Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BENKI
ya Posta Tanzania (TPB) kwa kushirikiana na mfuko wa pensheni wa LAPF
wamezindua mpango maalum wa kutoa mikopo kwa wanachama wastaafu wa mfuko
huo.
Akizungumza Dar es
Salaam jana Waziri wa kazi Ajira na Vijana Gaudensia Kabaka mara baada
ya uzinduzi huo, alisema lengo ni kuwasaidia wastaafu katika kukidhi
mahitaji yao na maslahi yao kwa ujumla.
Alisema upatikanaji wa
fedha hizo kwa wastaafu utawawezesha kumudu gharama za mahitaji muhimu
ya muda mfupi na mrefu ambayo ni endelevu kama tafiti mbalimbali
zinavyoonesha kwa wastaafu waliotangulia.
"Napenda kuwasisitiza
wastaafu wenye sifa za kuomba mikopo hii wajitokeze kwa wingi kutumia
fursa hii kujiendeleza kimaisha hivyo mikopo hii ikitumika vizuri
itakuwa ndiyo chachu ya maendeleo kwa wastaafu kuishi maisha ya
faraja,"alisema Kabaka.
Aliwataka wastaafu
kukopa kwa sababu maalum ili kuepuka matumizi mabaya ambayo yatapelekea
kuwa na uwezekano wa msongo wa mawazo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa (TPB) Sabasaba Moshingi,alisema lengo ni
kuwezesha wastaafu kukidhi mahitaji halisi ya fedha na hatimaye
kuboresha maisha yao.
Alisema miongoni mwa
mahitaji makubwa ya fedha kwa wastaafu ni pamoja na gharama za matibabu,
ada za shule, kuendesha biashara na miradi mbalimbali.
Pia alisema kwa muda
mrefu taasisi mbalimbali zimekuwa hazitoi mikopo kwa wastaafu wakidhani
hawana uwezo wa kulipa na kujenga dhana ya kutokopesheka.
"Kwa kuliona hili na
kutambua mchango wa wastaafu TPB kwa kushirikiana na LAPF wamebuni
mpango huu wa kipekee nchini wa kuwakopesha wastaafu wa mfuko
huo,"alisema Moshingi.
Hata hivyo alizitaka
taasisi nyingine za fedha kuangalia namna ya kuweka mipango ya kusaidia
wastaafu hapa nchini ambao kwa ujumla wana kiasi kikubwa cha fedha
ambacho kikitumiwa vyema kinaweza kuleta mchango mkubwa katika uchumi wa
nchi.
Alisema mstaafu anayetaka mkopo hatahitaji kuwa na dhamana na riba inayotozwa kwa mkopo mdogo ukilinganishwa na mikopo mingine.
Alisema mkopo huo
umewekewa bima hivyo endapo mkopaji atafariki familia yake haitaendelea
kudaiwa, hivyo wastaafu wa LAPF wanaweza kupata mikopo ambayo marejesho
yake ni kati ya mwaka mmoja hadi miaka mitatu.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment