Utambuzi wa historia ya
nchi una mchango mkubwa kwa vijana kuweza kufahamu madhila yaliyotokea na jinsi
viongozi walivyopigana katika kuleta uhuru na maendeleo ya Taifa. Katika makala
haya Judith Mhina wa Idara ya Habari
MAELEZO anaelezea.
Waziri Mkuu Mstaafu wa
Awamu ya Kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt Salim Ahmed
Salim amesema kuwa vijana barani Afrika wana wajibu wa kujua historia ya nchi na
viongozi waliojitolea kuleta uhuru, umoja, amani na maendeleo ya watu.
Amesema, athari za
vijana kutojua historia ya nchi na viongozi waliopigania uhuru ni pamoja na kukosa
uzalendo na uwajibikaji katika kutekeleza malengo ya Serikali katika kuleta
mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii jambo ambalo linarudisha nyuma
maendeleo ya nchi.
Ameeleza kuwa, nafasi
waliyonayo kama vijana ni kujifunza jinsi viongozi wetu walivyoweza kuweka
misingi ya umoja, amani, mshikamano na changamoto zilizowakabili na jinsi
walivyoweza kuzitafutia ufumbuzi badala ya kukata tamaa na kuilaumu Serikali
kuwa haiwasaidii.
Dkt Salim amefafanua
kuwa nchi yetu imeonyesha muelekeo mzuri katika
kulikomboa kundi kubwa la vijana kuelekea kwenye uchumi wa viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa. “Mimi binafsi naipongeza Serikali yetu kwa
kuonesha nia njema ya kupunguza au kuondoa changamoto, zinazowakumba vijana wetu.
Vijana ni wengi kuliko kundi lolote nchini na hawana uhakika wa maisha yao ya
kila siku hivyo wanahitaji kubadilika.”
Mwana-diplomasia huyo
mkongwe nchini ameendelea kusema kwamba maamuzi ya Serikali ya Tanzania kuelekea
kuwa Taifa la viwanda yatahamasisha vijana kupenda kujishughulisha na kazi
mbalimbali za uzalishaji kama vile kilimo nk.
“Jambo la msingi kwa
Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira mazuri na rafiki kwa vijana
kuvutiwa katika sekta mbalimbali kwani nchi yetu inayo ardhi ya kutosha tofauti
na nchi nyingine barani Afrika. Lakini pia napenda kuchuku fursa hii kuwaasa
vijana kuchangamkia fursa hiyo kwani ni mtaji mkubwa kwao katika kujiletea
maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.”
“Serikali ya Awamu ya
Tano imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba malighafi zote zinapata masoko katika
viwanda, miundombinu ya uhakika. Aidha, hii itachochea uzalishaji na ajira kuongezeka
maana bidhaa zote zitaongezwa dhamani hapa nchini badala ya kuagiza nje bidhaa
zilizoongezwa thamani na kudidimiza uchumi wa nchi yetu.” Amesisistiza Dkt
Salim.
Akitoa Mfano wa athari
za vijana kutojua historia yao Dkt Salim amesema Afrika ya Kusini ni moja kati
ya nchi za Afrika amabazo vijana wake wamekata tamaa na kutowathamini Wazee walioshiriki
katika harakati za kuleta ukombozi. Amesema, kitendo hiki cha kuwadharau wazee
kimepelekea mfarakano kati ya makundi haya mawili ambayo yanawajibu mkubwa wa
kushirikiana na kuijenga Afrika ya Kusini yenye neema kwa wananchi wake wote
bila kubagua.
Ameeleza kwamba vijana
hao wamejenga chuki na kuwachukia vijana wenzao waliotoka katika nchi nyingine
za Afrika na kuwaona maadui kwa kwenda nchini mwao na kufanya kazi ambazo wao
wanadhani ni za kwao. Athari hii inajitokeza kwa kuwa hawajui historia ya nchi
yao na nini viongozi wao walipigania katika kuweka misingi ya umoja, amani na mshikamano
Barani Afrika.
Hata hivyo siwalaumu
vijana hata kidogo kwa hakika vijana wana hali ngumu ya maisha kweli kweli, wanahangaika
kutafuta riziki, bila mafanikio. Ni vema kukaa nao na kuongea kuhusu hali zao
za maisha na changamoto zinazowakabili kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa
changamoto husika.
Bara la Afrika lina changamoto
nyingi, kama za uongozi, vita vya madaraka, makundi yanayohamisiana, vita vya
wenyewe kwa wenyewe , ukabila na mengineyo ambayo hayaleti picha nzuri kwa
Afrika na yanadhoofisha ustawi wa Bara letu na vijana kukata tamaa.
Taasisi ya Mwalimu
Nyerere ina jukumu la kutoa elimu kwa vijana wote Barani Afrika juu ya
mustakabali wao na kuweka misingi imara ya umoja, amani, mshikamano
na Maendeleo kwa watu wote katika nchi zao bila kubaguana.
Tunaendesha
makongamano, midahalo na semina katika majukwaa mbalimbali ili kuwaelimisha vijana
kuhusu historia za nchi zao , viongozi wao na misingi waliyoiweka na umuhimu wa
kutanzua kwa pamoja changamoto zilizopo na kuongea yale yote ambayo wanadhani
hayaendi vizuri.
Dkt. Salim amewomba
vijana kuzingatia elimu wanayopewa maana Taasisi ya Mwalimu Nyerere inahitaji
kupata viongozi miongoni mwa vijana wa Tanzania. Ni vema kujua changamoto
zilizopo ili vijana hao watakaochukua uongozi kuendelea kuelezea, kufundisha,
kuuisha katika misingi ya umoja, amani, mshikamano na maendeleo kwa watu wote na
pia ustawi wa Mataifa yote ya Afrika.
Akizungumzia suala la
uongozi na ushiriki wa vijana katika kujenga Taifa, Dkt Salim amesema ni vema
vijana kushirikishwa katika uongozi kwa kuwa bado wana nguvu ya kuleta
maendeleo katika nchi zao. Hata hivyo alitoa tahadhari na kusema “Kijana sio
kigezo cha uongozi hata kidogo”,
Akitoa mfano Dkt Salim amesema,
“Mimi niliteuliwa kuwa Balozi wa
Tanzania nchini Misri nikiwa na miaka
22, nadhani ni umri mdogo kuliko vijana wa sasa wanaoteuliwa, lakini niliaminiwa na kutimiza wajibu wangu
kwa nchi na viongozi wangu walioniteua, kwa kuwa nilijua tulikotoka, tulipo na
tunakotaka kuelekea. Hayo nilijifunza kutoka kwa viongozi wangu Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.”
Dkt Salim muda wote wa
uongozi kama Balozi na mwakilishi wa nchi kimataifa alielezea msimamo, matakwa
na mapendekezo tunayokubaliana nayo kimataifa. Aidha, alisisitiza suala la umoja,
amani, mshikamano na jinsi ya kuleta maendeleo katika nchi zote za Afrika kwa
kuwa nchi yetu inaona bila umoja hakuna suluhisho la amani katika nchi zetu na
alifanya hayo kwa kuwa nilijua historia ya nchi yangu.
“Wito wangu kwa vijana ambao
watakuja kuiongoza Taasisi ya Mwalimu Nyererer ni vema wakajipanga kwa kuwa kazi
iliyopo mbele yao ni kuwaelimisha vijana wenzao ili kuthamini na kuuisha umoja,
amani na kuleta maendeleo kwa watu wote iwe ni sehemu ya maisha yao.”
Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ni mfano wa kuigwa katika kudumisha umoja,
amani na mshikamano katika Bara la Afrika. Umoja wao ulizaa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar. Dkt. Salim alimalizia kwa kusema Mwalimu Nyerere siku
zote za maisha yake, alikuwa akitembea na kuwaasa Watanzania juu ya umoja,
aman, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi. Mwalimu alitambua
wajibu wake.
Akitoa hitimisho Dkt
Salim amesema: “Hapa Tanzania asilimia 60 ya idadi ya watu milioni 50 ni
vijana, hawa wasipoelewa na kuuisha misingi ya Taifa lao yaani umoja, amani, mshikamano
na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi tutakuwa tumefanya kosa kubwa sana na
dunia itatulaumu kwa hilo, kwa sababu Tanzania ndio mfano wa kuigwa.”
0 comments:
Post a Comment