Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TAMKO SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

TAMKO SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA: TAREHE 16/6/2017

         Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inautaarifu umma kuwa Tanzania inaungana na Nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, tarehe      16 Juni 2017.

         Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za        Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini           Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa       rangi.

         Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za          kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya         kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto   wa Afrika.

          Kupitia Maadhimisho haya, Serikali na wadau wengine tunakumbushwa kuandaa            mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii      kuhusu            utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.  

         Aidha, maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu             maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na   malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa   kwa ujumla.
         Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yatafanyika kimkoa hivyo kila Mkoa utaadhimisha   siku hii             kwa kuzingatia mazingira ya mkoa husika.
         Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa            Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu     wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto     ili iweze kudhibiti         changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa       haki sawa kwa watoto            wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Wizara inatoa wito kwa  wanahabari, Asasi za Kiraia na wadau wengine  kushirikiana na Serikali katika kuadhimisha Siku hii na kuelimisha jamii kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu. Utekelezaji wa Kaulimbiu hii utasaidia  kuimarisha ulinzi, usalama wa Mtoto na kutoa haki sawa kwa watoto wote kwa lengo la kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

         Mwisho, tunapenda kuwakumbusha Watanzania wote kutambua kuwa kila mmoja wetu   ana      wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wanapata Haki zao za Msingi kuanzia katika ngazi ya             familia ambayo ni kitovu cha maendeleo ya Mtoto, jamii na taifa kwa ujumla.

                                                                           S. Nkinga
   KATIBU MKUU
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO - 10/6/2017
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa