Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Sekta
ya Habari na Utangazaji ni moja ya sekta za huduma za jamii nchini
inayotoa huduma ya haki ya msingi ya raia kama ilivyojieleza katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Historia inaonyesha kuwa kwa zaidi ya miaka 20 sasa wadau wa sekta ya habari wamekuwa wakipigania kuipa heshima taaluma ya habari na kuifanya kuheshimika kama fani nyingine nchini.
Mwezi September mwaka huu katika mkutano wa tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muswada wa huduma za habari ulisomwa kwa mara ya kwanza na kutolewa fursa kwa wadau wa habari kutoa maoni ili kuuboresha zaidi.
Jumla ya taasisi 10 ziliwasilisha maoni mbalimbali kuhusu muswada huo ikiwemo Baraza
la Habari Tanzania (MCT), Tanzania Citizens Information Bureau
(TCIB),Chama cha Wanasheria,Sikika, taasisi ya Nola, Jukwaa la Wahariri
Tanzania na Kituo cha Sheria na Haki za binadamu Tanzania
Taasisi
nyingine ni Chama cha waandishi wa habari Tanzania (TAMWA),Kituo cha
kutetea haki za binadamu Tanzania, Chama cha wamiliki wa Vyombo vya
Habari nchini (MOAT), na taasisi ya habari ya nchi za kusini mwa Afrika
tawi la Tanzania (MISA – TAN) .
Aidha
Asilimia 90 ya maoni yaliyowasilishwa na wadau hao yamejumuishwa katika
muswada huo ili kuwezesha muswada huo kuwa na sheria inayokidhi matakwa
ya wanahabari, kwa kuzingatia mapendekezo waliyoyatoa.
Akiwasilisha
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari katika Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Huduma za Maendeleo ya Jamii,Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye alisema kuwa muswada huo unalenga kuihamisha sekta ya habari kuwa taaluma kamili na kuweka masharti ya kukuza na kuimarisha taaluma na weledi.
Waziri
Nape alisema muswada huo umeandaliwa kukabiliana na changamoto
mbalimbali zilizopo katika tasnia ya habari nchini ambazo ni pamoja na
upungufu wa sheria zinazosimamia tasnia hiyo na mabadiliko ya teknolojia
ya habari.
“changamoto kubwa katika sekta hii ya taaluma ya habari ni kutotambulika
kama taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, kukosekana vyombo madhubuti
na huru vya usimamizi na badala yake mambo mengi kuwa chini ya serikali
moja kwa moja,”
“Sheria
hii italeta mageuzi makubwa katika usimamizi wa sekta ya habari hapa
nchini ambayo inakwenda kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
kuifanya rasmi sekta ya habari kuwa sekta rasmi kama zilivyo sekta
nyingine za uhasibu, udaktari,” alisema Waziri Nape.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Hassan Abbas anasema lengo la muswada huu ni
kuja na sheria itakayokuza na kuimarisha taaluma na weledi katika
tasnia ya habari na kuweka mfumo wa usimamizi wa huduma za habari.
Aidha Abbas anasema muswada
huo utakusudia kuiongezea nguvu tasnia ya habari ikiwemo suala zima la
kuzingatia sheria na mipaka ya nchi katika utoaji wa habari na taarifa
maalum za Serikali kwa umma na kuzingatia ukomo wa kimataifa.
“Azimio
la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948, pamoja na kuzungumzia kuhusu haki ya
kupata taarifa lakini pia limeanisha sheria mbalimbali ambazo hazina
budi kuheshimiwa, na sheria hizo ni pamoja na sheria za ulinzi na
usalama” alifafanua Mkurugenzi Abbas.
Anaongeza
kuwa kifungu cha 19 cha mkataba wa geneva wa mwaka 1966 pamoja na mambo
mengine umeeleza kuhusu haki ya kupata habari na taarifa ingawa
imeanisha wajibu hasa katika maeneo yanayohusu usalama wa taifa.
Kwa kuzingatia mkataba huo wa kimataifa sehemu
ya nane Masharti ya Jumla kifungu 55 katika muswada wa huduma za
habari, Waziri atakuwa na mamlaka ya kuzuia uchapishaji au utangazaji wa
maudhui yanayohatarisha usalama wa Taifa au afya ya jamii.
Katika hatua hiyo Mkurugenzi Abbas
alisema kuwa yapo masuala kadhaa yanayopaswa kuchuliwa hatua za haraka
za maamuzi ikiwemo suala la uchochezi, uasi wa kikundi fulani cha watu
kinachotaka kuigombanisha Serikali na wananchi.
“Uchochezi
ni kuhatarisha amani ya nchi, lakini mwandishi akiikosoa Serikali
haitokuwa uchochezi bali kwa atakayeleta habari za uchochezi kwa maana
ya uasi atatakiwa kuwajibishwa” alifafanua Mkurugenzi Abbas.
Akifafanua
zaidi alisema endapo mwandishi ataandika habari za kichochezi za
kuhatarisha amani ya nchi hana budi kuchukuliwa hatua na kama
hajaridhika na hatua hiyo ana uwezo wa kupeleka jambo hilo katika
mamlaka husika ikiwemo kupeleka Mahakamani.
Akizungumza
kuhusu suala la taaluma la mwandishi wa habari katika masuala ya Elimu,
Abbas anasema suala hilo halitaainishwa katika sheria bali litaainishwa
katika kanuni za Bunge ili kuweza kutolewa baadhi ya marekebisho.
Abbas
alisema Sheria hiyo itumika Tanzania Bara pekee, kwa kuwa suala la
habari si suala la Muungano japo sekta hizi zinashirikiana kwa namna
moja au nyingine.
Mbali
na hayo alisema kuwa lengo la muswada huu ni kusajili vyombo vya habari
vyenye mfumo wa machapisho ikiwemo magazeti, majarida na si mitandao ya
kijamii kama inavyosemwa na baadhi ya watu.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment