Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MSUYA:KESI ZA EPA ZIHARAKISHWE

MSUYA:KESI ZA EPA ZIHARAKISHWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399
.

Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, ameeleza kusikitishwa kwake na ucheleweshwaji wa kutoa hukumu katika kesi za wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT).

Mzee Msuya alisema inasikitisha kuona kesi hizo zinazohusu wizi wa takriban Sh. bilioni 133, zinakaribia kuchukua miaka 10 bila kuhukumiwa.

Kampuni 23 zinadaiwa kuchota fedha hizo katika akaunti hiyo na iligundulika baada ya ukaguzi wa hesabu uliofanywa na kampuni ya kigeni ya Ernst & Young mwaka 2005/2006, ambayo ilipewa kazi iliyoachwa na Deloitte & Touche ya Afrika Kusini.

Kesi zinazohusu wizi katika Epa zilifunguliwa mwaka 2009 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Hadi sasa tayari kesi tatu zimekwishakutolewa hukumu.

Alisema mahakama nchini zinashindwa kuendesha kesi haraka na kuvishauri vyombo vya usalama kufanya kazi zake bila kumwogopa mtu yoyote.

Msuya alisema hayo jijini Dar es Salaam juzi usiku katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV. 

“Likitokea jambo lichunguzwe haraka. Hatua zichukuliwe na watu waone hatua zimechukuliwa. Kama mahakama haiwezi kutoa hukumu haraka haraka, zianzishwe mahakama kama za kijeshi kama wanavyofanya nchi nyingine,” alisema Msuya.

Alisema kwa sasa kunahitajika kuwapo na sheria zitakazowabana viongozi watakaokwenda kinyume cha sheria za nchi, hususan watakaobainika kufuja mali za nchi.

Mzee Msuya alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, watu wanaiba fedha katika benki kwa kutumia mitandao, hivyo, akashauri polisi na wahusika wa benki kuelimishwa na kujua mbinu hizo.

Alisema lazima kuwapo na mipaka na vyombo vya kusimamia sheria, ambavyo vitakakuwa imara pasipo kuyumbishwa.

Aliwashauri viongozi wa serikali kutenganisha shughuri za biashara na utumishi wa umma.

“Kuna baadhi ya viongozi wanatumia vyeo vyao kujinufaisha na masuala yao binafsi. Hivyo, itungwe sheria itakayotenganisha madaraka na umiliki mali,” alisema Msuya.

Aliongeza: “Utakuta mtu ni mkuu wa mkoa, halafu wakati huo huo unasikia yupo katika masuala fulani ya kibiashara. Sasa inatakiwa ukiwa kiongozi, basi uachane na mambo mengine.”

Pia alivitaka vyombo vingine vya kutoza kodi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha taasisi na viongozi wa serikali wanalipa kodi ipasavyo.

Alisema kumekuwapo na madai kuwa baadhi ya vigogo serikalini na wafanyabiashara wameficha fedha nje ya nchi na kusema unahitajika uchunguzi wa tuhuma hizo.

Alishauri Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya upelelzi nchini kupewa mafunzo ya kiuchunguzi yatakayowawezesha kubaini watu wanaoficha fedha nje ya nchi. 

Kuhusiana na upatikanaji wa gesi na mafuta nchini, Mzee Msuya alisema lazima kuwapo na viongozi imara na waadilifu watakaoweza kusimamia nishati hiyo ili iwanufaishe wananchi na Taifa.

Alisema ikiwa viongozi hao hawatasimamia vizuri rasilimali hiyo, wanaweza kulipeleka Taifa katika machafuko.

Mzee Msuya alisema hiyo ni kutokana na wachache kuiba fedha za mapato ya rasimimali hiyo na kushauri watakaofanya hivyo wachunguzwe na fedha walizotorosha zirejeshwe.

Alisema ikiwa serikali itashindwa kufanya uchunguzi, iajiri wataalamu kutoka nje kuja kufanya kazi hiyo.Alitolea mfano wa nchi ya Nigeria, ambayo ilitumia wataalamu wa uchunguzi na kufanikiwa kukamata fedha zilizotoroshewa nje na kuzirudisha.

“Kwa mfano, Nigeria, kuna kipindi viongozi waliiba fedha zilizotokana na mafuta na kuzificha Ulaya, lakini waliweza kuwabaini na kuzirudisha pesa hizo. Sasa serikali yetu inapaswa kuiga hilo, siyo kuongea ongea kuwa kuna viongozi wameficha pesa ulaya,” alisema Msuya.

Alisema kuitawala nchi ya watu waliosoma ni kazi kubwa kuliko kuitawala ya watu, ambao hawajasoma.Alitoa mfano kwa Uingereza na Marekani kuwa zina wasomi wengi na ndiyo sababu ni vigumu kutawaliwa.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusiana na changamoto za uongozi, kuanzia awamu ya kwanza na zilizofuatia.Alisema serikali kwa sasa ina changamoto kubwa ya kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja wakati uchumi wa nchi unakua kwa kasi.

Msuya alishauri kuwa ili kuondokana na tatizo hilo, serikali inapaswa kuwawezesha wananchi katika sekta ya kilimo, kuongeza fursa za ajira na uwekezaji katika viwanda.
Alisema nchi kwa sasa inahitaji kiongozi mahiri atakayeweza kufufua na kufungua njia za usafirishaji, zikiwamo sekta ya reli, bandari na anga.

Msuya alisema nchi ina matatizo ya upatikanaji wa umeme, hivyo rais ajaye ana kazi ya kuhakikisha kuna upatikanaji wa nishati hiyo katika kila eneo la nchi.

“Kilimo kinahitaji kupanuka, utalii, watu wapate ajira, uchumi uongezeke kama usipopanuka nchi inaweza kuingia kwenye matatizo kama Misri, asimamie rasilimali za nchi, gesi na mafuta pia,” alisema.

Alipoulizwa viongozi wastaafu kama yeye kukaa kimya bila kukemea mambo yasipoenda sawa.Alisema wanatoa ushauri kwa sehemu husika na kwamba, hata mchakato wa kupata rais ajaye watatoa ushauri wao nje ya mfumo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa