Na Beatrice Lyimo
MAELEZO
10/12/2016
DAR ES SALAAM.
MAKAMU
wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameitaka Taasisi ya kuzuia na kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) kuongeza kasi ya kuwabaini na kuchukua hatua za
kisheria bila kuwaonea aibu na uoga wahalifu wa vitendo vya rushwa
nchini.
Akizungumza
katika maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu na uzinduzi
wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa yaliyofanyika leo jijini Dar es
salaam, Makamu wa Rais alisema mapambano dhidi ya rushwa hayajaelekezwa
upande wa watumishi wa Serikali pekee, bali pia kwa wafanyabiashara
pamoja na asasi za kiraia.
Samia
alisema Serikali itaendelea kutambua mchango wa taasisi za uwajibikaji
na utawala Bora katika jitihada zao za kuimarisha misingi ya Utawala
bora, uwazi, uadilifu na uwajibikaji.
Taasisi
hizo ni Ofisi ya Rais-(Utumishi na Utawala bora), Takukuru,
Sekretarieti ya Maadili, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Tume ya Haki za binadamu, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma, Ofisi ya
Taifa ya Ukaguzi.
Aidha,
Makamu wa Rais alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika
taasisi hizo ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora za ukaguzi zenye
kuleta tija kwa wananchi na hivyo kuimarisha uwajibikaji na thamani ya
fedha kwenye makusanyo na matumizi ya rasilimali za umma.
“Serikali
imeendelea kuziwezesha kiutendaji taasisi hizi ili kuhakikisha zina
uwezo wa kukuza na kusimamia viwango vya maadili kwa kutoa elimu,
kufanya uchunguzi, kupokea na kuhakiki matamko ya mali na madeni ya
viongozi wa umma kwa lengo la kutekeleza falsafa ya utawala bora”
alisema Samia.
Akifafanua
zaidi Makamu wa Rais alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi
kuwa baadhi ya watumishi na watendaji wa Serikali wamekuwa
wakiwabambikia kesi wananchi wasio na hatia kwa kupata hukumu
zisizostahili, kitendo kinachopelekea kukwamisha maendeleo ya taifa.
Aliongeza
kuwa Serikali katika kuhakikisha inalinda rasilimali za umma, inaondoa
uonevu na dhuluma, kwa kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa TAKUKURU ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Ni
jukumu na wajibu wetu kama Serikali kutoa Ulinzi, Usalama na Huduma
Bora kwa jamii, lakini ufanisi wa kutekeleza wajibu huu utawezekana
endapo watumishi wote wa Serikali watawajibika ipasavyo kuwaongoza
katika utendaji kazi” aliongeza Mama Samia.
Kwa
upande wake Mkurugezi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), Valentino Mlowola alisema kuwa maadhimisho hayo yamelenga
katika kuimarisha nidhamu kwa watumishi wa umma kwa kuzingatia kasi ya
maendeleo ya Taifa.
Naye
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga
alisema kuwa ni mara ya kwanza kwa kampeni hii kufanyika nchini kwa
lengo la kihimiza ukuzaji wa maadili katika utumishi wa umma na katika
jamii kwa ujumla, utetezi na ulinzi wa haki za binadamu, uwajibikaji,
utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufusadi na ubadhilifu
wa mali za umma.
Kampeni
ya siku ya Maadili na Haki za binadamu yenye iliyobeba kauli mbiu
“kujenga na kukuza Maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji, Utawala Bora
na Mapambano dhidi ya Rushwa” imedumu kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia
Novema 10 hadi 10 Desemba mwaka huu.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment