Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SWALA YAVUNA WANAHISIA KIBAO

SWALA YAVUNA WANAHISIA KIBAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Kampuni ya Swala Energy inayoshughulikia mafuta na gesi imeuza hisa zake zote milioni 13.3 ilizoziingiza kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya kupata wanunuzi wengi kuliko ilivyotarajiwa licha ya njama zilizoonekana kutaka kuikwamisha kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Aidha, kutokana na zoezi hilo, sasa kampuni hiyo imefanikiwa kuwa na wanahisa wa zamani na wapya wanaofikia 1,869.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kupitia kwa mkurugenzi mtendaji wake, Dk. David Ridge, kampuni hiyo ilisema kuwa mwitikio  wa Watanzania ulikuwa mkubwa kuliko.

“Ofa ya awali kwa umma (IPO) imepata wateja wengi ambao wamenunua hisa zaidi ya kiwango kilichokuwa kimewekwa,” alisema.

Alisema ofa hiyo ililenga kutoa fursa ya kuwanufaisha Watanzania wote walioko ndani na ughaibuni na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Hisa (CMSA) iliruhusu watu wajiunge kwa wingi, ikiwamo kupitia njia ya maombi iitwayo 'green shoe option'.

Kwenye taarifa hiyo, Dk. Ridge alisema kipengele hicho kinamruhusu mtoa hisa kutoa hisa zaidi ya kiwango cha makubaliano ya awali.

Alisema mafanikio haya ambayo ni ya kwanza katika sekta ya mafuta na gesi ni ushahidi tosha unaoonyesha kuwa wawekezaji wa Kitanzania wana hamu na uwezo wa kushiriki kabisa kwenye ujenzi wa utajiri unaombatana na maendeleo ya maliasili za nchi.

Alisema wanategemea ufanisi iliyoupata kampuni ya Swala katika nyanja hiyo kuboreka zaidi kama kampuni nyingine zitatoa fursa ya kuwashirikisha wawekezaji wa ndani.

Mafanikio haya ya kampuni ya Swala katika kuziuza hisa zake zote ilizoziingiza kwenye soko la hisa na mitaji Juni 9 mwaka huu hadi Julai 4 mwaka huu yamezima jitihada zilizofanywa na TPDC katika kuirudisha nyuma, hasa kutokana na tahadhari iliyotoa kwa umma kuhusiana na mauzo hayo.

Mwezi uliopita, TPDC ilitoa tahadhari kwa wananchi kuwafahamisha kuwa taarifa ya kwamba kampuni ya Swala imegundua gesi na mafuta katika maeneo ya Morogoro na Kilimanjaro haikuwa sahihi.

Aidha, mbali na TPDC kuwa na taarifa ya kampuni ya Swala kuwa na nia ya kuuza hisa zake katika soko la Hisa la Dar es Salaam ili Watanzania washiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, bado ilitoa msimamo ulioonekana ‘kuzinanga’ juhudi hizo.

“Suala la kampuni ya Swala kuuza hisa zao ni jema, lakini TPDC linawashauri wananchi wafanye maamuzi mazuri na kuwatumiwa washauri wao kuhusu ununuzi wa hisa hizo kwa kuzingatia mambo yaliyoelezwa hapo juu,” TPDC ilisema.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa