Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TAARIFA YA MAOMBOLEZO YA KIFO CHA SIR GEORGE KAHAMA

TAARIFA YA MAOMBOLEZO YA KIFO CHA SIR GEORGE KAHAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.



WASIFU WA MAREHEMU BALOZI SIR CLEMENT GEORGE KAHAMA

Balozi Clement George Kahama, aliyejulikana zaidi kama Sir George alizaliwa tarehe 30 Novemba, 1929 katika Wilaya ya Karagwe na kufariki dunia tarehe 12 Marchi, 2017 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ugonjwa wa Figo  Renal Failure)  kwa takribani miaka miwili.
Katika uhai wake, Marehemu alifanya kazi katika Serikali kwa vipindi mbalimbali zaidi ya miaka 50 ikiwemo awamu tatu za uongozi wa taifa hili baada ya uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1961. Marehemu Sir George alikuwa miongoni mwa waafrika wachache waliopata fursa ya  kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza  la Kutunga Sheria yaani  Legislative Council mwaka 1957 na miaka miwili baadaye kuteuliwa kuwa Waziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mpito ya kikoloni kuelekea uhuru kwa nafasi ya  Waziri wa Ushirika na Ustawi wa Maendeleo ya Jamii akiwa na Wenzake wazalendo Chief Abdalah Fundikira, Amir Jamal, na Solomon Eliufoo na  Mwalimu akawa Waziri Kiongozi ( Chief Minister).
 Baada ya Uhuru Mwaka 1961, Mhe Balozi George Kahama aliteuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Baraza la Mawaziri la Watu tisa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akiwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru.  Kutoka Uhuru mwaka 1961 hadi mwaka 2005 Sir George Kahama aliuteuliwa na Baba wa taifa na baadaye Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, kushika nyazifa za Wizara mbalimbali serikalini zikiwemo Wizara ya Mawasiliano, Uchukuzi na Ujenzi, Wizara ya Biashara na Viwanda, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ushirika na Masoko, Waziri Ofisi ya Rais anayeshughulikia Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma na wakati huohuo akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA).
Katika muda wote wa utumishi wa Umma, Sir George aliaminiwa sana na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere baadaye Mhe Benjamin Mkapa kwa nyakati tofauti waliweza kumtuma katika nchi mbalimbali kuwawakilisha kama  mwakilishi maalum wa Rais (Special Envoy) katika nchi mbalimbali ikiwemo Zaire ambayo sasa inajulikana kama DRC, Burundi na Rwanda,  Holy See (Vatican) na nchi nyingine.
Kazi nyingine alizowahi kufanya Mhe Sir George Kahama ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa Shirika la Maendeleo la taifa (NDC), taasisi iliyopewa jukumu la kusimamia uanzishwaji wa Viwanda nchini, Mkurugenzi Mkuu  na mwanzilishi wa Kituo  cha Kuvutia wawekezaji (IPC) ambacho baadaye kimekuja kujulikana kama  Tanzania Investment Centre-TIC. Kabla ya Uhuru Sir George alikuwa kiongozi wa Chama cha ushirika cha Bukoba, chama ambacho  kilitoa msaada mkubwa wa hali na mali katika kusaidia harakati za ukombozi na kuimarisha TANU kama ilivyokuwa kwa vyama vingine vya Ushirika katika maeneo mbalimbali nchini. Itakumbukwa kuwa  Wazalendo watano waliounda Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mpito mwaka 1959 akiwemo Mzee Paul Bomani, Chief Abdullah Fundikira (Tabora), Solmon Eliufoo (Kilimanjaro), Amir Jamal ( Morogoro) na Kahama Mwenyewe (Kagera) walikuwa viongozi katika vyama vya ushirika katika maeneo waliyotoka.
Aidha, katika Uhai wake, Sir George Kahama aliwahi kutumikia taifa katika nyanja za kidiplomasia kama Balozi wa Tanzania Ujerumani mwaka 1965-1966, Balozi wa Tanzania China (1984- 1989) na Balozi wa Tanzania Zimbabwe (1989-1991).
Katika uhai wake, Sir George Kahama aliwahi kutunikiwa nishani mbalimbali za kitaifa na Kimataifa ikiwemo Knight Commander of the Order of St. Gregory the Great iliyotolewa na Pope John XXIII mwaka 1962. Hii ndiyo  nishani iliyozaa jina la Sir George. Nishani zingine ni kama “The Order of Kilimanjaro iliyotolewa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi 1990, ambayo ni nishani ya juu kabisa wanayotunukiwa watumishi wa umma. Mwaka 1975-1976 alikuwa Mjumbe wa Kundi la Watu Mashuhuri duniani walioteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya utafiti kuhusu athari za Uendeshaji wa Makampuni Makubwa ya Kimataifa katika uchumi wa nchi zanazoendelea.
Mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika ndani ya Chama cha Mapinduzi na Serikali ikiwemo Serikali kuhamia Dodoma kwa kasi kubwa  na chama kuimarika zaidi kumetokea siku chache kabla ya kufariki kwake na kutimiza ndoto  yake zaidi ya miaka 40 aliyojishughulisha na mradi wa Ustawishaji ya Makao Makuu.
Mwaka 1976, Sir George aliteuliwa na Serikali ya Nigeria kama Mjumbe wa Kamati ya watu watatu waliopewa kazi ya kufanya tathmini ya mchakato wa uhamishaji wa Mji Mkuu wa Nigeria kutoka Lagos kwenda Abuja.
Sir George aliwahi kuandika maandiko na vitabu mbalimbali katika Nyanja za Kidiplomasia,  Ushirika, Uchumi,  Maendeleo ya Ujenzi, ikiwemo kitabu cha “The Challenge for Tanzania’s Economy” kilichochapishwa na kampuni ya James Currey Heinemann ya Uingeleza na “Tanzania into the 21st Century”,pia alichangia kuandika kitabu cha “The First Tanganyika Industrial Development Blue Print” pamoja na  Arthur D. Little Inc. wa Marekani.
Mbali na utumishi Serikalini, Sir George Kahama alikuwa Baba mzuri wa familia aliyependa umoja wa familia na alikuwa baba tuliyemtegemea kwa ushauri na dira katika maisha yetu.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe

Utaratibu wa Maombolezo na Mazishi ya Balozi Sir Clement George Kahama aliyefariki Dunia tarehe 12 Machi, 2017

Mwili wa marehemu utawasili nyumbani kwake eneo la Mikocheni B kituo cha Mabasi kijulikanacho kama Business, mnamo saa 11 jioni tarehe 15 Machi, 2017 (Jumatano) na kukesha hadi asubuhi tarehe 16 Machi, 2017.

Mwili wa Marehemu utaondolewa nyumbani kwake kuelekea Julius Nyerere International Convention Centre kuanzia saa  mbili kamili kwa ajili ya viongozi mbalimbali na wananchi kutoa heshima zao za mwisho kabla ya kuelekea Kanisa la Mtakatifu Petro ( St. Peters) Oysterbay Dar es salaam saa tano na nusu 5.30 asubuhi kwa ibada.

Ibada ya mazishi itafanyika katika Makaburi ya Kinondoni  kuanzia saa tisa na nusu  9.30 alasili.









 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa