Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MBEGU ZA KIUME ZA MWENYE VVU ZAOSHWA ZATUMIKA KATIKA UZAZI

MBEGU ZA KIUME ZA MWENYE VVU ZAOSHWA ZATUMIKA KATIKA UZAZI

 Hakika teknolojia inazua mengi, hata yale ambayo hayakuwahi kufikiriwa na mababu zetu karne nyingi zilizopita.
Hivi karibuni, wanasayansi wameweza kugundua namna ya kuzisafisha mbegu za kiume za mtu mwenye virusi vya Ukimwi na kuondoa virusi hivyo ili kumwezesha kutungisha mimba bila kumwathiri mwenza wake.,
Hii ni kwa wenza ambao mwanamume anaishi na VVU na mwanamke akiwa hana virusi hivyo.
Programu hiyo maalumu ijulikanayo kama SPAR, ilibuniwa ili kuwasaidia wenza hao kupata mtoto bila kumwambukiza mama na mtoto ambao mwanamume anaishi na VVU aweze kuzalisha.
Inafanyikaje?
Kisayansi, damu pekee si kipimo cha kuonyesha kuwepo kwa maambukizo ya VVU katika mwili bali hata katika majimaji ya mwilini.
Ogani zinazozalisha majimaji ya mbegu za kiume huathiriwa kwa namna ya pekee na VVU.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa magonjwa, Henry Mwakyoma anasema kwa kawaida Virusi vya Ukimwi hupenda kukaa katika chembehai nyeupe(CD4).
“Kwa kawaida VVU haviishi katika mbegu za kiume. Lakini hupendelea zaidi kukaa katika CD4 au chembehai nyeupe za damu ambazo zipo katika damu na katika majimaji ya mbegu za kiume au semen,” anasema.
Anasema ndiyo maana inawezekana mwanamume mwenye VVU asimwambukize mwenza wake.
“Kama hana michubuko mwanamke anaweza asipate maambukizo, kwa kuwa majimaji ya mbegu za kiume yanakosa mahali pa kuingia,” anasema.
Hata hivyo, Dk Mwakyoma aliona kuna ugumu kuzisafisha mbegu za kiume na kuondoa majimaji yake yenye VVU, ili kuzipandikiza mbegu hizo ili zitungishe mimba kama unavyosema utafiti huo.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Innocent Mosha anaungana na Dk Mwakyoma na kusema, kwa kawaida mbegu za kiume hazina VVU kwa sababu ni seli inayojitegemea lakini majimaji yanayobeba mbegu hizo ndiyo huwa na VVU.
Wanasayansi wanasema mwanamume anaweza asionyeshe VVU katika damu, lakini majimaji ya mbegu za kiume yakaonyesha uwepo wa virusi.
Wanaeleza kuwa lakini kwa mwanamume anayetumia dawa za kufubaza makali ya VVU, majimaji hayo yakipimwa hayaonyeshi uwepo wa VVU bali virusi huonekana katika damu tu. Hii ni kwa sababu ARV hupunguza wingi wa virusi na hivyo kushuka na kufikia kiwango cha kutoonekana.
Jarida la Science Daily la nchini Uingereza linasema robo tatu ya wanaume wanaoishi na VVU na wanaotumia ARV, walipopimwa majimaji yanayobeba mbegu za kiume hayakuwa na VVU.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa mwaka 2009 na Jarida la Tiba la nchini Canada ulibaini kuwa mbegu za kiume zina nafasi kubwa ya kusambaza virusi vya Ukimwi.
Utafiti huo ulikinzana na huu wa usafishwaji wa mbegu hizi kuondoa majimaji ambayo kwa kawaida ndiyo hudhaniwa kubeba VVU.
Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa mbegu za kiume zina nafasi kubwa ya kusambaza VVU wakati wa tendo la ndoa kwani virusi hivyo hujichimbia katika chembehai nyeupe ambazo utafiti ulisema ipo katika mbegu za kiume.
Utafiti huo ulikanusha tafiti za awali ambazo zinathibitisha kuwa ni majimaji tu yanayobeba mbegu hizo ndiyo yenye kuathiriwa na VVU.
Jinsi inavyofanyika
Programu ya SPAR huanza kwa kuwapa ushauri nasaha wenza. Kisha majimaji ya mbegu za kiume hupimwa iwapo yana virusi. Kipimo maalumu na makini cha PCR hutumika kuangalia uwepo wa VVU.
Utafiti wa taasisi ya Bedford unaonyesha kuwa asilimia 24 ya vipimo vya majimaji hayo yaliyotolewa kutoka kwa wanaume 262 ulionyesha uwepo wa VVU hata kama sampuli za damu hazikuonyesha VVU. Hii ilionyesha hakuna VVU katika majimaji hayo kwa kuwa walengwa walikuwa wakitumia ARV.
Kwa kawaida majimaji haya ni ya muhimu kwani ndiyo huzipa mbegu uhai na kuzilinda. Ndizo zinazosaidia mbegu kusafiri/kuogelea kwa urahisi hadi katika mji wa mimba.
Katika kusaidia uzalishaji huu, majimaji yenye mbegu hutenganishwa kwa kifaa maalumu na kuhifadhiwa.
Mahali zinapohifadhiwa mbegu, huwekwa majimaji ambayo huzipa uhai kama zinapokuwa katika korodani.
Baadaye, mbegu hizo huhifadhiwa na ili mama ashike mimba mchakato wa upandikizaji au In Vitro Fertilization (IVF) hufanyika.
Mwanamke hutakiwa kupimwa iwapo amepata maambukizo kwa bahati mbaya kila mara anapofanya majaribio ya upandikizaji.
Usafishaji huu wa mbegu za kiume unahusisha pia kuondoa uteute wa aina yoyote katika majimaji hayo. Pia katika usafishaji huu, magonjwa ya aina yoyote ya zinaa huondolewa ili kuondoa nafasi ya kuambukiza mama.
Inaelezwa kuwa hata kwa wanaume ambao bado wana idadi ndogo ya virusi (Viral load) kwenye damu bado VVU vinaweza kuonekana katika majimaji ya mbegu za kiume.
Hivyo basi, teknolojia hii ya usafishaji wa mbegu hizi ili kuondoa VVU, inahitajika zaidi kwa wenza ambao wanahitaji kupata watoto hasa pale mwanaume anapokuwa na VVU na mwanamke hana
Tangu Januari 2014, watoto 150 walizaliwa kwa kupitia programu hii. Miongoni mwao ni pacha 22.
Dk Athuman Mjombikisa, wa Hospitali ya Nyangao, Lindi anasema watafiti wamekuwa wakijaribu njia mbalimbali za kuwasaidia wenza wenye VVU kupata watoto bila mafanikio.
Akielezea teknolojia hii katika muktadha wa Tanzania, Dk Mjombikisa anasema bado ni vigumu wenza kukubali, pia watakaoweza ni wachache wenye kipato kikubwa.
Umuhimu wa majimaji ya mbegu za kiume
Kwa kawaida majimaji haya si mbegu za kiume. Lakini yana umuhimu mkubwa katika utengenezwaji na uhifadhi wa mbegu hizo. Majimaji haya husaidia mbegu kusafiri kwa urahisi hadi katika mji wa mimba.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa