Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » AIBU YA SAMAKI WA MAGUFULI IWE FUNZO GANI KWETU

AIBU YA SAMAKI WA MAGUFULI IWE FUNZO GANI KWETU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi (wakati ule), Dk John Magufuli alipokamata meli yenye jina la Tawaliq 1 mwaka 2009, ilionekana kama vile tumepiga hatua kubwa katika kulinda rasilimali zetu. Iikuwa ni kazi nzuri aliyoifanya Dk Magufuli (sasa Waziri wa Ujenzi) mara baada tu ya kuhamishiwa wizara ile ya vitoweo, lakini sasa kesi hiyo imetupwa na Serikali inatakiwa iwarejeshee Wachina hao pasi zao za kusafiria na meli yao inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh3.3 bilioni.
Meli hiyo iliyokuwa na tani 293 za samaki aina ya jodari waliovuliwa katika ukanda wa kiuchumi wa Tanzania bila kibali, sasa imeshazama baada kukatwa mabati yake na kuibwa vifaa huku Serikali ikigawa bure shehena ya samaki hao.
Hapa ndiyo najiuliza naomba wanasheria wanisaidie. Ilikuwaje watu waliovua samaki kwenye eneo la Tanzania bila kibali, leo hawana kesi ya kujibu?
Miaka yote mitano waliyokamatwa, wanasheria wa Serikali hawakujua kwamba hakuna kesi?
Hayo tisa, kumi ni ile meli waliyokamatwa nayo iko wapi? Maana yake ni kwamba sasa Serikali imepoteza kesi, halafu ilipe Sh3.3 bilioni? Hii ni kashfa kubwa mno kwa Serikali na inaniwia vigumu mno kuamini umakini wa Serikali yetu.
Hii siyo kesi ya kwanza ya Serikali kupoteza, kwani ni mwaka huu tu Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) ilipoteza kesi dhidi ya Kampuni ya Atom Red Met Zoloto (ARMZ) ya Urusi inayokusudia kuchimba madini ya urani nchini siku za usoni.
Baada ya kupoteza katika kesi hiyo, TRA walikosa Sh340 bilioni za kodi ya ongezeko la mtaji. Yaani, kama nchi tumepoteza kiasi hicho cha fedha wakati madini ni yetu, na yalishagunduliwa na Serikali tangu miaka ya 1970, kisha leseni ya ugunduzi wa madini hayo ikapewa kampuni ya kigeni kwa bei ya kutupa.
Hapohapo kuna zaidi ya Sh200 bilioni zimepotelea kwenye sakata jingine la IPTL ambapo viongozi wetu wanadai siyo za Serikali huku upande mwingine ukidai ni za Serikali.
Ilimradi tu kila siku Serikali inapoteza mabilioni ya fedha, iwe ni kwenye kesi au wizi. Yaani, nchi hii imekuwa ya wapiga dili.
Watendaji wengi wa Serikali siyo waaminifu, kibaya zaidi hakuna wa kuwawajibisha. Kwa upande mwingine wapo watendaji wengine waaminifu, ila hata wakitoa ushauri kwa Serikali haufuatwi.
Hata ukifuatilia miradi mingi ya maendeleo utakuta fedha zinazotumiwa ni za wafadhili, siyo fedha za Serikali, wakati kuna uwezekano mkubwa tu wa kuzalisha fedha nyingi na zikaingizwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kwa ufupi, nchi yetu inaelekea kubaya. Tunaweza kujifariji tu kwa maendeleo kidogo tunayoyaona tena kwa fedha za misaada, lakini uhalisia ni kwamba hali tuliyonayo kama Taifa ni mbaya na inatia aibu.
Yote haya yanasababishwa na kukosekana kwa uadilifu hasa kwa watendaji wa Serikali.
Viongozi walio wengi wanapopata fursa badala ya kuangalia masilahi ya Taifa, wanaangalia manufaa yao na kuhakikisha wanabadili maisha yao na siyo ya wananchi.
Ni jukumu la watendaji wa Serikali sasa kurejesha uadilifu huu, vinginevyo nchi yetu inazama na kupotea kabisa.
Chanzo;Mananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa