Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Pia mahakama hiyo imeamuru vyombo vya dola kuacha
kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani kusikiliza kesi zake, na
kushauri kama wana wasiwasi nao, waweke mashine za ukaguzi katika mlango
wa kuingilia mahakamani hapo.
Mwenendo huo wa Sheikh Ponda ulihojiwa mahakamani
hapo na Jaji Augustine Shangwa juzi kabla ya kuanza kusikiliza rufaa
yake ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia
hatiani katika kesi ya jinai, mwaka 2012.
“Sheikh Ponda, sijui ni kwa nini una kesi nyingi
kiasi hiki. Kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi (Kisutu) una kesi, Mahakama
Kuu una kesi. Nani yuko nyuma ya kesi zako? Je! Serikali inakuchukia?”
alihoji Jaji Shangwa.
Licha kumhoji Sheikh Ponda maswali hayo,
alimweleza kuwa kama atakuwa na jambo la kuzungumza, atampa nafasi siku
nyingine rufaa yake itakapotajwa. Pia Jaji Shangwa alimshauri apunguze
mapambano.
“Ikiwezekana uyapunguze (mapambano) maana dunia
hii si ya kupambana nayo,” alisema Jaji Shangwa na kusisitiza kuwa
lazima ajiulize kwa nini ana kesi nyingi.
Jaji Shangwa aliendelea kusema: “Jambo likitokea
Zanzibar, wewe umo; likitokea Morogoro umo; likitokea Dar es Salaam umo.
Bahati mbaya kuna kikundi cha Uamsho kinadaiwa kulipua mabomu na kuua
watu, nasikia na wewe unatajwa kuhusishwa.”
Hata hivyo baadaye Jaji Shangwa alimuuliza Ponda kama ana la kueleza kuhusu wingi wa kesi zinazomkabili.
Sheikh Ponda alidai kuwa kesi hizo ni mzigo
anaotwisha kutokana na kutetea kile alichokiita masilahi, huku
akijitetea kuhusu hukumu ya kesi iliyomtia hatiani ambayo amekata rufaa
kuipinga, akieleza kuwa eneo analodai kuvamia ni mali ya Waislamu.
Hata hivyo, Jaji Shangwa alimkata kauli akisema
anayoyaeleza yanapaswa kusemwa na mawakili wake katika rufaa hiyo kama
alikuwa na hatia au la. Alimtaka aeleze ni kwanini anakabiliwa na kesi
nyingi.
Hata hivyo, wakili wake Juma Nassoro alisimama na
kuieleza Mahakama kuwa si kwamba mteja wake ana kesi nyingi, bali
anakabiliwa na kesi mbili tu moja iliyokuwa Mahakama ya Kisutu ambayo
ndiyo wameikatia rufaa na ile iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Awali, wakati akivipiga ‘stop’ vyombo vya dola
kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani, Jaji Shangwa alisema: “Huyu
Sheikh Ponda ana wafuasi wengi, wanahitaji kuja kusikiliza kesi yake.
Vyombo husika visiwazuie, waacheni waje wasikilize kesi ya Sheikh wao.”
Pia aliwaonya wafuasi hao kuacha mapambano na vyombo vya dola
“Mnaweza kuona kama vile Sheikh wenu anasulubiwa lakini hapa
hasulubiwi bali haya ni mashtaka ya kawaida tu ambayo anatakiwa
kuyajibu,” alisema.
Kuhusu rufaa yake, Jaji Shangwa aliamua isikilizwe
kwa njia ya maandishi na pande zote, mrufani (Ponda) na mjibu rufani
(Jamhuri) watawasilisha hoja zao za rufaa na majibu ya hoja hizo kwa
njia ya maandishi na kisha kusubiri hukumu.
Katika rufaa hiyo, Ponda anadai hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Katika kesi ya msingi, Ponda na wenzake walikuwa
wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh
59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali
eneo la ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd, na uchochezi.
Katika hukumu yake ya Mei 9, 2013, Hakimu Mkazi
Victoria Nongwa wa Mahakama ya Kisutu alimtia hatiani Ponda peke yake
kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la Agritanza Ltd, lakini
ikawaachia huru washtakiwa wengine wote.
Licha ya kumtia hatiani Ponda, mahakama hiyo ilimwachia huru kwa masharti ya kutotenda kosa lolote katika kipindi cha miezi 12.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment