Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Pikipiki zawaongeza ufanisi wa kazi Waratibu Elimu Mkoa wa Dodoma

Pikipiki zawaongeza ufanisi wa kazi Waratibu Elimu Mkoa wa Dodoma

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Lilian Lundo - MAELEZO - Dodoma

Ugawaji wa Pikipiki kwa Waratibu Elimu Kata Mkoa wa Dodoma umeleta mafanikio makubwa katika nyanja ya elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu ndani ya mkoa huo.

Hayo yamesemwa na Mratibu Elimu Kata wa Sanzawa Wilaya ya Chemba Sweetbert Malimi, leo Mjini Dodoma katika semina ya Waratibu Elimu inayoendelea Mjini hapo.

"Pikipiki imeniwezesha kushughulikia kwa wakati matatizo yanayotekea katika shule ninazozisimamia, vilevile kufuatilia kwa wakati maendeleo ya taaluma ya wanafunzi pamoja na ufundishaji wa walimu", alifafanua Malimi.

Ufuatiliaji huo umeletea mafanikio makubwa katika Mkoa wa Dodoma, ambapo ufaulu wa darasa la saba kwa wilaya ya Chemba peke yake ulipanda kutoka asilimia 30 mwaka 2015 mpaka asilimia 46 mwaka 2016. 

Kwa upande wake Mratibu Elimu Kata wa Songambele iliyoko Wilaya ya Kongwa amesema kuwa katika kata yake ana shule Sita za kuzifuatilia ambapo kabla ya kupata pikipiki alikuwa anatumia baiskeli kutembelea shule hizo na aliweza kutembelea shule hizo mara moja kwa wiki.

Aliendelea kwa kusema kuwa, baada ya kupata pikipiki anauwezo wa kutembelea shule hizo mara tatu hadi nne kwa wiki akifuatilia maandalio ya walimu, maazimio ya kazi, utengenezaji wa zana za kufundishia, mahudhurio ya wanafunzi pamoja na kuhudhuria vikao vya kamati ya shule.

Aidha amesema kuwa, kutokana na ufuatiliaji huo wa mara kwa mara katika shule hizo kumepelekea umakini mkubwa wa ufundishaji wa walimu kwa kufuata taratibu za ufundishaji kama vile kuwa na maandalio, maazimio ya kazi pamoja na kuwa na zana za ufundishaji.

Serikali kwa kushirikiana na Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) ilitoa jumla ya Pikipiki 192  kwa Waratibu Elimu Kata wote wa Mkoa wa Dodoma mwaka 2014 na 2015. Pikipiki hizo zimekuwa zikitumika na Waratibu hao kufuatilia maendeleo ya taaluma ya shule wanazozisimamia.

Mwisho


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa