Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Ziara ya Mfalme wa Moroko ni Fursa kwa Wafanyabiashara

Ziara ya Mfalme wa Moroko ni Fursa kwa Wafanyabiashara

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Immaculata Makilika- MAELEZO
Moroko ni nchi iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Afrika, ambayo imepakana na bahari za Atlantiki na Mediteraniani, na upande wa bara imepakana na nchi za Algeria, Mauritania.mpaka wa kusini unatajwa kuwa Sahara Magharibi.
Nchi ya Moroko inakadiriwa kuwa na eneo la Km2 446,550, huku sehemu kubwa ikiwa ni jangwa la Sahara na watu wengi nchini humo huishi kwenye sehemu zilizo na rutuba hasa karibu na maeneo ya pwani.
Nchi hiyo ina milima inayofunika eneo kubwa, ikiwemo milima ya Atlas ambayo ipo katikati ya nchi hiyo kutoka kusini magharibi kuelekea upande wa kaskazini mashariki na mji mkuu wake ukiwa ni Rabat wenye wakazi milioni 2, aidha mji mkubwa ni Casablanka.
Nchi ya Moroko ilipata uhuru wake mwaka 1956 kutoka kwa nchi za Ufaransa na Hispania zilizokuwa zikiitawala, na kikatiba  inaongozwa na Mfalme, kwa sasa inaongozwa na  mfalme anayeitwa Mohammed wa VI, na Waziri Mkuu  ni Abdelilah Benkirane.
Watu wa Moroko hutumia lugha rasmi za  kiarabu na kiberiberi. Fedha yao inajulikana kama Dirham, zaidi ya 90% ya watu wake ni waislamu.
Uchumi wa Moroko unategemea zaidi utalii, sekta ya mawasiliano, viwanda vya nguo pamoja na kilimo.
Hivi karibuni,  kwa mara ya kwanza tunashuhudia ziara ya Mfalme wa Moroko Mohammed wa VI aliyewasili nchini wiki hii kwa ziara ya siku tatu hadi Oktoba 25 mwaka huu.
Ujio wa Mfalme huyo wa Moroko unaidhihirishia dunia  kwa kiasi gani diplomasia ya Tanzania imeendelea kukua kwa kasi, ikiwa ni sambamba na kukuza diplomasia ya uchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi  Augustine Mahiga anasema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukuza uhusiano wa kati ya Tanzania na Moroko hususani katika masuala ya uchumi na biashara kwa faida ya watu wa nchi hizi mbili.
“ Ziara hii imejikita zaidi katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na biashara, ikizingatiwa kuwa nchi ya Moroko imefanikiwa katika nyanja mbalimbali kama vile miundombinu, afya, madini  na ulinzi”.
“Vile vile  wafanyabiashara kutoka Moroko watafanya mazungumzo  na wa hapa nchini kwa lengo la kubadilishana uzoefu na ni hatua nzuri itakayoweza itakuza uhusiano wetu pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi” anasema Balozi Mahiga.
Maroko imepiga hatua katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, uvuvi ,viwanda, kilimo na madini.
Mambo yaliyopo katika mpango huo ni pamoja na maboresho ya reli, na barabara, kuboresha viwanja vya ndege kwa viwango vya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya ndege zinazoingia Moroko. Sambamba na hilo bandari maarufu zimeandaa utaratibu wa safari za kitalii.
Vitu na Maeneo mbalimbali yamekuwa sehemu ya kuvutia utalii kutoka nchi za Ujerumani, Ufaransa, na  Hispania, ambapo huvutiwa na fukwe za bahari,milima ya Atlas, pamoja na miji maarufu ya kama ya Tangie, Marrakech, Casablanka na Tarfaya.
Sekta ya madini ni sekta muhimu kwa vile inachangia uchumi wa nchi kwa  asilimia 6 ya pato la ndani la  taifa na asilimia 35 ya  pato la kigeni kwa nchi ya Moroko.
Ili kukuza sekta ya utalii nchini humo, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  yameimarishwa na kuweza kutangaza vivutio mbalimbali kwa kuhususha sekta binafsi katika kutangaza utalii wa ndani, na kati ya nchi zilizofanikiwa katika hilo ni pamoja na nchi ya Malaysia ambapo mwaka 2011 ilipata watalii milioni 24.7 na mwaka 2012 ilipata watalii milioni 25 kutokana na matumizi ya TEHAMA.
Jitihada mbalimbali zimefanyika katika kusaidia  sekta ya utalii nchini kukua na kuchangia zaidi  pato la taifa, ambapo kupitia maboresho kuongeza ndege zenye safari ya moja kwa moja hadi nchini, na kuboresha miundombinu ya barabara sekta hiyo imeweza kupata mafanikio.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu anasema kuwa  hivi sasa sekta ya utalii inakuwa, ambapo imechangia zaidi katika pato la ndani la taifa mara tatu kuliko sekta ya kilimo iliyokuwa ikichangia zaidi uchumi wa nchi.
“Sasa sekta ya utalii inakusanya dola bilioni 1 fedha ambazo ni  mara tatu zaidi ya sekta ya kilimo, sekta ambayo kwa miaka mingi ilikua ikichangia kwa kiasi kikubwa katika pato la ndani la taifa” anasema Prof. Ndulu.
Kufuatia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi wa nchi, ziara hii ni fursa ya kipekee kwa serikali pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania kwa kujifunza kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa nchini Moroko kwa lengo la kukuza pato na hatimaye uchumi wa nchi.

mwisho

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa