Na Benedict Liwenga-WHUSM.
WAZIRI
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ameahidi
kuzitataua baadhi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Chama cha
Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) ikiwemo upatikanaji wa Hati
Miliki ya Kiwanja kwa ajili ya kazi zao, Ushuru unaotozwa kupitia Idara
ya Maliasili nchini pamoja na Sheria ya Tozo katika Viwanja vya Ndege.
Mhe,
Nnuaye ametoa ahadi hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na
Wanachama wa Shirikisho hilo ambapo amesema kuwa, suala la upatikanaji
wa Hati Miliki ya eneo kwa ajili ya kazi za Wachongaji hao alishaanza
kuifanyia kazi kwa kufanya mawasiliano na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na amewahakikishia kwamba Hati
ya eneo hilo itapatikana ili Wachongaji hao waweze kuwa na eneo lao
maalum la kazi zao.
‘’Suala
la upatikanaji wa Hati Miliki katika eneo lenu ambalo limekuwa likileta
minong’ono niachieni mimi kwani najua katika hili kuna baadhi ya watu
wenye fedha wanataka kuwakandamiza watu wasio na uwezo kwa kudai kuwa
eneo ni la kwao, hapo awali nilishafanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi na nawahahakikishieni kuwa haki
itatendeka, kwani hakuna mtu mwenye mfuko mkubwa wa kuweza kuiingiza
Serikali nzima katika suala hili’’, alisema, Mhe. Nnauye.
Kuhusu
suala la Ushuru unaotozwa na Maliasili nchini, Mhe. Nnauye amesema kuwa
yuko tayari kukaa na watu wa Maliasili na kuona namna gani ushuru huo
unavyotozwa hususani kwa Wachonagji hao pasipo kuonewa mtu ambapo pia
ameshauri kuwa baadhi ya kodi ambazo zinazoweza kuua biashara za watu
wenye vipato vya chini ni vema zikaondolewa ili zisiendelee kuwaumiza.
Aidha,
Mhe, Nnauye ameahidi kutembelea maeneo ya Viwanja vya ndege ili kuweza
kujua baadhi ya bidhaa za kazi za Uchongaji ambazo zimekuwa zikikamatwa
na Watendaji viwanjani hapo zimekuwa zikiishia wapi ili kuondoa
malalamiko yanayoelekezwa katika viwanja hivyo.
‘’Niwahakikishieni
kwamba nitakwenda mwenyewe katika viwanja vya ndege ili nijue ukweli wa
malalamiko yenu kwamba kumekuwa na baadhi ya kazi zenu za sanaa kama
vile Uchongaji ambazo zimekuwa zikikamatwa katika baadhi ya viwanja
vyetu vya ndege lakini mwisho wa siku hazijulikani zinaishia wapi’’,
Alisema, Mhe. Nnauye.
Mhe.
Nnauye ameahidi pia kujenga utaratibu wa kutembelea maeneo ya kazi za
sanaa mara kwa mara na kwa namna nyingine amewaasa Kampuni ya Quality
Group kusaidia kuzitangaza kazi za sanaa za Wachongaji hao kwani wao
wameshafungua Duka Maalum ambalo linarahisisha upatikanaji wa bidhaa za
sanaa kwa wageni na wenyeji ili kuwasaidia Wachongaji hao nchini.
Sambamba
na hayo, Mhe. Nnauye amewashauri Wanachama hao kuunda SACCOS imara
ambayo itawasaidia katika kujikwamua kiuchumi kutokana na kazi zao na
kuwaahidi kuwatafutia mitaji kwa makubaliano ya kwamba, wanapaswa
kuwachagua viongozi waaminifu ambao wanaweza kuongoza vema Saccos hiyo
kwa manufaa ya wanachama wote.
Kwa
upande wake Rais wa Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania
(CHAWASAWATA), Bw. Adrian Nyangamalle amepongeza juhudi za Serikali
katika kuwasimamia Wasanii kote nchini ambapo ameiomba Serikali pia
kuharakisha suala la upatikanaji wa Sera ya Sanaa pamoja na Mfuko wa
Sanaa kwa ajili ya Wasanii hao.
‘’Nikuombe
Mhe. Waziri kutusaidia kuzishawishi baadhi ya Taasisi na Makampuni
nchini kujenga utarataibu wa kuwatembeza wageni wanaokuja nchini katika
maeneo ya sanaa ili soko la bidhaa zetu liweze kukukua ndani na nje ya
nchi yetu’’, alisema Bw. Nyangamalle.
Chama
cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) kilianzishwa mnamo
mwaka 1984 na kimesajiliwa kihalali na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)
ambapo mbali na majukumu yake kimeweza kuwaandaa na kuwashirikisha
Wasanii wa ndani na nje ya nchi pamoja na kutetea Wasanii katika kupata
haki zao.
0 comments:
Post a Comment