Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » WAMACHINGA KUMVAA MEYA SILAA KWA MAANDAMANO

WAMACHINGA KUMVAA MEYA SILAA KWA MAANDAMANO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Meya wa Manispaa ya Ilala,Jerry Silaa.
Wafanyabishara soko la Machinga Complex, jijini Dar es Salaam, wamejipanga kufanya maandamano makubwa mpaka katika ofisi ya Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, wakimtaka awalipe Sh. milioni 250, walizopewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha daladala mtaa wa New Kisutu vinginevyo kutamburuza mahakamani.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Abubakari Rajeshi, katika mkutano uliowakutanisha wafanyabiashara wa soko hilo.

Alisema wazo lao la kujenga kituo cha daladala hapo ‘New Kisutu’ ni lengo la kujiongezea mapato na kwamba fedha zingine zingetumika kwa ajili ya kulipia ushuru wafanyabiashara  katika soko hilo.
“Tunafanya maandamano kesho kutwa (leo), mpaka ofisini kwake kumshinikiza atupe fedha zetu na kama atashindwa tutamburuza mahakamani,’’alisema.

Aliongeza kuwa Silaa ni kikwazo cha wao kutoendelea na iliishafikia hata kutoa maoni yake katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa jengo la Machinga halijajengwa kitaalamu na haliwezi kuwasaidia wafanyabiashahara kunufaika nalo.

Aliongeza kuwa Silaa anawadhalilisha hata viongozi wake walioona kuwepo wa jengo hilo wakati ni moja ya kuwasaidia wafanyabiashara kunufaika nalo na kuachana na tabia ya kufanya biashara pembezoni mwa barabara huku wakikimbizana na polisi na kuchukuliwa mali zao.

Alisema kuwa, pamoja na kukutana na changamoto mbalimbali katika kazi zao, walifunga safari hadi Dodoma na kufanikiwa kuzungumza na Waziri Mkuu ili awapatie fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha daladala na akawaahidi kuwapatia Sh. milioni 250.

Alisema waliporudi Dar es Salaam ndipo Waziri Mkuu aliwaambia kuwa fedha hizo alikabidhiwa Katibu Mkuu wa Tamisemi, Jumanne Sagini, na kuwa zimeisha pelekwa ofisi ya Meya wa Ilala kwa ajili ya kuanza matengenezo ya kituo cha daladala.

“Jamani cha kushangaza tumefuatilia fedha hizo mpaka tumechoka na majibu kuwa fedha hizo zimetumika katika matumizi mengine, sisi hatuyajui hayo matumizi mengine, tunafanya maandamano makubwa mpaka katika ofisi yake Silaa kumwambia atupe fedha zetu na akishindwa kutulipa tutamfikisha mahakamani kwa sababu tumeishaanza kufanya mawasiliano na wanasheria wetu,’’ alisema.

Pia, alidai kuwa Silaa, bila uwoga aliidanganya Tamisemi kuwa ameshaziondoa gereji bubu katika eneo hilo ambalo lilitengwa rasmi kama sehemu maalumu ya kituo cha daladala cha Machinga Complex,  wakati anajua fika kuwa zoezi hilo halijafanyika.

NIPASHE ilipomtafuta Silaa  kwa njia ya simu ili kujibu tuhuma hizo dhidi yake, alipokea simu na alipoulizwa madai hayo wafanyabiashara alijibu kuwa atapiga simu muda si mrefu kutokana na shughuli aliyokuwa akiifanya.

“Nitapiga simu baadaye kuna mambo nafanya,” alisema. Hata hivyo, baada dakika 40, mwandishi alimtafuta tena , lakini hakupokea simu na kisha kuizima.

Soko hilo lina vizimba 4,500 vya wafanyabiashara, lakini kutokana na mzunguko wa biashara katika eneo hilo hususani wafanyabiashara wadogo kushindwa kuendesha biashara zao hapo limejikuta likimiliki wafanyabiashara hai chini ya 1,000.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa