Home » » MAJAMBAZI YAPORA TABATA

MAJAMBAZI YAPORA TABATA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki

Kundi la watu watano wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia duka la jumla la vinywaji na la wakala wa huduma za pesa kwa njia ya simu ya mkononi usiku wa kuamkia juzi, maeneo ya Tabata Magengeni, jijini Dar es Salaam.

Majambazi hao walifanikiwa kupora kiasi cha Sh. milioni 2.8/- mali ya Jerome Urassa, mkazi wa Tabata wilayani Ilala.

Mmiliki wa maduka hayo, alisema kuwa majambazi hayo yalifanya uporaji huo saa 1:00 usiku kwa kuwatishia wafanyakazi wake kwa bastola.

“Nilijulishwa taarifa za tukio na wafanyakazi wangu, nikaja nilipofika nikaelezwa jinsi hali ilivyokuwa, haikuchukua muda polisi walifika na kuanza kuchukua maelezo ya awali, tulivyofanya hesabu tuligundua duka la vinywaji Shilingi milioni moja ziilibiwa huku  lingine zikiibiwa Sh. milioni 1.8,” alisema Urassa.

Kwa upande wake, mfanyakazi Laurent Kimario, alisema walifika watu wawili mmoja akiwa na bastola huku mwingine ameshika chupa ya bia na walipofika karibu walimsukumiza ndani ya duka na kumuamuru aonyeshe fedha zilipo.

“Walivyoingia ndani waliniamuru nikae chini niseme mahala pesa zilipo la sivyo wataniua, aliyeshika chupa alifungua droo akakosa hela niliwaonyesha, walipotoka nje walipiga  risasi moja hewani,” alisema Kimario.

Mfanyakazi mwingine wa duka la pili, Gervas Maliseli, amesema majambazi hao wakati wanamvamia walimkuta akiwa katika harakati za kumhudumia mteja aliyekuwamo ndani.

“Walipoingia dukani walinitaka nitoe hela nilizokuwanazo, sikuwabishia niliwapa, hawakuishia kwangu tu walimpora mteja pia kiasi cha Shilingi laki kisha wakatokomea kwa kutumia pikipiki,” alisema Maliseli.

Shuhuda wa tukio hilo, Jeremia Josia, alisema wakati tukio likiendelea alikuwa amekaa nje karibu na biashara yake ya matunda ndipo aliposikia kelele zikitoka ndani ya maduka hayo akiwa anatafakari jambazi moja llilitoka na kupiga risasi iliyosababisha taharuki.

Aidha, alisema walipomaliza kufanya tukio walitokomea kwa kutumia pikipiki mbili ya kwanza ikibeba wawili na ya  pili watatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, hakupatikana na simu yake iliita na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa