Na: Frank Shija – MAELEZO
WATANZANIA
watakiwa kuchangamkia fursa za Ajira zitokanazo na utekelezaji wa
Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) Line
kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
Wito
huo umetolewa na Afisa Uhusiano wa Shirika Hodhi la Miundombinu ya Reli
(RAHCO) Bi. Catherine Mushi wakati wa ziara ya kutembelea ujenzi wa
Kambi ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Yapi Merkezi inayotekeleza ujenzi wa
mradi huo iliyo Shaurimoyo, Kariakoo Jijini Dar es Salaam leo.
“Nitoe
rai kwa watanzania wajitokeze kwa wingi kuomba nafasi za ajira
zitokanazo na ujenzi wa Reli hii, mkataba baina yetu na Mkandarasi uko
wazi, wazawa wana asilimia 20% ya nafasi zote za ajira, pelekeni maombi
yenu katika ofisi za Mkandarasi zilizopo Upanga mtaa wa Lugalo ili mnufaike na rasilimali zenu,” alisema Bi. Catherine.
Wakati
huohuo Bi.Catherine amewatahadharisha wananchi kuepuka kutapeliwa na
watu wanaopita mitaani wakiwalaghai kuwa wao ni mawakala wa ajira
waliotumwa na RAHCO kwa ajiri ya kutoa ajira kwa watanzania wanaohitaji
kufanyakazi katika ujenzi wa mradi wa Reli hiyo badala yake amewataka
wananchi kupelekea maombi yao kwenye Ofisi za Mkandarasi Kampuni ya Yapi
Merkezi zilizopo Mtaa wa Lugalo Upanga Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia
mradi huo amesema kuwa ujenzi umeanza kwa hatua mbalimbali za Kiinjinia
ambazo ni pamoja na kupendekeza njia ambapo Reli itapita, ujenzi wa
Kambi zitakazotumiwa na mafundi pamoja na wafanyakazi wakati wa ujenzi
wa mradi huo.
Bi.
Catherine amezitaja Kambi hizo kuwa ni pamoja na Shaurimoyo, iliyopo
Ilala, Dar es Salaam, Soga Kibaha mkoani Pwani pamoja na Ngerengere
mkoani Morogoro.Ambapo Kambi ya Soga ndiyo itakuwa kubwa itakayokuwa na
kiwanda kwa ajili ya kutengeneza Mataruma ya Reli yanayotumia Simenti.
Amesema
kuwa Kambi hizo zitatumiwa na wafanyakazi waandamizi wa Kampuni ya Yapi
Maerkezi ambapo watakuwa wanalala hapo kwa ajili ya kurahisisha
shughuli zao ikiwemo urahisi wa kuhamisha mitambo kutoka sehemu moja
kwenda sehemu nyingine kadri ya mahitaji.
Kwa
mujibu wa Afisa Uhusiano huyo takribani watanzania 150 wameajiriwa
katika hatua ya awali ya ujenzi wa Kambi ya Shaurimoyo ambayo
inakadiriwa kutumiwa na wafanyakazi zaidi ya 100 itakapokamilika.
Ujenzi
wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) Line kutoka Dar es
Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa Kilomita 300 ulizinduliwa rasmi
tarehe 12 Aprili, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo, ujenzi huo unafanywa na
Kampuni ya Yapi Merlkezi kutoka Uturuki kwa kushirikiana na Kampuni ya
Motaengli Afrika na kugharimu takribani sh.2.7.
Ujenzi
huu ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Ujenzi wa Reli
ya Kisasa (Standard Gauge). Mradi wote utajengwa kwa awamu nne ambapo
una jumla ya urefu wa kilomita1,219 utakaoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza. Mradi huo unatakadiriwa kuibua takribani ajira milioni moja hadi kukamilika kwake.
Mwisho.
Virus-free. www.avast.com |
0 comments:
Post a Comment