Kiwango
cha biashara kati ya Tanzania na China kimefikia Dola bilioni 4.7
katika kipindi cha mwaka 2015 na kwamba kiwango hicho kinatarajiwa
kuongezeka zaidi.
Mwakilishi Mkuu Mkazi wa Masuala ya Uchumi na Biashara, kutoka Ubalozi wa China hapa nchini, Bw. LIN Zhiyong,
amesema hayo Jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya
forodha kuhusu Maboresho na Vihatarishi hatari vya kiforodha,
yanayotolewa kwa maafisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na
wataalamu kutoka Chuo cha Forodha cha Shanghai-China.
Bw. Zhiyong
amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na kwamba
hivi karibuni nchi yake iliipatia Tanzania seti 3 za makontena ya vifaa
vya kisasa kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar
es Salaam, vyenye uwezo mkubwa wa kugundua pembe za ndovu, dawa za
kulevya na silaha zinazosafirishwa kimagendo kutoka ndani na nje ya
nchi.
Alisema
pia kuwa hivi sasa nchi yake ni kama imeondoa kabisa kodi kwa bidhaa za
Tanzania zinazosafirishwa kwenda China hadi kufikia asilimia 97, na
kwamba anatarajia kuona wafanyabishara wa Tanzania wakichangamkia fursa
hiyo na kuongeza kiwango cha bidhaa za Tanzania zenye ubora
zinazosafirishwa kwenda nchini mwake.
Bw. Zhiyong,
amezishauri Idara za Forodha za Tanzania na China kuimarisha
ushirikiano na kukuza biashara na uwekezaji kwa faida ya pande zote
mbili.
Akizungumzia
kuhusu sekta ya elimu, Mtaalamu huyo wa masuala ya Uchumi na Biashara
amesema kuwa hadi mwishoni mwa mwaka uliopita, Watanzania 5,000 wako
nchini China wakipatiwa mafunzo mbalimbali kupitia Wizara ya Biashara ya
nchi hiyo kwenye vyuo mbalimbali.
Alisema
kuwa wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini China wameiletea sifa
kubwa Tanzania kutokana na umahili wao mkubwa katika masomo pamoja na
nidhamu ya hali ya juu jambo linalowafanya wawe mabalozi wazuri wa nchi
yao ndani na nje ya nchi kwa ujumla.
Akifungua
mafunzo hayo ya majuma mawili, Naibu Kamishna wa Maboresho ya
vihatarishi hatari, kutoka Idara ya Forodha ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania-TRA, Bw. James Mbunda, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga
kuwajengea uwezo wafanyakazi wa idara hiyo wa kukabiliana na vihatarishi
vyote vya masuala ya forodha kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini
kwenda nje ya nchi.
Amesema
kuwa mafunzo hayo yameratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Utumishi
ikiwa ni hatua ya Serikali ya kuboresha utendaji kazi wa idara hiyo kwa
manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Ameyataja
baadhi ya masuala watakayopewa utaalamu na wakufunzi watano kutoka Chuo
hicho cha Forodha cha Shangai wakiongozwa na Profesa wa masuala ya
forodha Bi. Sun Hao, ni pamoja na kupitia sheria mbalimbali za forodha,
misamaha ya kodi, udhibiti wa biashara, namna ya kukabiliana na watu
wasio tii sheria na vigezo vya utoaji leseni.
0 comments:
Post a Comment