Jonas
Kamaleki, Maelezo
WAAENDESHA pikipiki maarufu kama bodaboda wameiomba
serikali kuwachukulia hatua kali abiria wanaokataa kuvaa kofia ngumu (Helmet)
ili kutoa fundisho kwa watu wengine wasihatarishe maisha yao.
Akiongea katika mahojiano maalum, mwendesha
pikipiki, Nathanael Kiula wa Dar es Salaam amesema kuwa abiria wanaokataa kuvaa
helmeti wachukuliwe hatua kali ikiwepo kutozwa faini isiopungua Tsh.
30,000/= ili liwe fundisho kwa wengine.
“Mimi nina helmeti mbili ya kwangu na abiria lakini
abiria wengi hawataki kuvaa helmeti hasa akina mama kwa madai kuwa nywele zao
zinaharibika pia wanadai kuwa zina uchafu.”alisema Kiula.
Kiula alisema kuwa elimu itolewe kwa abiria na waendesha
pikipiki juu ya umuhimu wa kuvaa helmeti kwani ni kwa manufaa yao wanapopata
ajali wasiumie sana au kupoteza maisha na si kwa ajili ya kuwakwepa matrafiki.
Mwendesha pikipiki aliyejitambulisha kwa jina la
Isaac William alisema abiria wanaokataa kuvaa helmeti waadhibiwe vikali ili
kukomesha tabia hii isiokubalika katika suala zima la usafirishaji.
“Abiria wangu baadhi wanakubali kuvaa helmeti lakini
walio wengi hukataa kuzivaa kwa madai kuwa wanaogopa magonjwa ya kuambukizwa
kupitia vifaa hivyo,”alisema William.
Naye abiria wa bodaboda ambaye ni mkazi wa Dar es
Salaam, Bi Fatuma Abdallah amesema yeye hawezi kuvaa helmeti kwani zinatumiwa
na watu wengi hivyo anaogopa kupatwa na magonjwa.
“Siwezi kuvaa mikofia yao kwani inatumiwa na watu
wengi huwezijua wana magonjwa ya ngozi kiasi gani, kamwe sintoyavaa
ng’o,”alisema Fatuma.
Kwa upande wake Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabarani nchi, Mohamed Mpinga alisema kuwa uvaaji wa kofia ngumu kwa
waendesha pikipiki ni lazima. Anayekaidi amri hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa
dhidi yake.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Helmet Vaccine Initiative Tanzania Foundation, Bw. Alpherio Nchimbi alisema matumizi ya Helmeti
hayaepukiki kwa usalama wa mwendesha pikipiki na abiria.
“Kwa umuhimu huo, Taasisi yetu inatoa msaada wa
kiufundi kwa Jeshi la Magereza nchini kwa ajili ya uanzishwaji wa kiwanda cha
kutengeneza kofia ngumu kwa kufuata viwango vya Shirika la Viwango nchini (TBS)
na pia tunatoa elimu kwa bodaboda kuhusu matumizi ya kofia ngumu na madhara
yatokanayo na kutovaa kofia hizo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa
ujumla,” alisema Nchimbi.
Kuhusu suala la kuvaa helmeti, Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa mwendesha pikipiki na abiria ni lazima
wavae helmeti na ifikapo Julai 1, 2016 hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
abiria au mwendesha pikipiki atakayekaidi amri hiyo.
“Nawaambia, hatutamvumilia mtu yeyote, mwendesha
pikipiki na abiria asiyevaa helmeti tunawahesabu kuwa wana mpango wa kujiua,”alisema
Makonda wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Taifa wa Usalama wa raia wa Jeshi la
Polisi.
Suala la kuvaa kofia ngumu au helmeti kwa waendesha
pikipiki na biria wao limekuwa likipuuzwa kwa muda mrefu ndio maana serikali ya
Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Jeshi la polisi wameandaa utaratibu
wa kuwafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria kwa ajili ya kunusuru maisha
yao. Mpango huu unaanza rasmi tarehe 1, 2016.
0 comments:
Post a Comment