Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » CHAKUA YAMUOMBA MAGUFULI KUTOA MAAGIZO KUTUMIKA KWA TIKETI ZA KIELETRONIKI

CHAKUA YAMUOMBA MAGUFULI KUTOA MAAGIZO KUTUMIKA KWA TIKETI ZA KIELETRONIKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Na Bushiri Matenda na Thobias Robert-Maelezo

Chama cha kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA) kimemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutoa maelekezo rasmi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa  Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kuharakisha uanzishwaji wa mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki.

Mwenyekiti wa CHAKUA Taifa, Hassan Mchajama, ametoa kauli hiyo leo, Jijini Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hasara inayoipata Serikali kwa kutotumika kwa tiketi za kielektroniki kwa vyombo vya usafiri.

Mchajama amesema kuwa chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuelimisha Umma pamoja na kuzungumza na mamlaka husika juu ya umuhimu wa kuwa na mfumo bora wa utoaji huduma ikiwemo suala zima la ukataji wa tiketi za mabasi kwa njia ya kielektroniki.

“CHAKUA tunaamni kuwa suluhisho la kuwaondolea abiria kero na usumbufu wa kuibiwa, kulanguliwa tiketi, kudhalilishwa na wapiga debe na kuuziwa tiketi feki liko katika kuanza kwa matumizi ya mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki,” alisisistiza Mchajama.

Kupitia mfumo wa kielektroniki utawezesha Serikali kukusanya mapato yake kwa uhakika kuliko ilivyo sasa na kumsaidia mtumiaji wa huduma kununua tiketi popote alipo na kuepusha adha zinazojitokeza sasa kwa abiria.

Pia chama hicho kimepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mabadiliko makubwa na yenye tija kwa Taifa ikiwemo kufunguliwa kwa Kituo maalum cha kuhifadhi kumbukumbu za matumizi ya malipo na utoaji risiti kwa mfumo wa Kielektroniki.

Aidha Mchajama amesema kuwa, Serikali inapoteza takribani shilingi milioni 300 kila baada ya miezi mitatu kutokana na kutotumika kwa tiketi za kielektroniki kwa wasafiri wa mabasi.

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wadau wote wanaohusika na usafirishaji wakiwemo SUMATRA, TRA, Jeshi la Polisi, TABOA kwa pamoja waweze kushirikiana katika kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa mfumo huo.

Chama cha CHAKUA kimekuwa kikikutana na wadau mbalimbali wa usafirishaji na kuwaeleza changamoto zinazowakabili abiria katika sekta ya usafirishaji wa nchi kavu na majini hapa Nchini, ukiwemo urasimu unaofanyika katika ununuzi wa tiketi ambapo kwa sasa wanalazimika kununua tiketi moja kwa moja kwa mawakala na wapiga debe, ambapo wengi wao wamekuwa wakiwatapeli abiria.

Hivyo basi, kwa kuanzishwa mfumo wa kielektroniki utaondoa adha hiyo kwa abiria na Serikali kukusanya mapato kwa uhakika na kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa jamii na maendeleo kwa ujumla

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa