Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeandaa
operesheni kabambe katika stendi ya Mbagala ili kuhakikisha biashara
zote zinafanyika katika maeneo yaliyotengwa na yasiyohatarisha afya ya
jamii.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wananchi
wa eneo hilo juu ya wafanyabiashara mbalimbali waliovamia eneo hilo na
kulifanya kuwa la biashara.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,
Nassib Mbaga na kuwataka wafanyabiashara wanaofanya biashara zao katika
mazingira yasiyo rasmi kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria na
taratibu.
“Tumeandaa
operesheni kabambe ya kuondoa Kero zilizogundulika katika stendi ya
Mbagala ili kuhakikisha kwamba biashara zote zinafanyika katika maeneo
yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo” alisema Mbaga.
Aliongeza
kwa kuwataka watu wote wanaofanya biashara bila kibali katika maeneo ya
stendi hiyo waondoke kabla ya zoezi la kusafisha halijaanza na kwa wale
watakaokaidi, hatua za kisheria zitachukulia dhidi yao.
Aidha
Mbaga alieleza kuwa kumekuwepo na jitihada za wazi za kuiweka
Halmashauri katika hali ya usafi ikiwemo kutoa elimu kwa umma pamoja na
kuhamasisha wananchi kuweka mazingira katika hali ya usafi na kuzuia
unywaji wa maji ya kwenye vifuko vya plastiki yajulikanayo kama
viroba/Kandoro kwa kuwa hayana viwango vya ubora.
Vilevile
Halmashauri hiyo itaendelea kuwakamata wale wote wanaofanya biashara
hiyo na kuteketeza mali zao kisha kuwafikisha Mahakamani au kuwalipisha
faini.
Mkurugenzi
huyo ameyataja maeneo matano ambayo yametengwa rasmi kwa ajili ya
biashara yakiwemo soko la Toangoma, Kilamba, Makangarawe, Sigara na
Kiponza ambapo maeneo hayo yana huduma zote za jamii ikiwemo vyoo bora.
Maeneo
mengine yaliyotengwa na Halmashauri kwa ajili ya Masoko ni pamoja na
Temeke Stereo, Vetenari Tazara, Madenge, Tandika Kuu, Tandika Kampochea,
Keko Magurumbasi, Temeke Mwisho, Bulyaga, Kizuiani, Zakhem, Mbagala
Rangi tatu, Kampochea Mbagala, Mtoni Mtongani, Lumo, Urassa,Feri,
Maguruwe, Limboa na Kabuma.
Mkurugenzi
Mbaga ametoa rai kwa wananchi wanaohitaji kupata nafasi za kufanyia
biashara katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo kufanya
mawasiliano na Ofisi yake ili kupatiwa maeneo rasmi kwa ajili ya
shughuli hizo.
0 comments:
Post a Comment