Imeandikwa na Mwandishi Wetu
KAMPUNI nne za mafuta zimeshinda zabuni za uletaji wa mafuta nchini
kwa mwezi Septemba mwaka huu. Ufunguaji na utangazaji wa washindi wa
zabuni ulifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Uagizaji
wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), chini ya uenyekiti wa Ali Ahmed Saeed.
Kampuni zilizoshinda zabuni hiyo ni Trafigura Pte Limited, Addax
Energy SA, Sahara Energy Resources Limited na GBP Tanzania Limited.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PBPA, Modestus Lumato, alifafanua kwamba
zabuni hizo zinahusu uletaji wa jumla ya tani 360,000 za dizeli na tani
110,000 za petrol, mafuta ya taa na ndege.
Lumato alisema mahitaji ya mafuta yameongezeka, hivyo zabuni hizo
zimehusisha uletaji mafuta ya nyongeza kwa mwezi Agosti kuziba upungufu
uliojitokeza. “Kwa mwezi wa tisa tunategemea kuwa na meli saba, mahitaji
ya mafuta yameongezeka sana…tutakuwa na meli saba yaani meli tatu kwa
ajili ya dizeli tani 360,000 halafu meli tatu za petroli, meli ya mafuta
ya ndege na mafuta ya taa,” alisema.
Lumato alitaja baadhi ya sababu za mahitaji ya mafuta kuongezeka ni
pamoja na usafirishaji wa mazao mashambani kuongezeka kipindi cha mavuno
na kuondolewa kwa kodi ya leseni ya usafirishaji.
Katika zabuni hiyo iliyoshuhudia kampuni ya Kitanzania ikishinda
tenda ambayo ni GBP Tanzania Limited, Lumato alisema kwamba kwa siku
nchi hutumia lita milioni 4.7 za dizeli, lita milioni 3.7 za petroli,
lita 450,000 za mafuta ya ndege na lita 150,000 za mafuta ya taa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment