hakuna juhudi zozote
kutoka kwa viongozi wetu kukemea ubaguzi hakuna sumu mbaya katika nchi
zozote duniani kama ubaguzi" alisema Kabwe.
Alisema kauli za vitisho
na kibaguzi zinatoka huku watu wanashangilia, lakini pia wanashangilia
matusi ya kupandikiza chuki... hatuwezi kujenga nchi kwa mtindo huo,
hivyo watu wajadiliane kwa hoja na watu wenye hoja zao watoe hoja zao na
baadaye tukubaliane na tuamue.
Alisema kuna baadhi ya wajumbe
wanazungumzia gharama kwa Serikali tatu zitakuwa kubwa, lakini hakuna
hadi sasa utafiti wowote wa kitaalam ambao unathibitisha hilo na baadhi
ya wachumi wameshindwa kuithibitisha.
Alisema kinachofanyika ni
kuondoa mambo yale ya kidola unaweka pembeni na tutaweza kuwa na Rais
mmoja, lakini wakuu wa Serikali ni wawili katika nchi moja ni jambo la
Makubaliano kwani hatuhitaji kujenga Ikulu mpya.
"Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment