Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Taasisi
ya Mifupa Muhimbili (MOI) imejipanga kuongeza muda wa kutoa huduma za
afya ili kuweza kutoa tiba kwa wagonjwa wengi pamoja na kuongeza mapato
yatakayotumika kuendeshea taasisi hiyo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface ameyasema hayo leo wakati wa
kikao cha 4 cha Baraza la 3 la wafanyakazi wa taasisi hiyo
kilichofanyika katika ukumbi wa Iddy Nyundo ulipo Jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Boniface amesema kuwa bajeti ya Serikali pekee haiwezi kujitosheleza
hivyo menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hiyo wana wajibu wa kutafuta
vyanzo vingine vya halali vitakavyoiwezesha taasisi kujiendesha kama
ilivyokuwa awali.
“Katika
taasisi yetu wateja wetu ni wagonjwa hivyo tunatakiwa kuimarisha huduma
zetu ili tuweze kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi, tumepanga kuongeza
muda wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa kawaida na wanaohitaji upasuaji,
kuongeza vifaa vya maabara pamoja na wodi za wagonjwa ikiwa ni njia ya
kuongeza mapato ya taasisi,” alisema Dkt. Boniface.
Mkurugenzi
Boniface ameongeza kuwa ni muhimu wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii
kwa kutafuta njia mbadala za kujiinua kuliko kulalamika hivyo ni vema
kutumia mfumo wa ufanyaji kazi wa sekta binafsi na kuweka timu bora kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu kwa ajili ya mapambano yatakayopelekea kuboresha huduma na mapato.
Kwa
upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa MOI, Prof. Bakari
Lembariti amesema kuwa ili kuleta mageuzi makubwa ndani ya taasisi na
kuhakikisha taasisi inafanya vizuri ni wajibu wa kila mfanyakazi
kuhakikisha MOI inasimama kwa kujitoa kufanya kazi kwa moyo.
“Pamoja
na changamoto zote mlizokuwa nazo, nawashauri kuacha lugha chafu kwa
wagonjwa,utoro kazini pamoja na rushwa kwani vitendo hivyo viovu ndivyo
vinavyopelekea kupunguza wateja na kupeleka kupunguza kipato,”alisema
Prof. Lembariti.
Aidha,
amewataka wafanyakazi kuzipitia kanuni za utumishi wa umma na kuzielewa
ili wafanye kazi kulingana na kanuni hizo na kwa atakaepuuzia
achukuliwe hatua stahiki.
Taasisi
ya MOI imeanzishwa mnamo mwaka 1996 ikiwa na lengo la kutoa huduma bora
za afya kwa wagonjwa wa mifupa, upasuaji wa uti wa mgongo na mishipa ya
fahamu.
0 comments:
Post a Comment