Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hussein Makame, NEC
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst.
Damian Lubuva ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
kujifunza uzoefu wa tendaji wa Tume ya
Kudumu ya Uchunguzi (TKU) ili kuimarisha utawala bora nchini.
Jaji Mst. Lubuva ametoa wito huo wakati akeleza
uzoefu wake juu ya utendaji kazi wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (TKU) wakati wa
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Tume hiyo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee
jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na TKU kukabiliwa na changamoto
nyingi katika inatekeleza majukumu yake wakati huo lakini ilifanya kazi zake
kwa ufanisi kutokana na malalamiko ya wananchi yaliyoshughulikiwa kwa wakati
huo.
“Katika hali na mazingira ya Tume ya wakati huo,
bila kusita nashawishika kusema kuwa Tume ya Kudumu ilianzishwa wakati ambapo
si watu wengi kwa bahati mbaya Afrka ambao walijali haki za binadamu na utawala
bora” alisema Jaji Mst. Lubuva.
Aliongeza kuwa itakuwa si kusifia kusema kuwa TKU
ilifanya kazi nzuri katika kipindi chake cha miaka 32 kwani ulikuwa wakati
ambapo Tanzania ndio ilikuwa imejikomboa kutoka utawala wa Kikoloni na
ilijitahidi kuendesha shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Hata hivyo alisisitiza kuwa walithubutu kwa mwalimu
kuleta wazo la kuanzisha TKU ili kunusuru wananchi kutakona na madhila ya
matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi na watendaji kwa wakati huo.
“Kwa upande mwingine Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora ina kibarua kizito katika kutekeleza majukumu yake katika
mazingira ya sasa ambapo tume hii si rahisi kuelezea kwa wananchi kwa nini
isifanikiwe zaidi ya TKU”
Alisema THBUB tofauti na TKU ina bahati ya
kujifunza kutokana na uzoefu wa tume hiyo ya kudumu katika mazingira ya sasa kulinganisha
maendeleo na uelewa wawananchi kiujumla kuhusu haki zao za kimsingi kisiasa na
kiutawala.
“Hivyo tunaposherehekea miaka 50 ya Tume ya
Uchunguzi ni halali kusema kwamba ilikidhi haja na matakwa ya wananchi kwa
wakati huo kuweka misingi imara ambayo THBUB itaitumia katika juhudi za kusonga
mbele”alisema Jaji Mst. Lubuva.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Menejiment ya Utuishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki alisema lengo kubwa la
Serikali kuanzisha TKU ilikuwa ni kumlinda mwananchi na lilifanikiwa kwa
kushughulikia malalamiko 39,000 kwa kipindi cha miaka 35.
“Aidha malalamiko yaliyopokelewa katika kipindi
cha miaka 15 (2001-2016) ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni 32,000
na hivyo kufanya idadi ya malalamiko ya miaka 50 kufikia 71,000” alisema Mhe.
Waziri Kairuki na kuongeza kuwa:
“Idadi hiyo inaonesha jinsi vyombo hivi vilivyo na
manufaa kwa wananchi wanyonge.Baadhi ya malalamiko yaliyopokelewa ni kuhusu
vitendo vya unyanyasaji, masuala ya utumishi, kuchelewa kutekeleza wajibu, ,
kukataliwa kuomba rufaa, kutrofuata taratibu za kisheria, mirathi, matumizi
mabaya ya mali ya umma na migogoro ya ardhi”
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora Bahame Nyanduga alisema Maadhimisho ya Miaka 50 ya TKU yamekwenda
sanjari na kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuanzisha Tume
hiyo ikiwa ni taasisi ya kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma kwa
wananchi.
“Pili ni kujikumbusha huko tulikotoka na kujifunza
kutokana na kazi za TKU, changamoto na na mafanikio iliyoyapata na mwelekeo
unaotakiwa katika kuhakikisha dhana ya uwajibikaji na utawala bora
zinaendelezwa nchini Tanzania” alisema Nyanduga.
Katika maadhimisho hayo Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi walipata Tuzo na Cheti cha kutambua
mchango wao kuweka misingi ya uwajibika na utawala Bora.
0 comments:
Post a Comment