Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MABADILIKO YA NJIA KATIKATI YA JIJI DAR KUFANYIKA MWEZI HUU

MABADILIKO YA NJIA KATIKATI YA JIJI DAR KUFANYIKA MWEZI HUU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam jana.
 
Katika  juhudi za kuimarisha hali ya usafiri na kupunguza msongamano, alama mpya za barabarani na mabadiliko ya njia yanategemewa katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.
Kazi ya kuondoa alama za zamani na kuweka mpya katikati ya jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kuanza Aprili 28, mwaka huu.

Akielezea mabadiliko hayo jijini Dar es Salaam jana,  Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alisema mabadiliko hayo yanaendana na matakwa ya utaratibu mpya wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka yanayotarajiwa kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwaka huu. “Patakuwa na mabadiliko ya njia na alama mpya ambavyo vitapaswa kufuatwa na kuheshimiwa na madereva wote wa magari na vifaa vingine vya moto,” alisema Silaa.

Alisema mbali na kuhakikisha utaratibu wa mabasi yaendayo haraka unatekelezeka ipasavyo na kwa ufanisi, mabadiliko hayo pia yanalenga kimsingi kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji.

Kadhalika, alisema mabadiliko yanalenga kuongeza ufanisi wa ufanyaji kazi wa mabasi ya daladala na kutoa nafasi kwa baadhi ya eneo la barabara ya Morogoro kubakia kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka na waenda kwa miguu tu.

Kuhusu mabadiliko hayo, mwakilishi wa Halmashauri ya Ilala kwenye mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT), Mhandisi Tigahwa Serapion, alisema mabasi yote yanayopita barabara ya Kilwa yataishia Stesheni na kurudi kupitia njia hiyo hiyo, huku yale yanayopita barabara ya Nyerere na Uhuru yataishia kituo cha Mnazi Mmoja na kurudi kupitia njia zao.

Pia kutakuwa na mabasi yatakayoanzia Mnazi Mmoja kupitia njia ya Bibi Titi, Maktaba hadi kituo cha Posta ya zamani Benki ya NBC na kurudi kupitia njia hiyo hiyo. 

Serapion alifafanua kuwa mabasi yote yanayopita barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kuelekea katikati ya Jiji yataishia katika kituo cha YMCA barabara ya Upanga na kurudi kupitia njia hiyo hiyo.

Alisema pia barabara ya Sokoine zitaruhusiwa gari binafsi kupita kuanzia Kituo Kikuu cha Polisi kuelekea Kivukoni, Hospitali ya Ocean Road hadi kwenda kuungana na barabara nyingine ikiwamo ya Ali Hassani Mwinyi.

Kuhusu barabara ya Samora, badala ya kwenda hadi Hosptali ya Ocen Road, sasa gari ndogo binafsi zitaanzia katika hospitali hiyo kwenda Mnara wa Saa (Clock Tower).

Alisema njia zote za mabasi hayo ya daladala hazitakatiza katika barabara ya maradi wa BRT isipokuwa yale yanayotoka Mnazi Mmoja kwenda Posta ya Zamani.

Alisema alama zitawekwa kuonyesha njia hizo zitakavyokuwa na namna mabasi yanayotoka Mnazi Mmoja yatakavyokatiza katika barabara ya mradi huo wa mabasi.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa