Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » NEC yatoa wito kutoa elimu ya mpiga kura kwa vyombo vya habari

NEC yatoa wito kutoa elimu ya mpiga kura kwa vyombo vya habari



Hussein Makame, NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyombo vya habari kuialika tume hiyo iwapatie elimu ya mpiga kura ili kukuza uelewa wa vyombo hivyo juu ya sheria, kanuni, na taratibu zinazoongoza uchaguzi na kufahamu majukumu ya tume hiyo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani wakati akieleza tathmini yake juu ya elimu ya mpiga kura inayotolewa na tume hiyo ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Alisema NEC imejipanga kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima na iko tayari kupokea maombi ya kwenda kutoa elimu hiyo kwa wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na wafanyakazi wote wa vyombo hivyo ili kukuza uelewa wa sekta hiyo.

“Niwaombe vyombo vya habari, tumeanzisha programu ya elimu ya mpiga kura tualikeni kwenye vyombo vyenu vya habari, mtualike tuje tuzungumze na nyinyi vyombo vya habari kimoja baada ya kingine” alisema Bw. Kailima na kufafanua kuwa:

“Sisi tunataka kuzungumza na wewe mmiliki wa chombo na watumishi wako na viongozi wenzako wote ili tukueleweshe kuhusu Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, utaratibu mzima wa uchaguzi na uijue Tume ili unapoandika ujue ninachoandika si cha kubahatisha”

Bw. Kailima alisema elimu hiyo kwa vyombo vya habari pia itaviwezesha kuwa na uelewa mpana juu ya masuala mbalimbali ya uchaguzi na kutoa changamoto kwa mtendaji huyo wa NEC pindi anapopata na nafasi ya kuzungumza nao.

Katika kutekeleza mkakati endelevu wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, Bw. Kailima ameanza kutoa elimu hiyo kupitia televisheni mbalimbali nchini na kwamba yuko tayari kuzungumza na vyombo mbalimbali kutekeleza mkakati huo.Kwa upande mwingine, Bw. Kailima amewataka Watanzania wakisikia kuna maonesho au mkutano ambapo Tume inashiriki wafike banda la NEC waulize maswali wapate ufahamu na watapata uelewa mkubwa juu ya mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza kwa nyakati tofauti, Bw. Kailima alisema NEC itahakikisha inatumia maonesho, mikutano na mikusanyiko mbalimbali ikiwemo mikutano ya kidini ili kutoa elimu ya mpiga kura ikiwemo shule za sekondari nchini.Alisema lengo kuu la kutekeleza hayo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 wananchi wawe wamepata uelewa wa kutoa kuhusu taratibu za uchaguzi na kufahamu majukumu ya Tume ili kupunguza malalamiko na upotoshaji unaofanywa katika kipindi cha uchaguzi.

Tayari Bw. Kailima ameshatoa elimu ya mpiga kura kupitia televisheni za Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na Televisheni ya Afrika Mashariki (EATV) na amesema NEC inajipanga kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.Alisema aidha NEC itatoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuziomba Asasi za Kiraia zinazoweza kutoa elimu ya mpiga kura kutuma maombi ili kupatiwa ridhaa ya kutoa elimu hiyo kwa umma.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa