Na Husna Saidi- MAELEZO
Takribani shilingi milioni 271 zinadaiwa kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma Mjini, Mkoani Mara ikiwa ni kodi ya Pango la Ardhi.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi alipofanya ukaguzi wa mfumo wa kodi ya ardhi hivi
karibuni Mkoani humo.
Waziri
Lukuvi alisema kuwa amekagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini
ili kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari
kabla ya hatua za kisheria hazijafuata dhidi yao.
“Nimeagiza
kesi za madai ya kodi zitolewe hukumu ndani ya siku moja tu ili wadaiwa
waweze kuchukuliwa hatua ya kuuzwa kwa mali zao haraka”, alisema
Lukuvi.
Aidha
Waziri Lukuvi alimtaka Afisa Ardhi wa Manispaa ya Musoma Bw.Joseph
Kamonga kuwasilisha majina ya wadaiwa hao katika Mahakama ili waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupiga mnada majengo na
mali zao kama wakikaidi kulipa kodi hiyo.
Kwa
upande mwingine Lukuvi alifanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master
Plan) wa Manispaa ya Musoma na kuwapongeza viongozi na watendaji wa
Manispaa hiyo kwa kuwa Manispaa ya kwanza nchini kuweza kuzindua mpango
huo kutumia kampuni za ndani katika utekelezaji wa mpango huo.
Kufuatia
hatua hiyo Waziri Lukuvi amezitaka Manispaa nyingine kutumia kampuni za
ndani ya nchi ambazo zimesajiliwa na Wizara ya Ardhi katika kutekeleza mipango mbalimbali ya ulipaji kodi za ardhi.
Pia
Waziri Lukuvi aliiagiza Manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa
utekelezaji wa mpango kabambe kwa kutumia wataalam wao (wa serikali) au
Makampuni ya ndani na kutoa nakala za kutosha ili mpango huo uwafikie
wadau wote na kutaka mpango huo utafsiriwe kwa Kiswahili ili Madiwani na
Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waweze kuwafikishia wananchi kwa
urahisi.
0 comments:
Post a Comment