MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli
amembakiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika wadhifa huo
wakati akijaza nafasi zilizokuwa wazi katika Sekretarieti ya chama
hicho.
Aidha, ameendelea kuwaamini wanajeshi katika uongozi wake baada ya
kumteua Kanali Ngemela Lubinga kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, huku kada mwingine maarufu,
Humphrey Polepole akiula.
Katika mabadiliko ya kujaza nafasi zilizo wazi katika Sekretarieti
yaliyotangazwa jana baada ya kikao cha kwanza cha NEC kuongozwa na
mwenyekiti huyo mpya aliyechaguliwa Julai mwaka huu, Polepole ameteuliwa
kuwa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi huku Rodrick Mpogolo akiteuliwa
kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara.
Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye sasa anaondoka kumpisha Polepole,
Nape Nnauye ambaye pia ndiye Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo,
alitangaza uteuzi huo uliobarikiwa na NEC katika kikao chake
kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Aliwaambia wanahabari katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba,
kwamba mabadiliko hayo hayakumgusa Kinana, Katibu wa NEC wa
Oganaizesheni Dk Muhammed Seif Khatib, Katibu wa NC wa Uchumi na Fedha,
Zakia Meghji na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
“Wajumbe wengine ambao sikuwataja hapa watabaki katika nafasi zao.
Hao ni Mheshimiwa Kinana, Mama Meghji, Seif Khatib na Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar, Vuai,” Nape aliwaambia wanahabari jana jioni saa chache baada
ya NEC kukamilisha kikao chake cha siku moja chini ya Dk Magufuli.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Mwenyekiti wa CCM hupendekeza majina
ambayo hupelekwa kwa NEC kwa ajili ya kuridhiwa au kukataliwa, na kwa
mujibu wa Nape, majina hayo matatu yalipitishwa kwa kauli moja.
Wakati Polepole aliyewahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani
Mara, na kada maarufu wa CCM aliyekuwamo katika Tume ya Mabadiliko ya
Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, anamrithi Nape, Kanali Lubinga
anajaza nafasi ya Dk Asha-Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Balozi wa
Tanzania nchini Uingereza, Februari mwaka huu.
Kanali Lubinga alikuwa jeshini kabla ya kupelekwa kuwa Mkuu wa Wilaya
ya Mlele mkoani Katavi kisha kurejeshwa jeshini, ambako amekuwa Msemaji
wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), na sasa anapelekwa
CCM.
Kwa upande wake, Mpogolo ambaye naye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Chato mkoani Geita na kisha Msaidizi wa Rais Magufuli wa Masuala ya
Siasa, anachukua nafasi ya Rajab Luhwavi aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa
Balozi.
Mapema wiki hii baada ya kutangazwa kwa vikao vya Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kulikuwa na hisia za kuwapo kwa
mabadiliko makubwa katika Sekretarieti ya chama hicho tawala baada ya
kuondoka kwa viongozi wengi.
Hao ni kina Luhwavi, Dk Migiro, Dk Pindi Chana aliyekuwa akikaimu
nafasi ya Dk Migiro, pia Nape kushikilia wadhifa wa uwaziri na uteuzi wa
mwishoni mwa wiki wa Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka
kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
Hata hivyo, dalili za kubaki kwa Kinana katika wadhifa wake
zilionekana tangu asubuhi wakati wa ufunguzi wa kikao cha NEC licha ya
mwenyewe kujichomekea kuwa amewekwa kiporo baada ya uteuzi wa mabalozi.
Katika utambulisho wa mabalozi hao wateule pamoja na Mkuu mpya wa
Mkoa wa Njombe, Sendeka, Katibu Mkuu Kinana alieleza kuwa amefahamishwa
kuwa duniani kote ni watu wawili tu wanaotajwa kwa cheo cha Mtukufu, nao
ni Rais na Balozi.
“Jana kuna mtu alinifahamisha kwamba duniani ni watu wawili tu
wanaofahamika kwa cheo cha His Excellence (Mtukufu), akaniambia ni Rais
na Balozi. Akaniuliza sasa wewe ulikosaje kosaje (kicheko kwa wajumbe).
Nikamwambia kuwa Mwenyekiti ameniweka kiporo, atanipa zaidi ya hayo,”
alisema Kinana na kusababisha kicheko kikubwa ndani ya ukumbi wa Ikulu.
Alipotoa shukrani kwa watu mbalimbali, Mwenyekiti wa CCM Taifa,
alimuelezea mbunge huyo wa zamani wa Arusha na Kanali mstaafu wa Jeshi
nchini kuwa “nguzo na hazina muhimu katika chama chetu.”
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment