Na: Frank Shija-MAELEZO.
Yapata
miaka 55 imepita ikiwa ni muda ambapo wanajeshi wa lililokuwa jeshi la
Tanganyika walipojikusanya katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam
na kushusha chini bendera ya Malkia wa Elizabeth wa Uingereza na
kupandisha bendera ya Tanganyika ikiwa ni kielelezo cha kuwa sasa
Tanganyika (Tanzania Bara) iko huru kujitawala.
Hivyo
ndivyo ilivyokuwa siku ya tarehe 9 Desemba mwaka 1961 wakati nchi yetu
ikpata Uhuru huku jamaa zetu wa Zanzibar wakipata uhuru wao mwaka 1964
baada ya Mapinduzi yaliyowaondoa Watawala wa Kiarabu katika visiwa vya
Unguja na Pemba. Nchi hizi ziliungana tarehe 26 Aprili 1964 na jina
Tanzania kupatikana.
Nachelea
kusema kuwa hiyo ndiyo hali halisi ya Uhuru wetu, lakini kikubwa
ninachokusudia kujadili katika makala haya ni namna ambavyo wananchi
wamekuwa wakishirikishwa katika shughuli za kuijenga nchi yao na
kujiletea maaendeleo tokea nchi hizi zilipopata uhuru na kuungana.
Hapa
ndipo inapoibuka dhana ya ugatuaji wa madaraka mikoani (kwa wananchi)
ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa zilianzishwa ili kutekeleza na
kukidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 kwa lengo la kuwapa Wananchi uwezo wa kujiamualia masuala yao
ikiwemo uchumi na kuinua hali za maisha .
Katika
Ibara za 145 na 146 ya Katiba imetamkwa wazi kuwepo kwa vyombo vya
wananchi ambavyo vitaanda mazingira wezeshi ya kupeleka madaraka kwa
wananchi na kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika kubuni, kupanga,
kutekeleza na kusimamia mipango ya kijamii na kiuchumi Sera ya ugatuaji
madaraka ya mwaka 1998 imesisitiza kuongeza uwezo wa kifedha kwa Mamlaka
za Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha zenyewe.
Ili
kuimarisha Muungano wetu, Wizara zinazoshughulikia masuala ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa katika pande mbili za Muungano zimejiwekea
utaratibu wa kukutana katika Vikao vya Mashirikiano ambavyo hulenga
katika kubadilishana uzoefu katika utendaji wa sekta ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa.
Wakati
Tanganyika inapata uhuru wake ilikuwa na majimbo kumi ya Utawala ambayo
yalirithiwa toka utawala wa kikoloni wa Kiingereza. Mwaka 1966, Rais wa
Awamu ya kwanza Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere kwa Mamlaka aliyopewa,
aliunda Mikoa 15 na kuondokana na utaratibu wa mgawanyo wa nchi katika
Majimbo.
Madhumuni
ya kuanzishwa kwa maeneo haya ni kusogeza huduma za kijamii na
kiutawala karibu zaidi na wananchi. Kwa upande wa Serikali za Mitaa,
Serikali iliendelea na mfumo wa Serikali za Mitaa iliourithi kutoka kwa
wakoloni na kuutumia kama nyenzo za kuleta maendeleo kwa misingi ya
kidemokrasia.
Kutokana
na changamoto mbalimbali zilizoukabili utendaji wa Mamlaka za Serikali
za Mitaa mara baada ya uhuru na mwanzoni mwa miaka ya sabini, Serikali
ilizifuta Mamlaka hizi mwaka 1972 na kuanzisha Mfumo wa Madaraka
Mikoani.
Mfumo
huu ulizifanya Serikali za Mitaa kuitegemea Serikali Kuu kwa kila
jambo. Kutokana na wananchi kutoshiriki katika maamuzi na pia katika
shughuli za maendeleo, uchumi wa nchi ulididimia na viwango vya maisha
kushuka.
Kutokana
na hali hii, Serikali za Mitaa kwa upande wa Mamlaka za Miji
zilirejeshwa tena mwaka 1978 na mwaka 1984 Serikali za Mitaa upande wa
Mamlaka za Wilaya pia zilirejeshwa.
Ili
kuziimarisha na kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hizi ni kuanzishwa
kwa Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ulioanza mwaka
1998 ambao ulilenga katika kupeleka madaraka kwa wananchi.
Dhana
ya Upelekaji wa Madaraka kwa Wananchi imeelezwa kwa kina zaidi katika
Sera ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1998.
Katika
Sera hii, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapewa uhuru wa kufanya
maamuzi mbalimbali yahusuyo utoaji wa huduma kwa wananchi walio katika
Mamlaka zao na kuwashirikisha katika kujiletea maendeleo na ustawi wao
kwa ujumla. Pamoja na kupewa uhuru huo, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zinatakiwa kuutumia kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi na endapo
zitakwenda kinyume chake, Serikali Kuu inao wajibu wa kikatiba na
kisheria kuingilia kati na kuchukua hatua stahili dhidi ya Mamlaka hizo.
Mfumo
huu umeonyesha mafanikio katika nyanja za usimamizi wa fedha, raslimali
watu, ushiriki wa wananchi katika shughuli za kisiasa pamoja na
mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Ni
kutokana na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo
kulikoleta mafanikio makubwa katika kuongeza fursa za elimu ya msingi na
kupitia mipango ya maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari (MMEM na
MES).
Aidha,
kutokana na shule hizi kuwa katika kila Kata nchini, mwaka 2008
Serikali ilihamishia majukumu la usimamizi wa shule za Sekondari kutoka
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuyaweka chini ya TAMISEMI
wakati huo ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Ni
jukumu letu kulinda mafanikio haya na kukabiliana na changamoto ambazo
zimejitokeza katika kipindi hiki. Katika kutambua nafasi ya Serikali za
Mitaa katika kuleta maendeleo ya wananchi, mwaka 2005 Serikali iliamua
kwamba kila ifikapo tarehe 1 Julai ya kila mwaka iwe ni kilele cha Siku
ya Serikali za Mitaa nchini pote. Katika kipindi hiki, Serikali za Mitaa
hupata muda wa kujitathmini pamoja na kueleza mafanikio iliyoyapata kwa
Wananchi.
Sherehe
hizi hufanyika katika Halmashauri zote na kitaifa hufanyika katika
Halmashauri ambayo huchaguliwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya
Mamlaka za Mitaa Tanzania (ALAT).
Tuendelee
kuimarisha Sekta ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kutimiza
matarajio ya wananchi hapa ndipo tunahitaji zaidi kutumia dhana ya Hapa
Kazi Tu ili kila Mamlaka itimize wajibu wake kwa ukamilifu kwa kutumia
fursa zilizopo kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI George Boniphace Simbachawene anasema
kuwa Sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ilianzishwa kwa lengo la
kushirikisha wananchi katika hatua mbalimbali za kujiletea maendeleo
ikiwa ni njia ya kuwafanya wawe ni sehemu ya maendeleo yao wenyewe.
Simbachawene
anasema kuwa kutokana na sera hiyo Serikali imetenga maeneo mapya ya
kiutawala ili kusogeza karibu zaidi hadi 30, machi 2016 takribani wilaya
sita (6) zimeanzishwa na ikiwemo Mkoa mpya wa Songwe,
Anasema kuwa wilaya zilizoanzishwa kuwa ni pamoja na Wilaya za Songwe (Songwe), Kigamboni (Dar es Salaam), Ubungo (Dar es Salaam), Malinyi (Morogoro), Tanganyika(Katavi), Chalinze (Pwani), na Itigi (Singida).
Katika
mgawanyo huo pia zimeanzishwa mamlaka za Serikali za Mitaa za
Halmashauri za miji za Ifakara (Morogoro), Bunda (Mara), Mbulu
(Manyara),Kondoa (Dodoma), Newala (Mtwara) pamoja na Mbinga (Ruvuma).
Takwimu
zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2016 Tanzania bara ina
mikoa 26, Wilaya 139, Halmashauri 181, Tarafa 562, Kata 3,963, Mitaa
4,037, Vijiji 12,545 pamoja na Vitongoji 64,677.
“Lengo
la kuanzisha maeneo haya ya kiutawala ni kusogeza huduma za kijamii
karibu na wananchi na kuongeza kasi ya maendeleo,” alisema Simbachawene.
Katika kuhakikisha kunakuwepo na ufanisi katika utekelezaji wa dhana hiyo Waziri Simbachawene anasema kuwa
Wenyeviti wa Mitaa, Vijijini na Vitongoji hawana budi kutambua kuwa
dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi pamoja na mambo mengine
inawahimizia viongozi hao kutoa taarifa za mapato na matumizi ikiwemo
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila baada ya miezi mitata kama
kinavyoainishwa kwa mujibu wa sheria.
Dhana
hiyo inataka uwepo uwazi katika kutoa taarifa ili kukidhi matakwa ya
utawala bora, uwazi na uwajibikaji miongoni mwa jamii zetu jambo ambalo
linapunguza kama siyo kuondoa kabisa kero za wananchi.
Katika
moja ya ziara za kikazi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
amewahi kunukuliwa akisema kuwa wajibu wa viongozi wa Serikali za Mitaa
ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua huku huko kwani zipo Mamlaka
kamili zenye wajibu wa kuhudumia wananchi na siyo kusubiri mpaka waje
katika ngazi za juu.
Anasema
kuwa ngazi hizo za madaraka zimeanzishwa ili kurahisisha namna bora ya
kuwahudumia wananchi, ambapo wapo viongozi kuanzaia ngazi ya Kitongoji
hadi Manispaa na Majiji yote hiyo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma
katika maeneo hayo ya kiutawala.
“Sitegemei
kuona wananchi wanakuja kwangu kuleta kero zao nawaagiza mfanye kazi
karibu na wananchi uwepo wenu nyinyi kama viongozi si wa bahati mbaya;
utaratibu huu ulianzishwa mahususi ili kusogeza huduma kwa jamii ili
waweze kujiletea maendeleo, hivyo mshirikiane vizuri naamni kwa kufanya
hivyo tutakuwa tumefanikiwa,” anasema Makonda.
Wadau
mbalimbali wanaeleza kuwa Sera ya kupeleka madaraka kwa wananchi ni
nzuri na imesaidia sana katika kuharakisha maendeleo katika maeneo yao
kwani inawapa fursa ya kushirirki katika kubuni, kupanga na kufanya
maamuzi ya utekelezaji wa miradi ya maenedeleo katika maeneo yao.
Alex
Assenga, mkazi wa mtaa wa Mwongozo, kata ya Makuburi jijini Dar es
Salaam anasema kuwa katika mtaa wao dhana ya ugatuaji wa madaraka
imekuwa na tija kiasi kwamba wananchi bila kujali itikadi zao,
ushirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
“Sera
ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ni jambo jema sana kwani
inawafanya wananchi kuwa sehemu ya chimbuko la miradi ya maenedeleo
katika maeneo yao, na kusisitiza kuwa dhana hiyo inaongeza hamasa kwa
wananchi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza na kusimamia miradi
hiyo,” alisema Asenga.
Anasema
kuwa ongezeko la Shule za msingi na Sekondari katika maeneo mbalimbali
ya nchi ni moja ya matokeo chanya ya utekelezaji wa sera ya ugatuaji wa
madaraka kwa wananchi kwani wananchi walishirikishwa katika ujenzi wa
shule hizo na kweli waliitikia na kufanikisha ujenzi huo.
Kutokana na umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa karibu, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli aliamuwa kuirejesha Wizara ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa chini ya Ofisi ya Rais ili kuraishisha ufuatiliaji
utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi kwa karibu zaidi.
Pamoja
na mambo mengine Serikali kuu imeongeza usimamizi wa karibu zaidi ili
kuziba mianya ya rushwa kwa kusimamia mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa
ikiwemo baadhi ya tozo kuahimshiwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) nah ii imesababishwa zaidi na ubadhirifu uliokuwa umekidhiri hapo awali.
Sera
ya ugatuaji madaraka ya mwaka 1998 imesisitiza kuongeza uwezo wa
kifedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha zenyewe.
Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 imeainisha vyanzo vya
mapato kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo Mikopo ni miongoni mwa
vyanzo hizo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment