Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MCHAKATO WA UANZISHAJI TAASISI YA TEKNOLOJIA YA UJENZI WAANZA.

MCHAKATO WA UANZISHAJI TAASISI YA TEKNOLOJIA YA UJENZI WAANZA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano - Sekta ya Mawasiliano, Injinia Angelina Madete amesema uanzishaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ufundi (ICoT), utasaidia kupunguza pengo lililopo sasa baina ya wahandisi, mafundi sanifu na mafundi mchundo hapa nchini.
Akifungua warsha ya wataalam washauri na wadau wa Taasisi ya Teknolojia ya Ufundi Jijini Dar es salaam leo, Mhandisi Madete amewataka wataalam hao kufanya uchambuzi wa kina ili kuwezesha taasisi hiyo mpya kukidhi mahitaji ya mafundi sanifu na mchundo na hivyo kukidhi uwiano wa kimataifa unaotaka mhandisi mmoja, fundi sanifu watano na mafundi mchundo 25.
“Tunataka kuwa nchi ya viwanda vya kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ni lazima tuwe na wahandisi, mafundi sanifu na mafundi mchundo wa kutosha watakaofanyakazi kwa weledi na kumudu ushindani katika soko la ajira”, amebainisha Injinia Madete.
Mhandisi Madete amesema kuwa pengo la wahandisi, mafundi sanifu na mafundi mchundo limeongezeka kutokana na vyuo vingi vya kati kutoa shahada hivyo uwepo wa ICoT utakabiliana na kumaliza changamoto hiyo.
Aidha amezungumzia umuhimu wa taasisi hiyo mpya kuanzisha kozi ya waendesha mitambo ambayo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini na kwa sasa hakuna chuo kinachotoa kozi hiyo.
Hakikisheni taasisi hii inapata ithibati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), ili kuwawezesha wahitimu wote wa ICoT kupata fursa za kujiendeleza na elimu ya juu.
Naye mratibu wa wataalam wa uanzishaji ICoT Profesa Peter Chonjo amesema wamejipanga kuhakikisha taasisi hiyo ya teknolojia ya ujenzi inakuwa ya mfano hapa nchini kwa kuwa itawezesha wataalam wengi wa ujenzi kuwa na weledi unaokubalika na kuibua uwezo wa ushindani katika soko la ajira na hivyo kuwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Tanzania inakadiriwa kuwa na mtandao wa barabara wenye zaidi ya kilometa elfu 87 na kati ya hizo elfu 35 ni barabara za kitaifa na elfu 52 ni barabara za Wilaya ambazo ujenzi wake unahitaji wataalam wa kutosha katika fani ya ujenzi na uendeshaji wa mitambo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa