Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

MGOMO WA WALIMU WAANZA JIJINI DAR Es SALAAM

 Wanafunzi
wa shule ya msingi Makuburi manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,  wakiwa wameuchapa usingizi baada ya kuchoka kuwasubiri
walimu kuja kufundisha bila mafanikio, wiki iliyopita Chama cha Walimu CWT kilitangaza kuwa leo jumatatu walimu wa shule za Sekondari na Msingi wangeanza mgomo nchi nzima kutokana na kutofikia muafaka kwa madai yao dhidi ya Serikali.
(PICHA NA PHILEMON SOLOMON WA FULLSHANGWE) 


 Wanafunzi
wa Shule ya Msingi Mabibo iliyopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam
wakiwa wamelala baada ya kuchoka kuwasubiri walimu kuja kuwafundisha madarasani .

Picha kwa Hisani ya Full Shangwe Blog




MUDA WA VITAMBULISHO VYA TAIFA WAONGEZWA



Benjamin Masese na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeongeza muda wa wiki moja kwa wakazi wa Dar es Salaam wenye sifa ya kupatiwa vitambulisho hivyo.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu alisema shughuli hiyo itamalizika Agosti 6, 2012 huku akisisitiza muda mwingine hautaongezwa tena.

Maimu alisema wageni wote wanapaswa kujaza fomu 2A kwa kueleza ukweli uraia wa nchi zao na hadhi ya ukaazi wao.

Alisema kwa mujibu wa sheria za usajili na utambuzi wa watu kifungu cha 9 (2) waombaji wasiojua kusoma na kuandika watasaidiwa kujaziwa fomu na wale wanaojua kusoma na kuandika watapewa fomu ili kujaza wenyewe chini ya usimamizi wa usajili wa kituo husika.

Maimu alisema kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1) C inaeleza kwamba ni kosa la jinai kutoa taarifa ambazo si sahihi zikiwamo za uraia na kuongeza atakayebainika atatozwa faini au kwenda jela miaka isiyozidi mitatu.

Vile vile alisema watu walio katika makundi maalumu kama wazee, walemavu na wagonjwa watapelekewa mahitaji yao pale walipo na viongozi wa Serikali za mitaa.

AWALI kabla ya kuongezwa kwa muda huo shughuli hiyo ilikuwa imeonekana kukwama kutokana na kujitokeza kasoro kadhaa zilizosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kujiandikisha.

Wakizungumza jana na MTANZANIA kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wamesema NIDA haikuweka utaratibu mzuri jambo ambalo linaonekana kusababisha wananchi kukosa haki ya kujiandikisha kwa siku zilizopangwa.

Mkazi mmoja wa Mongola la Ndege, Herbert Masamu amesema shughuli hiyo imekuwa ngumu kutokana na uchache wa watu waliopangwa kuandikisha taarifa za wananchi jambo ambalo limesababisha msongamano katika vituo mbalimbali.

Alisema pia kukosekana kwa elimu ya kutosha za nyaraka au taarifa muhumi anazotakiwa kuwa nazo mwananchi anayekwenda kujiandikisha nalo limekuwa ni kero kwa wananchi hivyo kulazimika kwenda na kurudi katika vituo vya kuandikisha bila kufanikiwa kujiandikisha.

“ Katika hili la uchache wa watu wanaoandikisha limetusababishia usumbufu hivyo NIDA wanapaswa kuongeza siku na idadi ya waandikishaji kama ilivyo kwenye kitambulisho cha kupigia kura ili kila mwananchi apate haki ya kujiandikisha,”alisema Masamu.

Kiwalani

Katika siku mbili za Jumamosi na Jumapili,MTANZANIA ilifanikiwa kufika katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Hali ya Hewa kilichopo kata ya Kiwalani na kushuhudia umati wa watu wengi wakisubiri huduma hiyo bila mafanikio.

Katika kituo ambacho hicho kinachounganisha zaidi ya mitaa mitatu, kulikuwa na hali ya kushangaza kutokana na wananchi kufika kituoni kuanzia saa 12 alfajiri ili kuwahi kujipanga foleni huku wafanyakazi wa NIDA hawaoneki kituoni.

Katika kituo hicho, mwandishi wa gazeti hili alikuwa ni mmojwapo ya wanaohitaji kuandikishwa lakini hakuweza kupata fursa kutokana na waandikishaji kuchelewa kufika kituoni na kufanya kazi pole pole.

Hata hivyo ilipofika saa 3.13 asubuhi alionekana Mwenyekiti wa Mtaa wa Minazi Mirefu, Ubaya Chuma na kuanza kutoa maelekezo kwa wananchi utaratibu uliopo .

Licha ya kutolewa maelekezo hayo lakini wafanyakazi hao hawakutokea hadi ilipofika saa 3 .27 asubuhi ndipo wandikishaji watatu walionekana hapo na kuanza huduma huku mtu mmoja akichukua kati ya dakika 20 na 30 kuandikishwa.

Katika kituo hicho cha Hali ya Hewa ilielezwa kwamba kuna waandikishaji 10 lakini hadi inafika saa 10 .03 walikuwa wamefika saba kitendo ambacho kilisababisha ongezekao kubwa la wananchi huku wakilalamika. 

Wakizungumza na MTANZANIA baadhi ya wananchi walisema msongamano huo unasabishwa na wafanyakazi wa NIDA kuchelewa kufika kituoni pamoja na utaratibu uliowekwa. 

Wananchi hao walililamikia kituo kutokana na na kuwapo na matatizo mengi yakiwamo kitabu kuibiwa cha orodha ya wananchi kitendo kilichomlazimu Chuma kuweka utaratibu wa kuwatambua wananchi hao.

Vile vile katika kituo hicho kuina wananchi walipatikana wakiwa na photocopy ya kitambulisho cha kupigia kura cha mtu mwingine wakitaka kukitumia.

Kwa mujibu wa Ubaya aliwaeleza wananchi hao kwamba kuna watu wachache wasio wadilifu wanachukua kadi za kupigia kura za watu wengine na kubandua picha za mtu halali na kubandika za kwao kisha kuzitoa photocopy.

Chanzo: Mtanzania

AKUTWA NA UNITI 29,365.5 ZA SH MILIONI 8


na Shehe Semtawa
MKAZI wa Kariakoo Mtaa Agrey jijini Dar es Salaam, Ahamad Selemani anashikiliwa na Polisi baada mita yake ya Luku kukutwa na uniti za umeme 29,365.5, zenye thamani ya sh milioni nane.
Meneja wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Kanda ya Ilala, Athanasius Nangali, alisema jana kuwa mteja huyo ambaye jina analotumia kwenye mita yake ya Luku ni Mallick Bhachool, hajawahi kununua umeme tangu alipounganishiwa mita hiyo mwaka 2010.
Mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Kwa mujibu wa Nangali, tukio lingine kama hilo limetokea katika eneo la Kariakoo Mtaa wa Magila ambapo Meneja wa Hoteli ya Akubu Paradise, Inocent Masawe alikamatwa akiwa na uniti 1100 za umeme kwenye mita yake ya Luku, zenye thamani ya sh milioni 4.
Alisema mteja huyo amekuwa akifanya ujanja wa kununua umeme kidogo kwa ajili ya matumuzi ya hoteli yake, lakini umeme uliomo kwenye mita ni mwingi kuliko kiasi anachonunulia.
“Hawa tutakula nao sahani moja hadi watuambie wanakonunua umeme na hatimaye tutakamata mtambo unaozalisha uniti hizo bandia,” alisema.
Nangali alisema TANESCO itahakikisha inawatia mbaroni wauzaji wa uniti hizo kinyume cha sheria.
“Hawa kuna sehemu wananunua umeme lakini hatujafahamu ni wapi hivyo kukamatwa kwao ni dalili kubwa ya kubaini wanakonunua maana katika hali ya kawaida haiwezekani mtu awe na uniti hizi zote,” alifafanua Nangali.
Alitoa wito kwa Watanzania kutoa taarifa za wanaoihujumu TANESCO na kutangaza zawadi ya sh 50,000 kwa kila nyumba itakayokamatwa.
Alipoulizwa kuhusu ongezeko la faini na idadi ya watu waliofikishwa mahakamani, Nangali alisema idadi hiyo itajulikana mara baada ya kufanya majumuisho mwishoni mwa mwezi huu japo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 100 sasa wameshakamatwa na kulipishwa faini tangu kuanza kwa operesheni hiyo.
Wiki tatu zilizopita aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, William Mhando, alitangaza kukamatwa kwa watu watatu mkoani Dodoma na wawili jijini Dar es Salaam waliokuwa wakitumia umeme ambao haujafahamika unakopatikana.
Chanzo: Tanzania Daima


MKURUGENZI MAKUMBUSHO YA TAIFA, ASIMAMISHWA KAZI


Florence Majani


MKURUGENZI wa Makumbusho ya Taifa, Jackson Kihiyo amesimamishwa  kazi kwa muda usiojulikana  ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi huyo alisema  aliitwa na mkubwa wake wa kazi, ambaye ni Katibu Mkuu  Wizara ya Maliasili na kufahamishwa kuwa amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwani kuna tuhuma kuhusu utendaji wake katika ofisi hiyo.

“Baada ya kupewa taarifa hizo, juzi(jumanne) nilikabidhi ofisi na hivi sasa nipo nyumbani. Cha muhimu ni kuwa sijafukuzwa ila nimesimamishwa na ninaendelea kupata mshahara wangu kama kawaida haid pale watakapomaliza huo uchunguzi wao,” alisema Kihiyo


Kihiyo alisema, hakutaka kumhoji mkuu wake wa kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kwa sababu alitaka wawe huru na wafuatilie kwa kina bila kuingiliwa, hivyo hadi sasa hafahamu kilichomsimamisha kazi.

“Najua wakimaliza watanijulisha, sina mashaka yeyote kwa sababu najua hakuna kibaya nilichofanya, nikiwauliza uliza watadhani ninataka kuwaingilia katika uchunguzi wao. Waache wafanye uchunguzi kwa utaratibu na kwa uhuru wakimaliza watanieleza kilichopatikana,” alisema Mkurugenzi huyo. 

Chanzo cha habari kutoka katika ofisi hiyo kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake kilibainisha kuwa mkurugenzi huyo amefukuzwa baada ya wafanyakazi kupeleka malalamiko kwa katibu mkuu, Maimuna Tarishi, ikiwemo utata katika ukusanyaji wa mapato na  maslahi ya wafanyakazi.

“Mkurugenzi alitoa amri ya kukusanya mapato katika vituo vyote na kisha mapato hayo katika akaunti ya makao makuu. Hili jambo lilizua maswali kwa sababu tutapelekaje mapato yote makao makuu, vituo vitajiendesha na nini? Lakini lingine ni maslahi duni ya wafanyakazi, hatujaboreshewa mishahara kwa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa malalamiko mengine kuhusu  utendaji wa mkurugenzi huyo ni kitendo cha Ofisi kutumia Menejimeti ya Umma kumuadhibu mfanyakazi badala ya kutumia Kamati ya Nidhamu jambo alilodai linasababisha uonevu mkubwa kwa wafanyakazi.

Shutuma nyingine dhidi ya Kihiyo ni upandishwaji wa vyeo  kwa wafanyakazi usiozingatia sifa stahiki na kutokuwepo mipango endelevu ya mafunzo kwa wafanyakazi. 

Kabla ya Kihiyo kushika nafasi hiyo, Mkurugenzi wa Makumbusho alikuwa ni Nobert Kayombo, ambaye alifariki   Novemba 30, 2010.

Chanzo: Mwananchi


WATATU MBARONI KWA KUHUJUMU ZOEZI LA VITAMBULISHO VYA TAIFA


Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imewakamata watu watatu na kuwafikisha polisi kutokana na makosa ya kuomba fedha kwa watu wanaokwenda kujiandikisha vitambulisho vya utaifa.

Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Habari wa Mamlaka hiyo, Thomas William, alisema watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, yakiwemo Bunju, Mabwepande na Yombo Kilakala.

“Hawa watu wamefanya mambo ya kihuni…tumewakamata na tumewafikisha kwenye vituo vya Polisi, tunataka sheria ichukue mkondo wake. Hawa watu tumewakamata baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi, naomba wananchi waendelee kutupa taarifa kwani bila wao hatutajua uchafu unaofanyika katika vituo vya kujiandikishia,” alisema William.

Akizungumzia suala la msongamano kwenye vituo vya kujiandikishia, William alisema wameamua kuongeza idadi ya maofisa usajili katika vituo.

“Tumeongeza idadi ya maofisa usajili katika maeneo ..tumeongeza jumla ya wasajili 240…lakini pia mtu anayejua kusoma na kuandika atapewa fursa ya kujisajili mwenyewe kwa kupewa fomu, lengo ikiwa ni kupunguza foleni,” alisema William.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kuongeza muda wa kujiandikisha, alisema hivi sasa hawawezi kusema kama wataongeza muda hadi zoezi hili, litakapofika mwisho.

“Kwa sasa ni mapema kusema kama tutaongeza muda, tutakapofika tarehe ya mwisho ndiyo tutaona…lengo ni kuandikisha wananchi wote, kwa hiyo tutaona ifikapo mwisho,” alisema William.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dickson Maimu, alisema mamlaka ina vituo 451 na watendaji 2,279 na wataendelea kuongeza pale itakapohitajika.

“Tuna vituo 451 Dar es Salaam, huku watendaji wakiwa 2,279, lakini NIDA tumeongeza watendaji wengine 240 wiki hii na kufanya idadi hiyo kuwa ya kutosha kwenye vituo vyetu,” alisema Maimu.

Kwa mujibu wa Maimu, zoezi la uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa, limelenga kutengeneza daftari kuu la kudumu la utambuzi wa watu.

Hata hivyo, Mjumbe wa Serikali za Mtaa Sinza C, Fredriki Kapufi, amesema licha ya kuwa na mwamko mzuri wa wananchi, lakini kuna watu wengi bado hawajafikiwa.

Aliishauri Serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa vitambulisho vya taifa, kwani bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi.

Habari hii imeandikwa na Elizabeth Mjatta, Otilia Paulinus na Mariam Kibondei

Chanzo: Mtanzania

MADIWANI WA ILALA WAPITISHA SHERIA YA HUDUMA YA MFUKO WA BIMA YA AFYA NHIF KATIKA MANISPAA HIYO


Meya wa Manispaa ya Ilala Bw. Jerry Silaa akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Anatouglo jijini Dar es salaam, kazi kubwa ya Baraza jilo la Madiwani ilikuwa ni kupitisha sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo sasa mfuko huo kupitia TIKA utaanza kutoa huduma za matibabu kwa wakazi wa manispaa hiyo ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wa manispaa hiyo hasa wale wenye kipato cha chini.
Mmoja wa watumishi wa Manispaa hiyo akitoa SIWA mara baada ya Baraza hilo la madiwani kupitisha sheria hiyo na kuahirisha kikao hicho.
Madiwani mbalimbali wakiwa katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani.
Madiwani mbalimbali wakiwa katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani.

Meya wa Manispaa ya Ilala akiwa katika picha ya pamoja na Wakuuwa Mfuko wa Bima ya Afya NHIF baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha madiwani.
Wakuu wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii NHIF wakiwa katika picha ya pamoja.
Kwa hisani ya Full shangwe Blog

NEWS ALERT :MGOMO WA DALADALA D’SALAAM WIKI IJAYO



Na Harrieth Mandari, Dar es Salaam

CHAMA cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), kimetangaza kuanza mgomo Jumatatu ya wiki ijayo, hadi Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) itakapobadilisha mfumo wa ukamataji madereva wanaokiuka sheria za barabarani.


Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa DARCOBOA, Sabri Mabrouk, alisema wamiliki wa mabasi madogo ya kusafirishia abiria (daladala) wamechoshwa na matatizo na malalamiko wanayoyapata kutoka kwa waajiriwa wao ambapo magari hukamatwa bila mpangilio.

“Kwa kifupi sisi hatukatai kutii sheria na tunasisitiza kuwa iwapo dereva au kondakta atakamatwa akivunja sheria achukuliwe hatua, lakini siyo kupitia askari ‘maruhani’ ambao huwakamata na kuwabambikiza makosa madereva wanayodai ya zamani,” alisema Mabrouk.

Alisema askari hao wanajulikana kama ‘maruhani’, jina ambalo limetokana na kitendo cha kuendesha mpango wa kuwakamata kwa kujificha vituoni na kuwakamata madereva na kuwabambikizia makosa mengi bila mpangilio.

“Hatukatai kuwa makosa yapo, lakini kwa nini hao ‘maruhani’ wasitambulike rasmi na kukamata pale pale dereva anapokosa, badala ya kukamata kwa makosa wanayodai wamewakuta nayo ambayo mengi kwa mujibu wa madereva wetu ni ya uongo,” alisema Mabrouk.

Alisema askari hao ambao wengi wao walikuwa madereva zamani, wamekuwa wakiomba rushwa kwa lazima mara wanapowakamata na inapotokea wananyimwa wanawabambika makosa ya ziada.

Alisema ni vyema SUMATRA itamke rasmi kuwa imewaajiri na wadau wa usafiri jijini wawatambue ili kuepusha migogoro isiyokuwa na lazima.

“Tunaishauri SUMATRA isimamie mpango huo wao wenyewe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kudhibiti uombaji rushwa kupita kiasi na kukamata magari bila mpangilio, ambapo hadi sasa zaidi ya magari 100 yameshakamatwa,” alisema Mabrouk.

Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva na Makondakta jijini Dar es Salaam (UWAMADA), Shukuru Mlawa, alisema usumbufu wanaoupata kutoka kwa askari wa ulinzi shirikishi wanaotumiwa na SUMATRA ni batili, kwa kuwa wao kama wadau hawawatambui.

Aliishauri SUMATRA kutumia kitengo cha ukaguzi badala ya askari hao ambao wamekuwa wakiendesha mpango huo bila mpangilio.

SUMATRA hivi karibuni walianza mpango wa kukamata madereva na makondakta wa daladala wanaokiuka sheria za barabarani.


Chanzo: Mtanzania


WASOMI, WANAHARAKATI WAPINGA MABADILIKO NSSF, PPF



Gabriel Mushi na Elizabeth Mjatta, Dar es Salaam

WAKATI Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kikipanga kuiburuza Serikali mahakamani kupinga matumizi ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii,wasomi nao wamepinga sheria hiyo kwa kudai ni kandamizi.


Hatua hiyo, imekuja baada ya Bunge kuifanyia marekebisho na hatimaye Rais Jakaya Kikwete kuisani Aprili 13, 2012 kwa ajili ya kuanza kutumika rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, wakati uzinduzi wa ripoti ya haki za binadamu ya nusu mwaka, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Hellen Kijo Bisimba, alisema sheria hiyo ni kandamizi kwa wafanyakazi wote kwa sababu haikushirikisha hata wafanyakazi wenyewe ambao ni ndiyo wadau wakuu.

Alisema kipengele cha fao la kujitoa kifutwa na badala yake mwanachama apokea mafao yake, baada kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60).

“Kwa sababu katika mazingira halisi ya nchi yetu, muda wa kuishi kwa mtu ni miaka 45, sasa kama asipofikisha miaka 55 ina maana mafao yake yatapotea… huu ni ufisadi uliofanywa kwa maslahi yao binafsi kwa sababu kama tunavyojua, fedha hizi zinatumika kwenye miradi yao kama ile ya NSSF, ilivyojenga Chuo Kikuu cha Dodoma na sasa mradi wa Kigamboni.

“SSerikali inatakiwa kuzipitia upya sheria kama hizi, kwa sababu hata tulipoangalia kwenye rekodi za Bunge, sheria hii ilipitishwa kinyemel… kwa msingi huo tumejipanga kwenda mahakamani kupinga matumizi ya sheria hii,” alisema.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, (UDSM), Dk. Benson Bana, ameiponda sheria hiyo na kusema si rafiki wa wafanyakazi.

Aliiitaka Serikali kuacha kuingilia mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwani inaonekana inailazimisha mifuko hiyo kutekeleza majukumu yake.

“Mifuko hii inatakiwa iwe huru, kwa sababu wana hisa ni wafanyakazi wenyewe…kama ni kujenga miradi iache mifuko hii ijipangie yenyewe na si Serikali jamani,” anasema Dk.Bana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya alisema sheria hiyo inatakiwa kufutwa mara moja..

“Kwa maoni yangu, hii sheria inatakiwa ifutwe mara moja ina mkandamiza mfanyakazi…kwasababu wapo watu ambao baada ya kuwa katika ajira kwa muda fulani, wanataka kujiajiri sasa unasemaje mtu kama huyo asipewe mafao yake,”alisema Nkya.

Mbunge wa Kilwa Kaskazini, (CCM) Murtaza Mangungu, aliunga mkono hatua ya Rais Kikwete na Bunge kupitisha marekebisho ya sheria hiyo na hivyo kuwataka Watanzania kukubaliana na mabadiliko hayo.

“Tunatakiwa kujifunza, tuwe na tabia ya kujiwekea akiba, kwa sababu sheria hii inawataka wananchi wawe na tabia ya kujiwekea akiba ndio maana hata sisi wabunge tumeipitisha.

“Hapa wanashindwa kuelewa, kwa mfano nchi kama Marekani wananchi wake wanaruhusiwa kuchukua mafao yao wakishafikisha miaka 62 vile vile

Chanzo: Mtanzania



WIZARA YALALAMIKIWA KUTOONDOA MABANGO YA WAGANGA


Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imelalamikiwa kushindwa kuondoa mabango ya waganga wa tiba za asili na hali hiyo inazidisha kushusha heshima ya tiba za asili nchini.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Utabibu na Dawa za Asili Tanzania (ATME), Simba Abraham.

Alisema Serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilitoa amri ya kuondolewa kwa mabango yote ya waganga wa tiba za asili yaliyokuwa na ujumbe unaopotosha jamii, ikiwamo kushawishi mauaji ya albino.

“Toka Pinda atoe maagizo haya hatuoni mabadiliko, sana sana tunaona mabango ya kupotosha jamii ya waganga wa jadi ndiyo yanaongezeka, suala hili tumelipigia kelele kwa wenzetu wa Baraza la Tiba Asili Tanzania, lakini hadi leo hatuoni hatua zozote zinachukuliwa.

“Aprili 7, mwaka huu, tulikuwa na kikao na watu wa Baraza la Tiba Asili ambalo liko chini ya Wizara ya Afya, tuliwaeleza malalamiko yetu, walisema hatua za kuondoa mabango hayo zitafanyika haraka iwezekanavyo, lakini hadi leo hii mabango bado yapo na kibaya zaidi viongozi wa ATME tunatumiwa ujumbe wa vitisho kwamba sisi ndiyo tunang’ang’ania mabango yatoke na ipo siku tutakiona cha moto,” alisema Simba.

Chanzo: Mtanzania



Lori la Mchanga laangukia Gari ndogo Mbezi Beach

Ajali hii imetokea maeneo ya Mbezi Afrikana jijini Dar ambapo Lori hili lenye nambari za usajili T 545 BPU lililokuwa likimwaga mchanga na kujikuta likipiga mweleka na kuangukia Gari ndogo aina ya Toyota Rav4 yenye lambari za Usajili T839 BSL iliyokuwa imepaki katika eneo hilo.hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika ajali hii.

Kwa hisani ya Mtaa kwa mtaa Blog

UANDIKISHAJI VITAMBULISHO UTATA


na Nasra Abdallah
ZOEZI la kumpatia kila mwananchi kitambulisho cha uraia huenda lisifanikiwe kutokana na utaratibu ambao umekuwa ukitumika katika ujazaji fomu kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa taarifa gani hasa wanazotakiwa kuwa nazo katika ujazaji wa fomu.
Baadhi ya waandikishaji wamekuwa wakiwataka watu kuleta vyeti vya kuzaliwa, kitambulisho cha kupiga kura, leseni ya gari na kitambulisho cha kazi, wakati sehemu nyingine wakiambiwa ni kitambulisho kimojawapo tu kinachotakiwa.
Upungufu mwingine ni idadi ndogo ya makarani pamoja na kasi ndogo ambapo huchukua takriban dakika 20 hadi 25 kumhudumia mtu mmoja.
“Ili uweze kuwahi hapa inakupasa uje sio zaidi ya saa 4:00 asubuhi kwani ukichelewa itabidi uandikishwe tu kesho,” alisikika karani mmoja katika kata ya Mikocheni.
Hata hivyo, baadhi ya makarani walisema wanalazimika kujaza wenyewe fomu kwa kuwauliza wananchi maswali, kwa vile wengi wao wamekuwa wakijaza kwa makosa na hivyo kuchafua au kuharibu fomu.
Aidha, wananchi wengi hususan vijana hawajui majina yote ya wazazi wao wala kata walizozaliwa au namba zao za simu kitendo kinachowafanya kuanza kupiga simu kwa wazazi wao au ndugu zao kuuliza huku karani akiwa anasubiria majibu hayo.
Imebainika kuwa hakuna usiri wowote wakati wa uandikishaji huo kwa kuwa wakati mtu aliye nyuma ya anayeandikisha husikia kila kitu.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umegundua kwamba wageni wengine hawataki kujulikana.
Katika namna ya kushangaza, baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakitumia mwanya huo kuhamasisha wanachama wake kujiandikisha kwa wingi kama njia mojawapo ya kuwa na wapiga kura wengi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Khamis Juma, alisema walitegemea utaalamu zaidi utumike kupunguza kupotea kwa muda mwingi wa wananchi ambao wangekuwa katika shughuli za uzalishaji mali.
Naye Amina Salum alisema alitegemea siku ambayo waandikishaji walienda kuandikisha majina nyumbani wangejaza na fomu ili kuepusha usumbufu ambapo unapaswa kwenda kwa mara nyingine tena katika ofisi ya mtendaji.
“Lingine linalotushangaza ni kwamba unatakiwa kuleta picha yako,” alihoji dada huyo.
Wananchi wengi waliiomba Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) kutoa elimu zaidi ya nini hasa wananchi wanatakiwa kujaza katika fomu hizo ili wakifika kwa makarani iwe rahisi na kuepusha misongamano isiyo ya lazima.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Dickson Maimu alisema elimu ya uandikishaji imetolewa kwa kiasi kikubwa, na kwamba ni hali ya kutozingatia maelekezo hayo.
Alisema kuwa kuhusiana na wingi wa nyaraka, ni jambo jema kwa mtu kuwa na vitambulisho vingi, ingawa sio vibaya kuwa na kitambulisho kimojawapo.
“Hata pale ambapo kwa bahati mbaya hana kiambatanisho chochote, atakuwa na barua ya afisa mtendaji wa mtaa inayomtambulisha na ataandikishwa,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vema kuwa na uhakika wa taarifa za watu kwa sababu vitasaidia kumjulisha kuwa yeye ni Mtanzania kwa kujua amesoma wapi, shule gani, umri wake na mambo kama hayo.
Chanzo: Tanzania Daima

UDSM KUONGEZA UDAHILI FANI YA UVUVI, UCHUMI


na Nasra Abdallah
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinatarajia kuongeza udahili wa wanafunzi katika fani ya uvuvi na uchumi ili kuongeza idadai ya wataalamu katika sekta hiyo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Makamu Mkuu wa wa chuo hicho, Yunusi Mgaya, wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa uvuvi uliofanyika kwa siku nne jijini Dar es Salaam.
Mgaya alisema pamoja na sekta hiyo kuwa muhimu katika kuchangia pato la taifa lakini wamegundua kuwa kuna uhaba wa wataalamu wa fani hiyo, hivyo kazi hiyo kufanywa kienyeji zaidi.
Kwa mujibu wa Mgaya mpaka sasa ni vyuo viwili tu vinavyotoa taaluma hiyo ambavyo ni UDSM na Sokoine, jambo ambalo linahitaji jitihada zaidi za kuongeza wanafunzi watakaochukua fani hiyo.
Pia alisema wamedhamiria kuwa na tafiti nyingi zaidi katika sekta ya uvuvi ili ziweze kuja kusaidia vizazi vilivyopo na vijavyo na kuhakikisha sekta hiyo inachangia uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Visiwani Zanzibar, Abdillah Jihad Hassan, alisema bahari ni sawa na ardhi hivyo inapaswa kulindwa mazingira yake kwa hali ya juu.
Hassan alisema njia zinazotumika kwa sasa katika kuvua zinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, hivyo kusababisha kuua mazalia ya samaki na viumbe wengine wa majini.
“Ili kuhakikisha bahari inakuwa salama ni wajibu wa serikali na watu binafasi kuhakikisha tunapeana elimu ya uvuvi na mazingira ya bahari kwa kuwa kuna njia nyingi mbadala ambazo tunaweza kuzitumia katika kuvua ambazo haziitaji uwekezajki mkubwa,” alisema waziri huyo.
Mkutano huo wa uvuvi ulishirikisha takriban wajumbe 250 kutoka nchi mbalimbali duniani, ambapo Tanzania imekuwa ya kwanza kuwa mwenyeji kwa nchi zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Chanzo: Tanzania Daima

Madiwani K’ndoni wasusia uchaguzi wa Naibu Meya


Na Evans Magege, Dar es Salaam
MADIWANI wa vyama viwili vya upinzani (Chadema na CUF) wa Manispaa ya Kinondoni wamesusia kikao maalumu cha uchaguzi wa Naibu Meya.

Wakizungumza Dar es Salaam juzi, madiwani hao walisema walichukua uamuzi huo baada ya kugundua kikao hicho kiliitishwa kinyume cha Sheria na Kanuni zinazotumiwa na baraza hilo.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Baraza hilo, Boniface Jackob, alisema wameshangazwa na uongozi wa baraza hilo kuwaandikia barua za dharula za kutaka kufanya kikao maalumu ambapo walipofika ukumbini wakakuta ajenda ya kikao hicho ni kufanya uchaguzi wa Naibu Meya.

Alisema walipohoji ni kwanini uchaguzi huo unafanywa katika kikao maalumu na si mkutano mkuu, hapakupatikana majibu.

“Kuanzia sasa tumeamua kutangaza mgogoro rasmi na uongozi wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Kinondoni kwa sababu wameamua kuitisha uchaguzi batili wa kumchagua Naibu Meya.

“Tulisambaziwa barua kwamba tuhudhurie kikao maalumu, hatukujua kuna kitu gani kitakachojadiliwa lakini tuliyoyakuta ni madudu tupu.

“Kwanza tumefika tukakuta taratibu zimebadilika kwa kusainishwa posho za kikao kabla ya kikao kuanza na baadaye tunatajiwa ajenda kuu ni kufanya uchaguzi wa Naibu Meya, jambo hilo lilitushangaza na kutulazimu tususie kikao hicho ambacho kinaonekana kukumbatia mazingira ya ufisadi .

“Tukauliza mbona wanafanya uchaguzi huo kwa njia ya kulazimisha, wakabaki na kigugumizi huku madiwani wa CCM wakishinikiza ni lazima uchaguzi ufanyike, sisi tukasema hatuna tatizo na uchaguzi lakini uchaguzi huo si utavunja kamati zote na kusukwa upya, kwa maana hiyo miradi iliyokuwa ikisimamiwa na kamati hizo si itakosa muendelezo wa usimamizi mzuri lakini hawakutuelewa.

“Tukaendelea kuwadadisi kwa vipengele vya kanuni kuwa hadi sasa bado hatujafanya mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka ambao ungetuwezesha kupata taarifa za utendaji na uwajibikaji wa halmashauri na kisha uchaguzi wakabaki wanatoa macho, basi nasi tumeamua kususia mkutano huo kwa sababu ni uchaguzi batili,” alisema Jackob.

Hata hivyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, alisema uchaguzi huo ni halali na umefuata taratibu zote.

Alisema ameshangazwa kitendo hicho cha madiwani wa upinzani kugoma na kutoka nje ya ukumbi lakini akasema jambo hilo halikuharibu utaratibu mzima wa kupiga kura ambapo walibaki wajumbe 30 waliopiga na kumuwezesha Songolo Mnyonge kuibuka mshindi kwa kura zote za wajumbe.

“Uamuzi wao haujazuia uchaguzi wetu na kama wamesusia mbona hawakuzisusia posho walizozichukua asubuhi,” alihoji Mwenda.

Chanzo: Mtanzania







Alazwa kwa kupigwa risasi na polisi


na Abdallah Khamis, Dar es Salaam
MKAZI wa Mbezi kwa Yusuph, Calvin Muro, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi na askari polisi wa kituo cha Mbezi Luis.
Akizungumza na Tanzania Daima hospitalini hapo jana Muro alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1.00 usiku wakati askari hao wakiwa katika harakati za kulikimbiza lori la mchanga.
Alisema awali aliwaona askari hao wakiwa katika gari aina ya Defender wakilikimbiza lori hilo lililoegeshwa Kimara B na dereva wake ambaye hakufahamika kukimbilia kwenye nyumba moja ya kulala wageni kisha askari hao kumfuata na walipompata walimpiga ngumi na mateke.
“Mwanzoni tulishangaa tukajua ni jambazi lakini tulipoona wanaanza kumpiga ilitubidi tusogee kujua kinachoendelea ambapo tulimsikia yule dereva akilalamika na kusema sina pesa na ninatakiwa nipeleke hesabu nyie mmezoea kutuonea,” alisema Muro.
Alisema baada ya wananchi kusikia kauli hiyo walianza kuwazomea askari hao ambao waliondoka na baada ya muda wakarudi na kuanza kufyatua risasi hovyo ndipo moja ikampata yeye chini ya makalio sehemu ya paja la kushoto na kutokezea kwa mbele.
“Sikuusikia mlio wa risasi bali nilijihisi kama navuja maji na nilisogea katika mwanga nikaona tundu kubwa limejitokeza mbele ya paja langu huku damu ikinivuja kwa wingi ndipo wenzangu waliponichukua na kunipeleka polisi kisha Hospitali Teule ya Tumbi Kibaha ambao nao walinihamishia hapa Muhimbili saa nane usiku,” alisema.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo (jina linahifadhiwa) aliieleza Tanzania Daima kwamba askari waliotenda unyama huo walikuwa wakitumia gari la polisi lenye namba PT 1412.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Kimara aliyefahamika kwa jina moja la Papalika alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikataa kuzungumza na kutaka atafuatwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela.
Hata hivyo juhudi za kumpata kamanda Kenyela ziligonga mwamba baada ya simu zake za kiganjani kutopatikana kwa muda mrefu.
Chanzo: Tanzania Daima

Zaidi ya sh milioni 10zatengwa kufuturisha mkoa wa Dar es salaam


Zaidi ya sh milioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kufuturisha watu
wenye kipato cha chini kwenye
mwezi huu wa mfungo wa Ramadhani katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar
es Salaam.
 Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaa leo,
Mwenyekiti wa Taasisi ya Al Madina, Sheikh Ally Mubaraka alisema hayo wakati alipokuwa
akipata futari kwa pamoja na  waislamu wa Msikiti wa Sheikh Gorogosi, Tandika kwa Maguruwe.
 Alisema fedha hizo zimepatika kutokana na ushirikiano mzuri
uliyopo kati ya Ubalozi wa Emirate na taasisi hiyo inayojihusisha na utoaji
misaada katika jamii yenye mahitaji maalum.

Sheikh Mubaraka alisema taasisi hiyo inalenga kutoa futari
kwenye makundi ya watu ikiwa ni ishara ya huruma kama dini hiyo inavyoelekeza.
 “Ubalozi wa Emirate umejitolea fedha za kutosha kwa ajili kufuturisha
ambapo leo (jana), tumeanzia Tandika, mpango huu ni wa kila mwaka na utafika
katika maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam”alisema Sheikh Mubaraka.
 Sheikh Mubaraka aliwaasa wafanyabiashara kuacha kupandisha bei
za bidhaa kwa ajili ya kujipatia kipato kikubwa ambapo sheria za dini zinawataka
wanadamu kuoneana huruma wakati wote.
 Vilevile
alisema mwezi huu wa mfungo Ramadhani ni fursa njema ya kufanya ibada kitendo
ambacho kitawasidia waislam kufutiwa dhambi zao.
 “Yule mwenye
kula mchana katika mfungo huu,hata kama atakuwa akijibidiisha na swala atambuwe
kuwa hatoweza kufutiwa dhambi zake”alisema Sheikh Mubaraka.
 Akizungumzia
tukio la kuzama kwa meli ya Skagit, alisema taasisi hiyo imetoa pole kwa
familia zote zilizopoteza ndugu zao kwani tukio lile ni kubwa ambapo uchungu
wake umemgusa kila mtu katika nchi hii.



Uandikishaji vitambulisho vya taifa waingia dosari


na Dianarose Matikila, Dar es Salaam
ZOEZI la ujazaji fomu kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya taifa linaloendelea jijini Dar es Salaam, limeanza kugubikwa na dosari nyingi ambazo ikiwa hazitarekebishwa ni dhahiri wananchi wengi watashindwa kujiandikisha.
Licha ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kujaribu kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi, wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi kujaza fomu hizo kwa muda uliopangwa, uchunguzi wa Tanzania Daima katika vituo kadhaa vya uandikishaji umebaini zoezi hilo kuzorota.
Wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili, walilalamikia zoezi hilo wakidai linawachukua muda mrefu bila sababu ambao wangeutumia kufanya shughuli zao nyingine.
Kasoro mojawapo iliyoonekana kwenye vituo vingi ni watu kuanza kujiandikisha badala ya kujaza fomu hizo, jambo ambalo limeleta usumbufu mkubwa kwa wale waliokwisha andikishwa mapema.
Pia kumekuwa na upungufu wa makarani wa uandikishaji, jambo linalosababisha kuwapo kwa misururu mirefu ya watu vituoni.
“Haiwezekani tusimame hapa kwenye jua kwa muda wa zaidi ya saa moja na nusu halafu foleni yenyewe haisogei, na hiyo yote inatokana na utaratibu mbovu wa kwenda kujaza fomu hizo, alilalamika mkazi mmoja wa Kata ya Wazo.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa kata wameiomba NIDA iongeze idadi ya makarani vituoni kwa ajili ya kurahisisha na kuharakisha zoezi hilo la uandikishwaji na ujazwaji wa fomu hizo.
Chanzo: Tanzania Daima

Kufuatia Ajali ya Meli Zanzibar, Tume ya Mabadiliko ya Katiba Yasitisha Mikutano ya Kukusanya Maoni Kusini Pemba







Tume ya Mabadiliko ya Katiba imepokea kwa masikitiko makubwa Taarifa ya ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea jana, Jumatano, tarehe 18,  Julai  2012 katika eneo la Chumbe, Zanzibar.

Kutokana na msiba huu mkubwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa Taarifa kwa Wananchi kuwa imesitisha Mikutano ya kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokuwa inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba. Mikutano iliyositishwa ni ile iliyopangwa kufanyika kuanzia leo, Alhamisi, Julai 19, 2012 hadi Jumamosi, Julai 21, 2012 katika maeneo ya Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri, Pujini, Gombani na Wara.

Zoezi la kukusanya Maoni litaendelea kuanzia  Jumapili tarehe 22, Julai, 2012.  Ratiba ya Mikutano katika maeneo yaliyositishwa itatolewa baadaye.

Tume ya Mabadilikio ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa mabadiliko haya hayahusu mikutano ya kukusanya maoni inayoendelea kufanyika katika mikoa sita (6) ya Tanzania Bara ambayo ni Pwani, Tanga, Dodoma, Shinyanga, Kagera na Manyara.  Tume inawaomba wananchi wa Mikoa hii kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao.

Mwisho, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa pole kwa wafiwa, majeruhi na wote walioguswa na ajali hii na tunamuomba Mwenye Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na majeruhi wote wapone kwa haraka.

Imetolewa na:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM,
Alhamisi, Julai 19, 2012.

Wachungaji wa DECI wakutwa na hatia



Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WACHUNGAJI watano ambao pia ni Wakurugenzi wa Taasisi ya Kuendesha na Kusimamia upatu (DECI) waliokuwa wakifanya hivyo bila kibali wamekutwa na kesi ya kujibu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Stewart Sanga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Washitakiwa hao ni Dominick Kagendi, Jackson Mtares, Timotheo Ole Loitinye, Arbogast Kipilimba na Samuel Mtares.

Hakimu huyo alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 16 na vielelezo kadhaa kutoka upande wa mshitaka, bila kuacha shaka mahakama imewaona watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu.

Washitakiwa waliomba mahakama kuwapa nafasi ya kuwasiliana na mawakili wao ili waweze kupanga kama watatoa ushahidi kwa njia ya kiapo au la.

Katika kesi hiyo washitakiwa wanadaiwa kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume cha sheria pamoja na kupokea amana za umma bila leseni. 

Washitakiwa walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana
Chanzo: Mtanzania

Kizimbani kwa kutaka kuua kwa sindano ya sumu



Na Asifiwe George, Dar es Salaam
WATU wawili, Hussein Saidi (21), mkazi wa Tanga na Deogratus Rutaganda (52), mkazi wa Tabata Kimanga, wamefikishwa Mahakama ya Ilala kwa kosa la kujaribu kuua kwa kutumia sindano yenye dawa iitwayo Diazinon.

Wakisomewa shitaka lao na Mwendesha Mashitaka, Munde Kalombola mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda, alidai Julai 11, mwaka huu, saa tatu usiku, washitakiwa walitenda kosa la kujaribu kumuua Consolata Rutagandama kwa kutumia sindano yenye sumu.

Alisema washitakiwa kwa kutumia sindano yenye dawa hiyo walimvizia Rutagandama na kutaka kumchoma kwa lengo la kutaka kumuua.

Kwa upande wa Jamhuri ulisema upelelezi bado haujakamilika na uliomba Mahakama kupanga tarehe ya kusoma kesi hiyo ili kutoa nafasi upande wa upelelezi kufanya kazi yao.

Hata hivyo, washitakiwa walikana kosa hilo na wamerudishwa rumande kutokana na kesi yao kutotimiza masharti ya dhamana hadi Julai 30, mwaka huu itakapotajwa tena.

Aidha, walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wakiwa na dhamana ya Sh milioni moja kila mmoja pamoja na vitambulisho.

Wakati huohuo, mkazi wa Jangwani jijini Dar es Salaam, Austino Gasto (20), amefikishwa Mahakama ya Ilala kwa kosa la kujaribu kubaka.

Akisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashitaka, Credo Rugajo, mbele ya Hakimu Pamela Kalala, alidai Julai 6, mwaka huu, mtuhumiwa alitaka kumbaka Anita Jafesi (18) huko katika maeneo ya Ocean Road, karibu na Hospitali ya Aga Khan.

Kwa upande wa Jamhuri, ulidai upelelezi bado haujakamilika na uliomba Mahakama kupanga tarehe ya kusoma kesi hiyo ili kutoa nafasi kwa upande wa upelelezi kufanya kazi yake.

Mshitakiwa alikana kosa hilo na amerudishwa rumande kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana hadi Julai 25, mwaka huu, itakapotajwa tena.

Washitakiwa walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wakiwa na dhamana ya Sh milioni moja kila mmoja pamoja na vitambulisho.
Chanzo: Mtanzania

Kikongwe ‘ampiga singi’ shahidi mahakamani


Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
KIKONGWE amenusurika kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na umri wake, baada ya kumpiga singi shahidi aliyekuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kusafirisha binadamu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Salex Tannery Ltd, Salim Ally (60).

Ushahidi ulianza kutolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mashahidi wawili upande wa mashitaka walifanikiwa kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi, Illivin Mugeta.

Wakati shahidi wa pili, Raufu Byabato, akiendelea kutoa ushahidi akieleza jinsi walivyonyanyasika nchini Yemen hadi kufikia hatua ya kuwa ombaomba, aliingia mzee huyo wa Kiarabu asiyeweza kutembea vizuri kutokana na umri wake.

Kikongwe huyo ambaye ni ndugu wa mshitakiwa, aliingia na kupishwa mahali pa kukaa na wasikilizaji wengine, alikaa katika benchi nyuma ya shahidi kwa muda wa nusu saa akisikiliza kesi hiyo, ndipo alipoinua mkono wake na kumsukumiza singi kichwani shahidi.

Shahidi aliyekuwa akitoa ushahidi huku analia aliendelea kutokwa na machozi, huku ndugu wa mshitakiwa wakisaidiana kumshika mkono mzee huyo na kumtoa nje.

“Huyu mzee asirudi tena mahakamani,” hayo yalikuwa maneno ya askari magereza aliyesimama mlangoni kwa ajili ya usalama.

“Shahidi huyu ni mzee tumsamehe, punguza hasira. Ninahitaji ulinzi kwa shahidi wangu, rudi nyuma,” hakimu alitoa amri hiyo kwa mzee mwingine aliyetaka kukaa nafasi iliyoachwa na kikongwe aliyetolewa nje.

Byabato aliendelea kutoa ushahidi ambapo alidai walikwenda Yemen kwa makubaliano ya kujenga nyumba ya mshitakiwa Januari, 2010 na walikaa huko kwa miezi sita bila malipo yoyote, japo kazi walifanya katika nyumba za mshitakiwa.

“Tulikaa miezi sita Yemen, tulijenga ghorofa moja yenye vyumba 56 na nguzo 80, tulifanya ukarabati wa nyumba ya Mzee Salim, lakini hatukulipwa ujira wowote na tulipomwambia Abdulswamad kwamba hatufanyi kazi tena akatuambia tuendelee hatutadhulumiwa malipo yetu,” alidai Byabato.

Alidai Abdulswamad waliyekwenda naye ndiye aliyepaswa kuwalipa fedha hizo, kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa kakubaliana na mshtakiwa kwamba kuna kazi Yemen na kwamba hajui walikubaliana malipo kiasi gani.

Shahidi alidai chumba walichokuwa wamefikia na huduma ya chakula waliyokuwa wakipata bila kujua aliyekuwa akilipa gharama hizo, vyote baada ya muda vilisitishwa, hivyo walikuwa wanaomba omba misaada kwa watu mbalimbali wakiwamo marafiki wa mshitakiwa na viongozi wa msikitini.

“Tuliishi kwa kusaidiwa, hati zetu za kusafiria zilichukuliwa, tulianza kuuza vifaa vya kazi ikiwamo jenereta, mashine ya kukatia vigae na mashine ya kukata vyuma,” alidai shahidi huku anabubujikwa na machozi.

Alidai baada ya kushindikana kupata malipo yao kutoka kwa mshitakiwa walikwenda kutoa taarifa polisi na kwa mkuu wa mkoa ambapo walipewa barua ya kuwasaidia kupata haki yao lakini hawakufanikiwa.

Byabato alidai alitafuta namba ya simu ya mjomba wake, Kanali Ngimela Lubinga akampigia kwa ajili ya kuomba msaada wa kurudi walikotoka.

Kanali Lubinga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, alisaidia kutoa taarifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya kuwasaidia waweze kurudi nchini.

DC Lumbinga alifanikiwa kuwapatia msaada walalamikaji wakapata hati zao za kusafiria na walirudishwa kwa msaada hadi Dar es Salaam. Kesi inaendelea leo kwa mashahidi wengine kutoa ushahidi.

Upande wa mashitaka katika kesi hiyo unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila na upande wa utetezi unaongozwa na wakili Majura Magafu.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa Agosti 8, 2010, mshitakiwa alimsafirisha Abduswamadu Omary kutoka Tanzania kwenda Yemen kwa kusingizia kuwa anakwenda kumtafutia ajira na badala yake alimtumikisha kazi za lazima.

Ilidaiwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 4 kidogo cha (1) (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2008 cha kuzuia kusafirisha binadamu.
Chanzo: Mtanzania


 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa