Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MCHANGO WA MWL.NYERERE KATIKA KUIMARISHA UHUSIANO WA TANZANIA NA NCHI ZA NJE

MCHANGO WA MWL.NYERERE KATIKA KUIMARISHA UHUSIANO WA TANZANIA NA NCHI ZA NJE


 
 Na. Immaculate Makilika-  MAELEZO
 
Kati ya mafanikio makubwa ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni  kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi nyingi za jirani na hiyo  imeifanya Tanzana iitwe “Kisiwa cha Amani”.
 
Mwl. Nyerere amepanua wigo wa siasa ya Tanzania na  mataifa ya nje ambapo ameimarisha  uhusiano, ushirikiano na kuunga mkono vyama halisi vya Ukombozi wa Afrika kama vile FRELIMO ya Msumbiji, ZANU-PF ya Zimbabwe, ANC ya Afrika Kusini na MPLA ya Angola bila kusahau SWAPO ya Namibia pamoja na mataifa yaliyopo mabara ya Ulaya, Amerika  na Asia.
 
‘Tukiimarisha kushirikiana kwetu, tukielewa kuwa vita vyao ni vita vyetu, tutaongeza sana nguvu zetu za kuleta ukombozi wa Afrika nzima’ anasema Mwl. Nyerere.
 
Katika nukuu za Mwl. Nyerere, amewahi kusema “Uhuru wetu hauwezi kuwa kamili kama jirani zetu hawajapata uhuru.” Hii inadhihirisha jinsi gani muasisi huyu wa Tanzania alivyokuwa na dhamira ya dhati ya kushirikiana na mataifa mengine ya kiafrika.
 
Katika Azimio la Arusha Mwl. Nyerere amewahi kusema Tanzania iko tayari kushirikiana kirafiki na nchi yoyote yenye nia njema  bila kujali kama nchi hiyo ni ya upande wa Mashariki, kwa maana ya nchi zenye mlengo wa Kijamaa au Kikomunisti au Magharibi, zenye mwelekeo wa kibepari.
 
Aidha,  Mwl. Nyerere amesisitiza  juu ya  wajibu wa kuimarisha  ushirikiano na kuungana mkono  nchi za kimapinduzi za Afrika, kwa vile aliamini kuwa nchi zote zimo katika jahazi moja, yenye  safari moja, akiwa na maana ya mazingira na hali za kufanana za nchi  hizo.
 
Katika kipindi cha Utawala wake wa Awamu ya Kwanza na hata baadae Mwl. Nyerere ameshiriki katika jitihada mbalimbali za kusaidia mataifa ya kiafrika kujipatia Uhuru wake, pamoja na kutatua migogoro iliyokuwepo katika nchi hizo. Amekuwa Mwenyekiti wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa Afrika pia amekuwa msuluhishi wa migogoro ya Burundi.
 
Hali hiyo imesaidia Tanzania kuwa nchi yenye mahusino mema na nchi mbalimbali duniani bila kujali itikadi zao wala miongozo yao.
 
Kutokana mchango na jitihada za Mwl. Nyerere, Tanzania imekua kivutio cha wageni wengi kutoka nje, kuanzia wanasiasa wa kimataifa na wasomi kutoka Marekani, Ulaya Magharibu na kwingineko.
 
Wasomi hao wa Kimataifa  kutoka maeneo mbalimbali  walikuja kujionea  na kufanya utafiti juu ya sera ya Tanzania siri iliyomwezesha Mwl. Nyerere kuiweka Tanzania katika ramani ya Dunia.  
 
Pembuzi zao nyingi zilimwelezea Mwl. Nyerere  kama “Roho ya Afrika na tumaini la wasomi, wanasiasa wa Afrika na Dunia nzima”, kila neno lake lina thamani kubwa, lenye kupimwa na kuchanganuliwa kwa makini na nchi za Magharibi na za Mashariki.
 
Kitendo hicho cha jamii ya kimataifa kumfananisha Mwl. Nyerere  na wafalme wa nchi za ustaarabu wa kwanza Duniani, kama Julius Ceasar, Suleimani na Richard wa II, ni uthibitisho tosha kwamba kipaji chake kilivutia wengi.
 
Baadhi ya viongozi waliofurahishwa na uwezo wa Mwl. Nyerere ni pamoja na Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter ambaye mwaka 1977 alimsifia na kumwelezea Mwl. Nyerere kama “ Rais Mwandamizi, msomi, mwanafalsafa aliyetukuka na mwandishi mahiri”.
 
Imewahi kuelezwa kuwa Rais Carter alichukua daftari (notebook) na kuandika kila kitu alichokuwa  akisema Mwl. Nyerere na baadae gazeti moja nchini humo liliandika “Inapotokea Rais wa Taifa kubwa kumnukuu Rais wa Kiafrika” inaonesha ni  jinsi gani busara ya Mwl. Nyerere ilivyoheshimika na mataifa makubwa.
 
Mwl. Nyerere ameimarisha mahusiano baina ya nchi kadhaa  na Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi hizo na uhusiano huo umezaa matunda ambayo ni msaada katika kukuza uchumi wa nchi husika pamoja na kuchangia maendeleo kwa kutoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira, masuala ya kidiplomasia ama  utatuzi wa migogoro, sekta za viwanda, afya, kilimo, elimu, teknolojia na biashara.
 
Mchango wa Tanzania katika harakati  za ukombozi wa nchi za kusini  mwa Afrika ambazo bado zilikua zikikaliwa kimabavu na wakoloni  katika nchi za Zimbabwe, Msumbiji , Angola,  Namibia na Zimbabwe zimeimarisha uhusiano kati ya nchi hizo na Tanzania.
 
Kuwapatia  hifadhi salama  vyama vya ukombozi vya mataifa, pamoja na rafiki wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Dr. Kenneth David Kaunda (aliyekuwa rais wa Zambia) ulisaidia  jitihada za kuikomboa Afrika hususani Kusini mwa Afrika. 
 
Aidha,  kupitia uhusiano uliojengwa wakati huo kati ya Mwl.  Nyerere na Kenneth  Kaunda ulifanikisha   azma  ya biashara ya nchi ya Zambia iliyokuwa ikiuza  shaba kwa kiwango kikubwa katika  nchi za China, Ujerumani na kwingineko kwa kujenga   reli ya TAZARA kutokana na ufadhili wa Serikali ya China  kutoka Dar es Salaam hadi ukanda wa shaba nchini Zambia. 
 
Reli  hiyo ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yao, lakini pia ndiyo reli bora zaidi kujengwa Duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
 
Mwl. Nyerere hakuishia Afrika pekee, ameimarisha mahusiano baina ya Tanzania na China ambayo kwa hakika yamekua yakileta  faida kubwa  kwa nchi zote mbili.
 
Ni kutokana na mahusiano hayo mema kati ya Tanzania na China, ndio kumezaa matunda  yaliyochangia   juhudi zilizofanywa na Meya wa Mji wa Musoma Bw. Kisusura Malima na  aliyekuwa  Balozi Mdogo wa China nchini  Li Xuhang  alipokuwa mkoani Mara kuadhimisha miaka 50 ya Urafiki wa Tanzania na China.
 
Juhudi hizo ni katika  kuwaenzi  wanamapinduzi, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na muasisi wa Taifa la China, Mao Zedong, kwa kuunganisha mji wa Musoma kilipo kijiji cha Butiama alipozaliwa Mwalimu na Jiji la Xiang Tan nyumbani kwa Mao mwasisi wa China.

Miji hiyo inaungana kuifanya Butiama na Mara kuwa kivutio cha utalii, uwekezaji kibiashara na kitaaluma kwa kushirikiana Xiang Tan jiji lenye maendeleo makubwa.
 
Mahusiano mazuri ya Mwl. Nyerere yalishamiri pia katika taasisi mbalimbali duniani,  kwa mfano Robert Mac Namara, Rais wa zamani wa Benki ya dunia aliita Tanzania “kipenzi” chake cha Afrika.
 
Naye, Gavana Jerry Brown wa Marekani alipotembelea Tanzania, alikaa juu ya magoti ya Mwl. Nyerere  kwa kile alichosema “aweze kujifunza maajabu ya bara la Afrika kutoka kwa bingwa wa masuala ya Afrika na Dunia”.
 
Ikumbukwe kuwa  Mwl. Nyerere amekuwa na ushawishi  mkubwa na alitoa wazo la kuunda mashirika mbalimbali yanayoziunganisha nchi za Afrika ikiwa ni hatua mojawapo ya kuelekea kuunda Afrika  moja, hivyo mashirika kama vile SADC, ECOWAS, COMESA, EAC na kadhalika yaliundwa katika kufikia azma ya kuunganisha nchi za Afrika, na hivyo mashirika hayo yamekua yakiendelelea kufanya kazi hadi sasa.
 
Ni dhahiri kuwa Tanzania imendelea kuaminika  na kuwa kinara katika masuala ya  diplomasia na amani  duniani kote na kuifanya kuwa na mahusiano yaliyoimarika katika nchi  mbalimbali . Na hiyo ikiwa ni juhudi zilizofanywa na Mwl. Nyerere wakati wa utawala wake na hata baada.
 
Hakika mchango wake wa kukuza uhusiano wa Kimataifa na Tanzania utakumbukwa vizazi hadi vizazi.
 
Mwisho
 
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa