Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TWANGA, PAPII, BABU SEYA KUTUMBUIZA TAMASHA LA WAFUNGWA UKONGA KESHO

TWANGA, PAPII, BABU SEYA KUTUMBUIZA TAMASHA LA WAFUNGWA UKONGA KESHO

papii
Wanamuziki wakongwe wanaotumikia kifungo cha maisha ndani ya Gereza la Ukonga, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.
TAMASHA kubwa la wafungwa linatarajiwa kuunguruma kesho kuanzia saa 2 asubuhi na habari njema ni kwamba, Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ itatum-buiza sambamba na wanamuziki wakongwe wanaotumikia kifungo cha maisha ndani ya Gereza la Ukonga, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.Pia msanii wa Singeli, Msaga Sumu ataporomosha burudani.

Tamasha hilo lenye lengo la kuwatia moyo wafungwa na kuwaonesha kwamba wapo pamoja na Watanzania wenzao ambao wanaishi huru litakuwa la aina yake kwani mbali na burudani kamambe kutoka kwa Twanga Pepeta, mhamasishaji mashuhuri Afrika Mashariki na Kati, Eric Shigongo atakuwepo kuwatia moyo wafungwa.
twanga
Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’
Shigongo ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Global Publishers, Wachapishaji wa Magazeti ya Ijumaa Wikienhemda, Uwazi, Risasi, Amani, Ijumaa na Championi, amesema anatambua wafungwa waliopo gerezani nao wanahitaji faraja na kutiwa moyo kwa namna moja au nyingine, kwani nao walikuwa na ndoto zao hivyo kuwatia moyo ni jambo jema.

“Hii si mara ya kwanza kwa Global kuandaa tamasha la namna hii, mwaka 2008 tuliandaa, tunapozungumza pamoja na ndugu zetu waliopo gerezani huwa nao wanafarijika.

“Wanaona tuko nao pamoja. Mtu kufungwa haimaanishi kwamba hana maisha tena, haimaanishi kwamba hawezi kutimiza ndoto zake, haimaanishi kwamba alikuwa mkosaji sana asiyefaa katika jamii.
“Bado mfungwa ana nafasi ya kujitunza, kuwa na malengo, kujiandaa na kutimiza ndoto zake pindi wakitoka gerezani. Mifano ninayo mingi tu, kuna wafungwa ambao tulizungumza nao mwaka 2008, kesho hii wameshatoka na wanakuja ofisini kwetu kutushukuru.
live3
Msanii wa Singeli, Msaga Sumu.
“Wanasema kupitia tamasha lile tuliwatia moyo na walibadilika na sasa wanaishi vizuri katika jamii zinazowazunguka na wanafanya biashara mbalimbali na wana mafanikio makubwa tu,” alisema Shigongo.
Mratibu wa tamasha hilo, Juma Mbizo, amesema mbali na burudani kali kutoka kwa Twanga, kutakuwepo na michezo mbalimbali kama ya mpira wa miguu, kuvuta kamba na mingineyo ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi.
“Kama unavyojua Ijumaa itakuwa ni Nyerere Day, hivyo tutamkumbuka muasisi wa taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuimba, kucheza pamoja na wafungwa.
“Twanga wataporomosha nyimbo zao kali. Wanamuziki wote wakali wa Twanga watakuwepo, wataimba pamoja na wanamuziki waliopo gerezani.

“Kuna wanamuziki maarufu waliotamba enzi hizo kama Papii Kocha na Babu Seya ambao wanatumikia kifungo chao cha maisha, nao watatumbuiza siku hiyo, tutapata fursa ya kuwaona live ndani ya Gereza la Ukonga,” alisema Mbizo.

Pamoja na maneno mazuri ya kutia moyo yatakayotolewa na Shigongo, Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Stephen Mwaisabila naye anatarajiwa kutoa neno katika tamasha hilo sanjari na viongozi wengine wa magereza.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa