Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI KATIKA JAMHURI YA KOREA KWA MAFANIKIO

WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI KATIKA JAMHURI YA KOREA KWA MAFANIKIO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se. Mhe. Mahiga alikuwa nchini humo kwa ziara ya kikazi ikiwa pia ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.
=====================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alifanya ziara ya kikazi jijini Seoul, Jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko kutoka kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Yun Byung-se ambapo Waziri Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kumpatia mwaliko wa kutembelea taifa hilo hususan wakati huu inapoadhimishwa jubilee ya miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati  katika uwekezaji kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.
Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275  pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600 imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalum kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake. 
Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto Chanika yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160 inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha, Watanzania zaidi ya 1000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya Korea.
Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania mathalani ujenzi wa Reli ya Kati katika viwango vya kimataifa; uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; ujenzi wa maeneo ya viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika miradi mikubwa.
Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia wawakilishi wa  makampuni ya Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma mbalimbali katika sekta hiyo. 
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kukutana na Balozi Sul Kyung-hoon Makamu wa Rais wa KOICA ambapo aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuipatia zaidi misaada Tanzania kwa uwazi na bila ya masharti yeyote. Pia aliipongeza KOICA kwa kushirikisha jamii kuanzia wakati wa ubunifu wa mradi hadi kufikia utekelezaji pamoja na usimamizi. KOICA wameombwa kuongeza maeneo ya misaada na kujumuisha maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na nishati ya umeme wa jua, upepo na maji kwa ajili ya kusaidia maeneo ya vijijini. Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alishauri KOICA kuangalia uwezekeno wa kuanzisha vituo vya kilimo cha kisasa, vituo vya kufugia na vituo vya kufundisha ujasiriamali ili jamii kubwa ya Watanzania iweze kunufaika.
Katika jitihada za kutafuta washirika kwa ajili ya kusaidia kuboresha Chuo cha Diplomasia, Mhe. Waziri akiwa Seoul alitembelea Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha Jamhuri ya Korea na kufanya mazungumzo na Balozi Paik Ji-ah, Kaimu Mkuu wa Chuo. Lengo kuu lilikuwa kujifunza uendeshaji wa Chuo, mitaala iliyoandaliwa kutoa masomo, walengwa wa masomo hayo, aina ya wakufunzi, lugha zinazotumika kufundishia, utaratibu wa kuandaa wanadiplomasia na mifumo ya chuo hicho.
Vilevile kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe. Waziri alikutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Jamhuri ya Korea ambapo aliwahimiza kuheshimu Sheria na Taratibu za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta utaalam utakaosaidia kuiendeleza Tanzania.
Aidha, akizungumza  na Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, Mhe. Waziri aliwasihi kuzingatia masomo ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta faida kwa familia zao na taifa kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwahakikishia Wanajumuiya hao kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ubalozi wa Tanzania jijini Seoul na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa Balozi wa kwanza wa Tanzania katika nchi hiyo. 
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 28 Aprili, 2017

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa