Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TAMASHA LA MWALIMU NYERERE LATOA ANGALIZO UKOLONI MPYA.

TAMASHA LA MWALIMU NYERERE LATOA ANGALIZO UKOLONI MPYA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwalimu Julius Nyerere.
Tamasha la Saba la Kigoda cha Mwalimu Nyerere (pichani), mwaka huu, limeibua mambo mengi kutokana na watoa mada kueleza vitendo vya kikatili yakiwamo mauaji wanayofanyiwa wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo ya migodi ya madini na wachimbaji wadogo wa rasilimali hizo katika nchi mbalimbali barani Afrika, Tanzania ikiwamo.
 
Wakitoa picha halisi ya vitendo vinavyofanywa na wawekezaji katika maeneo wanayotoka, watoa mada katika tamasha hilo linalotarajia kumalizika leo katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walisema, bado vitendo vya kikatili vinaendelea kufanywa dhidi ya wananchi waishio maeneo ya migodi ikiwa ni pamoja na kutopewa haki zao za msingi za kijamii, kunyanyaswa na kuuawa.
 
Pius Lugendo, kutoka eneo linalozunguka Mgodi wa dhahabu wa Geita, alisema, wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo wanaendelea kufanyiwa vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi wanapokuwa wakiokota mawe yaliyotupwa mbali na mgodi huo kwa ajili kuyaponda na kuyauza.
 
Alisema  wananchi 77 ambao waliondolewa katika eneo hilo kupisha uwekezaji, hadi leo hawajajengewa nyumba zao kama walivyoahidiwa badala yake wanaishi kwenye makapeti waliyopewa kama msaada kutoka kwa taasisi za kidini.
 
Kwa mujibu wa mzee Lugendo, wananchi 10 pekee ndiyo waliyojengewa nyumba kwa madai ya kuwazima midomo katika kuwatetea waliobaki.
 
Baadhi ya watafiti ambao walikuwa ni miongoni mwa watoa mada katika tamasha hilo la Kigoda cha Mwalimu Nyerere kutoka Uganda na Afrika Kusini, walisema vitendo wanavyofanyiwa wazawa wengi barani humo  kwa kutonufaika na utajiri wa rasilimali zilizopo kwenye nchi zao yakiwamo madini, vinaibua ukoloni mpya wa ukandamizaji, unyanyasaji na dhuluma kutokana na serikali  kukumbatia wawekezaji ambao ni wachache.
 
Akichangia mada kuu katika tamasha hilo ya ‘taswira ya ubinafsishaji na haki kwa ajili ya jamii za chini’, mtafiti kutoka Taasisi ya Jamii, Kazi na Maendeleo (SWOP) katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Afrika Kusini, Dk. Sonwabile Mnwana, alisema bado serikali zinakumbatia wawekezaji na kuwaacha wazalendo, hivyo kurudisha ubaguzi wa rangi ambao ulilenga kuwanufaisha wachache ambao ni wageni.
 
Katika utafiti wake wenye kichwa cha ‘mapambano mapya katika ukanda wa bati…….Bakgatlaba-Kgafela, Jimbo la Kaskazini Magharibi’ nchini humo, Dk. Mnwana, alisema, maelfu ya wachimbaji wadogo katika serikali za Afrika, Afrika Kusini ikiwamo, hawajaliwi hata wakitaka mrabaha katika migodi hiyo, wanaandikishwa chini ya utaratibu wa kichifu, hivyo kurudisha ubaguzi wa rangi na kuibua ukoloni mpya.
 
Baadhi ya wachangia mada  walieleza kushangazwa na  wasomi ambao walitakiwa kuwaenzi waasisi ambao walipigania kupatikana kwa serikali huru za Afrika, wakiwamo Hayati Julius Nyerere wa Tanzania, Kwame Nkrumah wa Ghana na  Nelson Mandela wa Afrika Kusini, lakini wameungana na viongozi wa serikali hizo na kuwasaliti wananchi wa kawaida huku wakijifanya wako pamoja ili kufanikisha malengo yao.
 
Walizitaka serikali za Afrika kutokumbatia wachache na kwamba serikali yoyote ambayo inawekwa madarakani, inapaswa kuwatetea wananchi wake ili wanufaike na rasilimali zilizopo nchini mwao.
 
Naye mtafiti kutoka Uganda,  Deborah Iyebu, Karamoja, alisema maelfu ya wananchi hawanufaiki na migodi ya madini, hawana usalama, wanaibiwa ikiwa ni pamoja na kupewa malipo kidogo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa