JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI
YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 29 Aprili 2017, ameuagiza
Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuunda kamati itakayoshughulikia suala la kubadilisha
hati ya umiliki wa ardhi katika mkoa huo kutoka miaka 33 hadi miaka 99.
Rais Magufuli
ametoa agizo hilo katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma wakati alipokutana na
viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Jordan Rugimbana, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job
Ndugai na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Kamati hiyo
itahusisha wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano,Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Dodoma na Mkurugenzi wa Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma - CDA.
Rais Magufuli
amesema mji wa Dodoma pekee ndio wenye matatizo makubwa ya umiliki wa ardhi kutokana na hati zake kutolewa
kwa miaka 33 badala ya miaka 99 kama ilivyo miji mingine nchini kitu
kunachorudisha nyuma maendeleo ya mji huo ikiwa ni pamoja na uwekezaji.
'' Dodoma bado
kuna tatizo moja kubwa, katika viwanja vyote vinavyotolewa hapa hati zake ni za
miaka 33, huwezi ukajenga nchi ya viwanda,huwezi ukamvutia muwekezaji ambaye
hati yake ni miaka 33 na wakati anataka kwenda kukopa benki umpe garantii ya
miaka 33,nafikiri hii sheria tulikosea sana na nafikiri hii ni moja ya sheria
ambayo ilifanya hata viwanda vingi visijengwe hapa Dodoma''
amesema Rais Magufuli.
Katika hatua
nyingine, Rais Magufuli ameridhia ombi la Chuo Kikuu cha Dodoma kusamehewa
kulipa kodi ya ardhi ya zaidi ya shilingi Bilioni Mbili iliyokuwa inadaiwa na
CDA na kuagiza kutodaiwa tena kwa kuwa chuo hicho hakifanyi biashara bali hutoa
huduma kwa jamii.
''Chuo kikuu cha
Dodoma hakifanyi biashara ,kipo pale kwa ajili ya kutoa elimu kwa watanzania na
wengi wao ni watoto wa masikini ,ardhi zote kwa mujibu wa sheria namba nne na
namba tano ya mwaka 1999 na sheria nyingine zote za ardhi zikiwemo zile za
mabadiliko za mwaka 2007 mwenye Mamlaka makubwa ya kusimamia ardhi ni
Rais,kulingana na misingi hiyo ili mradi tu hili lisichukuliwe kwa kila
Taaasisi lakini nimetoa special offer kwa Chuo Kikuu cha Dodoma lile deni
lisamehewe , wasidaiwe na wala wasiwadai tena'' amesema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia
ameagiza Ujenzi wa Uwanja wa mkubwa wa michezo mkoani humo unaofadhiliwa na
Mfalme wa Morocco ujengwe karibu na eneo la Nane Nane mkoani Dodoma.
Aidha, Rais Dkt.
Magufuli amesema kuwa anataka uwanja huo
uwe mkubwa na wa kisasa utakaokidhi mahitaji ya kimataifa katika kipindi
cha zaidi ya miaka 100 ijayo na hivyo atasimamia mwenyewe
ujenzi huo.
Kwa upande wa
ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Dodoma, Rais
Magufuli ameagiza kufanywa tathmini ya nyumba zitakazo bomolewa kwa ajili ya
upanuzi wa Uwanja huo ili kulipwa fedha
zao mara moja hali itakayopelekea Uwanja
huo ukidhi mahitaji ya kutua ndege za kimataifa.
Katika hatua
nyingine Rais Magufuli amewashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa ukarimu na
makaribisho makubwa hususan katika sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika tarehe 26 Aprili mkoani humo.
Amesema Wananchi
wa Dodoma wameonyesha ukarimu na uvumilivu wa hali ya juu hata pale mvua
ilipokuwa inanyesha waliendelea kushuhudia sherehe hizo ni kitu ambacho cha
kuigwa na wananchi wa mikoa mingine nchini.
Rais Magufuli
ameondoka mkoani Dodoma kuelekea mkoa wa Kilimanjaro, ambapo pamoja na mambo
mengine atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za sikukuu ya wafanyakazi Duniani,
Mei Mosi.
Naibu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino,
Dodoma
29 Aprili,
2017
0 comments:
Post a Comment