Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MKATABA WASAINIWA MABASI YA KASI KUANZA

MKATABA WASAINIWA MABASI YA KASI KUANZA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 MIEZI imeanza kuhesabika kabla ya huduma ya usafiri kupitia mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam kuanza, baada ya mkataba kusainiwa kati ya serikali na wamiliki wa daladala kwa ajili ya kuendesha katika kipindi cha mpito.
Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imetia saini makubaliano ya uendeshaji na Kampuni ya Uda Rapid Transit kuendesha huduma ya usafiri huo katika kipindi cha mpito.
Kampuni ya Uda Rapid Transit imeundwa kwa pamoja baina ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (Uda) na wamiliki wa daladala. Kusainiwa kwa makubaliano hayo, kumeelezwa na serikali kuwa ni tukio la kihistoria katika mchakato wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka.
Mabasi yanunuliwa Katika mkataba huo wa miaka miwili, kampuni hiyo itatakiwa kununua mabasi 76 yenye urefu wa meta 12 na 18 kuanza kutoa huduma hiyo katika barabara za mradi jijini Dar es Salaam miezi minne kuanzia sasa.
Wakati Dart ikiwakilishwa na Mtendaji Mkuu wake, Asteria Mlambo, Kampuni ya Uda Rapid Transport iliwakilishwa na Robert Kisena na Sabri Mabruki. Walioshuhudia utiaji saini huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na viongozi wengine.
Tukio la kihistoria Akizungumza katika hafla ya utiaji saini jijini Dar es Salaam, Ghasia alisema tukio hilo ni la kihistoria katika mchakato wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka.
“Tumefikia hatua nzuri kwa nchi yetu kuwa serikali imeweza kushirikiana vyema na wadau binafsi wa usafiri kupata kampuni ya kuendesha huduma ya usafiri kipindi cha mpito,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba mradi mzima haujakamilika, serikali imeamua kuanza na huduma ya mpito katika barabara ya Kimara hadi Kivukoni ambayo imekamilika kwa asilimia 90 na kuwa sasa kazi inayofanyika ni ya kuweka taa za barabarani.
Alifafanua kuwa usafiri katika barabara hiyo utakuwa wa uhakika na wa kisasa kwa vile basi moja la urefu wa meta 18 litakuwa na uwezo wa kubeba watu 150 wakati ya meta 12 yatakuwa na uwezo wa kubeba abiria 80 kila moja.
Waziri Ghasia alitaka kampuni hiyo kuendelea kujenga mshikamano kupata uwezo wa kushindana katika zabuni ya kuendesha huduma ya kudumu ya mradi huo baada ya kipindi cha mpito kuisha.
Mwakilishi wa Uda Rapid Transit ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (Darcoboa), Mabruki alisema wamejipanga kutoa huduma nzuri ya usafiri katika kipindi cha mpito.
“Tunashukuru serikali kwa kutuwezesha wadau wa usafiri kufikia tulipo,” alisema. Mafunzo kwa madereva Alisisitiza kuwa katika kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa, kampuni yao itakuwa imeleta mabasi mawili yenye sifa zinazotakiwa kwa ajili ya kufundishia madereva na hadi kufikia Septemba 15, mwaka huu, mabasi yote 76 yatakuwa yameshaletwa.
Pia alisema kampuni yao inatarajia kujisajili katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kuwapa fursa wananchi kununua hisa katika kampuni hiyo na kuwa sehemu ya wamiliki.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki alisema mradi huo ni mkubwa hivyo wananchi pamoja na madereva wanatakiwa kuuthamini na kulinda miundombinu yake.
Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa