“HONGERA
MAGUFULI, TANZANIA BILA RUSHWA INAWEZEKANA”
Na Judith Mhina
- MAELEZO
“Rushwa ni adui wa
haki, sitapokea wala kutoa rushwa.” Haya
ni baadhi ya maneno yaliyomo kwenye ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Baba
wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ni mfano wa kuigwa duniani kwa kupinga
rushwa. Hakika maneno hayo yanaonyesha uzalendo, utii na uwajibikaji.
Serikali ya Awamu ya
Tano, katika kipindi cha mwaka mmoja, kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) imeweza kuokoa fedha za umma kutoka bilioni saba ambazo
zimeongezeka mpaka bilioni 53, huku kukiwa na mafanikio makubwa katika
kuthibiti mianya ya rushwa.
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere, katika moja ya hotuba zake amewahi kusema kuwa kuna haja ya
kutunga sheria inayosema kwamba “mtu yeyote
atakayepatikana akitoa rushwa na yule anayepokea wote wawili wana makosa sawa.”
Rushwa ni vita endelevu
iliyoanza Awamu ya Kwanza, na imeendelezwa na Marais waliofuatia wakiwemo Waheshimiwa Ali
Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete. Pamoja na juhudi
binafsi kama Marais na kwa kupitia TAKUKURU mwitikio wa Wananchi katika kupiga vita
rushwa bado ulikuwa mdogo. Hivyo, rushwa ilikuwa inaendelea.
Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, imeonyesha dhamira kubwa ya kuendeleza
mapambano dhidi ya rushwa kwa vitendo na kwamba “Tanzania bila rushwa inawezekana”. Ili kushinda vita hivi kila mtu
anatakiwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, naye kwa kushiriki kivitendo.
Mara tu baada ya
kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais
alifanya ziara katika baadhi ya ofisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu na Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA). Kufuatia ziara hiyo, Mheshimiwa Rais alijionea
mwenyewe mazingira ya kazi ambayo yalionyesha kutowajibika na kuwepo kwa mianya
mingi ya rushwa.
Mheshimiwa Rais
hakusita kuchukua hatua mara moja kama msemo wa Kiswahili usemao “linalowezekana leo lisingoje kesho”.
Aliamua kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi, lengo ni kuhakikisha kuwa
Wateule wapya wanatekeleza majukumu yao kulingana na kasi anayoitaka,
kipaumbelele kikiwa ni mapambano dhidi ya rushwa ili kujenga uchumi na
maendeleo ya nchi.
Katika ziara aliyoifanya
Benki Kuu, Mheshimiwa Rais aliwakumbusha Watumishi juu ya uwajibikaji ikiwa ni
pamoja na kuzingatia muda wa kufanya kazi katika kutekeleza majukumu yao ya
kila siku wawapo kazini. Aidha, Mheshimiwa Rais aliwaambia kuwa Benki Kuu ina
jukumu kubwa la kukusanya na kutunza fedha zinazotokana na mapato ya Serikali,
hivyo wawe makini katika kazi hiyo.
Katika ziara
aliyoifanya TPA Mheshimiwa Rais alifichua upotevu wa Makontena 600 ambayo
hayakulipiwa Kodi. Kutokana na upotevu huo ambao ulionekana kufanyika katika
mazingira ya rushwa na muelekeo wa Serikali kupoteza mapato mengi.
Aidha, Mheshimiwa Rais
aligundua uaribifu wa mashine za kufanyia kazi wakati wa kukagua mizigo jambo
ambalo lilionyesha kuwa ni sehemu ya mianya ya rushwa. Aliagiza mashine hizo
zitengenezwe haraka iwezzekanavyo na wakati huo huo aliamuru mashine za kutolea
risiti kielektroniki - EFDs zitolewe bure kwa Wafanyabiashara ili waweze kulipa
kodi.
Sambamba na matumizi ya
mashine za EFDs, Mheshimiwa Rais amewahamasisha Wananchi kudai risiti kila
wanapokwenda dukani kununua bidhaa. “Ukinunua dai risiti ukiuza toa risiti” alisisitiza
katika ujumbe alioutoa kwa Wananchi. Aidha, aliagiza kukoma kwa matumizi ya bei
elekezi (indicative prices) katika
mchakato wa uthaminishaji wa bidhaa bandarini na usajili wa magari.
Vile vile, Mheshimiwa
Rais aliagiza kuendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi ya juu, kusimamia kwa
karibu zaidi matumizi ya EFDs na utoaji wa risiti, kufuatilia na kudai malimbikizo ya kodi
kutoka kwa wadaiwa sugu, ukaguzi wa kodi
kwa wafanyabiashara na uthibiti wa
misamaha ya kodi.
Pamoja na maekelezo
hayo, Mheshimiwa Rais alilazimika kufanya mabadiliko ya uongozi wa TPA na TRA ambapo
baadhi ya Watendaji wake walichukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengua
nyadhifa zao, kusimamishwa kazi, kuhamishwa na kupelekwa mahakamani. Kufuatia
mabadiliko hayo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, pato la Serikali sasa
limeongezeka kutoka Bilioni 800,000 hadi 1.1 Trilioni kila mwezi.
Maeneo mengine ambayo
Mheshimiwa Rais alifuatilia katika suala la ukwepaji wa kodi ni uwanja wa ndege
wa Dar Es Salaam. Uwanja wa ndege ulikuwa ni eneo jingine ambalo lilikuwa
likitumika kupitisha bidhaa kwa njia ya rushwa zikiwemo rasilimali za misitu, maliasili, madini, nyara za serikali, na madawa ya kulevya.
Kutokana na matukio
mbalimbali ya ukamataji wa Watuhumiwa na bidhaa haramu, Tanzania ilionekana
kuwa kinara katika usafirishaji wa madawa ya kulevya Afrika Mashariki na Kusini
mwa jangwa la Sahara.
Kuhusu utendaji wa
mahakama katika kusikiliza kesi mbalimbali hususani makosa ya rushwa,
Mheshimiwa Rais alionyesha kutofurahishwa na maamuzi yenye dalili za mazingira
ya rushwa yanayoendelea katika chombo cha haki. Alitolea mfano maamuzi yanayotolewa
pale mtu anapokamatwa na vielelezo vyote, na kupelekwa mahakamani maamuzi huchukukua nuda mrefu kwamba
upelelezi unaendelea.
Mheshimiwa Rais alihoji
ni upelezi gani unaoendelea wakati vielelezo vyote vipo? Aidha, ili kudhibiti
rushwa nchini Mheshimiwa Rais ameamua kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi kwa
ajili ya kuwashughulikia wala rushwa.
Vita dhidi ya rushwa na
madawa ya kulevya inayoendelea nchini Tanzania ikiongozwa na Rais wetu
Mheshimiwa John Pombe Magufuli imeacha simulizi katika Ukanda huu wa Maziwa
Makuu, Afrika na Dunia kwa ujumla. Harakati hizi amezianza tangu alipotangaza
baraza lake la Mawaziri ambalo ni dogo ukilinganisha na Mabaraza ya Serikali za
Awamu zilizopita. Lengo likiwa ni kupunguza gharama za matumizi ya Serikali ili
fedha nyingi zitumike katika kutoa huduma muhimu za kijamii na maendeleo ya
nchi kwa aujumla.
Viongozi wa nchi
mbalimbali duniani, zilizoendelea na zinazoendelea, tajiri na masikini,
Mashirika ya Kimataifa na watu binafsi wamejitokeza na wanaendelea kujitokeza
hadharani kumpomgeza Mheshimiwa Rais kutokana na ujasiri alionao katika kutetea
haki za Wanyonge, kuleta mapinduzi ya uongozi wenye kuleta tija, kupiga vita
rushwa na kuzisimamia rasilimali za nchi ili ziweze kutumika kwa maendeleo ya
Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Baadhi ya nchi na
Mashirika hayo yakiwemo yale ambayo yalisitisha kutoa msaada kwa Tanzania
yamenza kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi katika Sekta za miundombinu,
nishati, kilimo nk. ili kuunga mkono juhudi anazozifanya Mheshimiwa Rais.
Katika ukurasa wake wa
Tweeter, Mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa Vyombo vya Habari nchini Dkt Reginald
Mengi ameandika “Nampongeza Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuonyesha kwa
vitendo kwamba Tanzania bila rushwa inawezekana, haya ni mafanikio makubwa na
ya kihistoria Tumuombee ” Amewataka
Wananchi kumwombea na kumuunga mkono katika harakati hizo.
Mheshimiwa Rais anaendelea
kufanya mabadiliko ya Watendaji Wakuu katika Wizara, Idara, Makampuni na
Mashirika ya Umma, Wakala na Taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kuweka
safu mpya ya uongozi ambao utatekeleza majukumu ya Serikali kwa kuzingati
misingi ya sheria na utawala bora.
Madhara ya rushwa yanagusa
kila mtu sio tu kwa Wanachama wa CCM ambapo imetamkwa kwenye ahadi, bali
Watanzania wote wakiwemo vijana
wanaoandaliwa kulitumikia Taifa lao.. Ni dhahiri maneno haya bado yana nguvu
kubwa katika kuhamasisha jamii hususani vijana mashuleni katika kuunga mkono
vita dhidi ya rushwa nchini.
Hakuna atakayepinga
kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli amethubutu na sasa anahitaji kuungwa mkono katika
vita dhidi ya rushwa, hamna vita ya mtu mmoja sote tushiriki. Hongera Mheshimiwa
Rais ni kweli unahitaji kuombewa na Wananchi wote wanaoitakia mema nchi yetu. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki
Afrika.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment