Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru vigogo saba wa
Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) baada ya kuwaona
hawana hatia katika mashtaka saba yaliyokuwa yakiwakabili ya kula njama
na matumizi mabaya ya madaraka.
Vigogo walioachiwa huru jana na Hakimu Mkazi,
Aloyce Katemana ni Kanali Ayoub Mwakang’ata, Luteni Kanali Mkohi
Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajenti John
Lazier, Meja Yohana Nyuchi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta, Luteni
Kanali Felix Samillan.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Katemana alisema
amepitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashtaka,
vielelezo 25 vya ushahidi walivyoviwasilisha na ushahidi wa upande wa
utetezi ulitolewa na washtakiwa, mashahidi wao tisa pamoja na vielelezo
vitano na kwamba hakuna ubishi kuwa washtakiwa hao walikuwa wajumbe wa
bodi ya Suma JKT pia wakurugenzi wa Bodi ya Takopa na watia saini wa
kampuni hiyo walihamisha Sh3.8 bilioni kutoka Takopa kwenda Suma JKT kwa
kufuata taratibu zote zilizowekwa na wanahisa hao kupitia nafasi zao.
“Hili shtaka la matumizi mabaya ya madaraka ni
lazima lionyeshe lengo la kujipatia faida au manufaa, si tu kutekeleza
sheria, kwa maana hiyo Mahakama hii kwa kulinganisha ushahidi uliotolewa
na mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi, unathibitisha mashtaka
yao hayawezi kusimama,” alisema Hakimu Katemana.
“Kwa kuwa walitekeleza majukumu yao kama watia
saini wa Kampuni ya Takopa licha ya kuwa ni wajumbe wa bodi ya Suma JKT
na hakuna kinachoonyesha kuwa walipata manufaa ya aina yoyote ile,
hawana hatia na Mahakama inawaachia huru.
Julai 2, 2012, Mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dominsian Kessy na Ben Lincoln
waliwafikisha washtakiwa hao mahakamani kwa mara ya kwanza wakidaiwa
kutenda makosa hayo.
Walidaiwa kutumia vibaya madaraka yao kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya 2007.
Wakili Kessy alidai kuwa Machi 5, 2009 katika
chumba cha mikutano cha Ofisi ya Suma – JKT, wakiwa wajumbe wa Bodi ya
Tenda ya shirika hilo, kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa
kutoa uamuzi wa bodi hiyo ambao ulionyesha kuwa umetolewa na Takopa kwa
madhumuni ya kununua magari na vifaa vya ujenzi bila kupata idhini ya
kutoka Bodi ya ya Wakurugenzi ya Takopa.
Alidai kuwa Machi 12, 2012 washtakiwa hao
walitumia vibaya madaraka kwa kupitishia maazimio ya kununuliwa kwa
magari na vifaa vya ujenzi ambavyo vilikuwa vimeshatumika kinyume na
Kifungu cha 58( 3) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2005.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment