Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » LOWASSA AMUOMBEA RADHI SITTA KWA KANISA

LOWASSA AMUOMBEA RADHI SITTA KWA KANISA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Wakati Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (MBK) ikitarajia kuingia katika hatua ya kura ya maoni mwakani, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameibuka na kuliomba radhi Kanisa Katoliki kufuatia mgongano iliyojitokeza kati ya kanisa hilo na baadhi ya viongozi serikali na wa Bunge hilo.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliomba msamaha huo wakati akitoa salamu zake katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge, mkoani Morogoro.

Alisema Kanisa Katoliki lina mchango mkubwa katika kudumisha amani na mshikamano nchini, hivyo mambo yaliyojitokeza yanapaswa kusamehewa.

“Najua hivi karibuni tumewaudhi, lakini mimi naomba mtusamehe bure tu, kama vile mzazi anavyomsamehe mtoto wake anapokosea,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa Kanisa Katoliki ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

Ingawa Lowassa hakueleza kwa undani tofauti zilizojitokeza kati ya Kanisa hilo na baadhi ya viongozi wa serikali, lakini  wakati BMK likiendelea, taasisi za dini zilisambaza waraka uliosainiwa na viongozi wake ukilikosoa Bunge hilo kwa mambo mbalimbali ikiwamo kuendelea kujadili rasimu bila maridhiano kutokana na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia.

Kadhalika, viongozi wa madhahebu hayo ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT) na Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), walilikosoa BMK kwa kupuuza maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Waraka huo ulisababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kujiweka katika wakati mgumu kwa kuzua mgogoro dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo, baada ya kuita waraka huo kuwa ni wa kipuuzi na wa hovyo hovyo.

Sitta ambaye alitoa kauli hiyo Oktoba Mosi mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa waraka wa maaskofu una lugha ya Ukawa, ingawa maaskofu kwa upande wao waliueleza kuwa ni waraka wa kinabii, kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.

Sitta alitoa kauli ya kuuponda waraka huo bungeni alipokuwa akielezea mwenendo wa upigaji kura za kupitisha ibara na sura za rasimu ya katiba iliyopendekezwa kabla ya upigaji wa kura na wakati wa kutangaza matokeo, akisema watu wa Mungu kama maaskofu hawawezi kutoa waraka kama huo na kudai kuwa amekuwa akituhumiwa kwenye mitandao kwamba anadharau maaskofu.

“Nimalizie na viongozi wangu wa kiroho…mababa zangu maaskofu, natuhumiwa sana kwenye mablog kwamba nadharau maaskofu. Wakiwa na matendo kama hayo hao baadhi ya maaskofu itabidi tuendelee kuwadharau,” alisema na kuongeza:

“Ninao waraka huu ambao umelazimishwa kutumwa katika makanisa. Sioni utukufu wa Ukristo katika waraka huo. Huu waraka unamwamuru Rais airudishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba.”

 Kuna Ukristo hapa?” alihoji na kuendelea: “Waraka huu unamlazimisha Rais asitishe mchakato wa Bunge Maalum…tangu lini watu wa kiroho wanatoa maagizo ya kisiasa? Hii sio haki hata kidogo…kuna Ukristo hapa? Waraka una lugha za wale Ukawa tuliowazoea.”

“Hivi kweli maaskofu wa Kikristo wanaweza kusema kwamba Wizara ya Katiba na Sheria irudishe tovuti ya Tume ya Jaji Warioba na kuirejeshea nyaraka zake zote ili wananchi wasome na kujifunza?” alihoji Sitta.

“Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauriwa na chama tawala, hivyo basi Bunge la Katiba lijadili na kuboresha tu rasimu ya katiba na si kubadilisha,” alisema Sitta.

“Waraka huu kwa shinikizo la maaskofu umesambazwa kwenye makanisa na kusomwa. Mimi nasema kama Mkristo, tukianza kuruhusu nchi yetu kutoa nyaraka hizi za kisiasa zisomwe makanisani kwa kudai huo ni msimamo wa maaskofu, basi nchi hii tutaipeleka kubaya.

“Na mini kama mtu mzima lazima nionye kuhusu tabia hii, ukizingatia nchi hii haina dini, hawa baadhi ya maaskofu ambao walikusanywa Dar es Salaam na makundi yale yale yanayohusishwa na Ukawa, kama wao ni wanachama wa siri wa vyama vya siasa vinavyochukia CCM wajitokeze waziwazi,” alisema Sitta.

Sitta aliendelea kunukuu waraka huo kwamba kuna askofu mmoja ameapa kwamba atawaelimisha waumini wake ili siku za usoni wawashughulikie viongozi kama mimi (Sitta). Nasema aendelee, lakini Mungu anaona yote yaliyo moyoni mwetu.”

Baada ya Sitta kutoa kauli hiyo, Askofu wa Jimbo la Katoliki la Bunda, Mhashamu Renatus Nkwande, alisema matamshi ya Sitta yanaonyesha anavyohangaika kualalisha kilicho haramu.

Alisema kitendo cha Sitta kuendesha BMK kwa kukejeli wajumbe wenzake walioondoka bungeni (Ukawa) na wajumbe walioandaa rasimu ya pili kwenye Tume ya Katiba Mpya chini ya Jaji Joseph Warioba, ni jambo la aibu ambalo halivumiliki, na ndiyo maana walitoa waraka wa kutokubaliana nacho.

“Kwa kweli Sitta ametutukana, ametafuta ubaya kwa viongozi wa dini, kwa kuwa tumesema ukweli ? Sisi tulikuwa tunatimiza wajibu wetu kwa Wakristo …tulizungumza kutokana na hitaji la wakati, na ulikuwa waraka wa unabii,” alisema.

Viongozi wengine wa kanisa Katoliki waliojibu kauli za Sitta ni Makamu Mwenyekiti wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, ambaye alinukuliwa akisema kuwa Sitta amelewa madaraka.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa