JAPAN kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (JICA) imetenga
bajeti ya Sh bilioni 251.2 kwa ajili ya misaada ya maendeleo kwa
Tanzania kwa mwaka wa fedha 2017/18 tofauti na Sh bilioni 90 ilizotenga
kwa mwaka uliopita 2016/17.
Fedha hizo ni mwendelezo wa Serikali ya Japan wa kutoa misaada na
mikopo kwa Serikali ya Tanzania tangu ushirikiano wa kimaendeleo kati ya
mataifa hayo mawili uanze mwaka 1963. Mwakilishi Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Toshio Nagase alisema jana Dar
es Salaam kuwa misaada ya Kijapani kwa Tanzania inakaribia dola za
Kimarekani milioni 3,855.31 kati ya kipindi cha mwaka 1963 hadi 2015.
Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kutolewa kwa Tanzania
ikilinganishwa na wapokeaji wengine wa misaada ya maendeleo kwa nchi za
Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara na ya kwanza kwa Afrika
Mashariki ikifuatiwa na Kenya (dola 3,835.41), Zambia (dola 2,598.33).
“Tunaridhishwa na matumizi ya fedha za misaada na mikopo tunazotoa kwa
Serikali ya Tanzania na miradi ambayo Japan imeisaidia Tanzania.
Kwa mfano, JICA imesaidia kuboresha barabara za jiji la Dar es Salaam
tangu mwaka 1980 ikiwemo daraja la Selander, Barabara ya Morogoro,
Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, barabara mpya ya Bagamoyo, eneo la
Kariakoo, Sinza, Mwananyamala, Ilala, Tabata, Kijitonyama na Barabara ya
Kilwa,” alisema Nagase na kuongeza: “Katika mwaka 2016/17, JICA
ilitekeleza majukumu yake kwa ufanisi hasa katika kuwekeza katika
miundombinu na rasilimali watu.
Baadhi ya uwekezaji katika miundombinu inajumuisha ujenzi wa barabara
za juu Tazara (Tazara flyover), uendelezaji wa barabra za ukanda wa
Mtwara (Mtwara corridor development project), uendelezaji wa barabara za
ukanda wa kaskazini ambao ni sehemu ya barabara kuu ya Afrika Na. 4
(Cairo- Cape-Trans-African Highway No. 4) na ujenzi wa laini ya umeme
kutoka Iringa hadi Shinyanga.” Imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa
barabara za juu Tazara ndiyo mradi mkubwa kati ya miradi ambayo JICA
imeitekeleza nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi wa Tazara, Nobuhiko Maruni, barabara za
juu Tazara zina urefu wa mita 425 na zina uwezo wa kutumika kwa miaka
100 ijayo kama zitatunzwa na kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara.
Nagase aliongeza kuwa Japan huipa Tanzania kila mwaka msaada wa
kimaendeleo wa dola za Kimarekani milioni 20 na mkopo wa dola za
Kimarekani milioni 100.
Kuhusu rasilimali watu, Mwakilishi huyo wa JICA alisema kwa mwaka
uliopita waliweza kuwekeza katika rasilimali watu katika sekta
mbalimbali kama vile kilimo katika maeneo mbalimbali nchini, biashara,
afya, uvuvi, lakini pia upatikanaji wa maji safi na salama katika mkoa
wa Tabora na Zanzibar, ufadhili wa masomo nchini Japan kwa vijana wa
Tanzania kupitia mpango wake ujulikanao kama elimu ya biashara Afrika
(African Business Education-ABE).
Kwa mujibu wa Nagase, JICA iliweza kuwasaidia Watanzania 18,613
kupata fursa ya mafunzo nchini Japan kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 2015.
Kwa kiwango cha shahada ya uzamili jumla ya Watanzania 81 wamesaidiwa
kupata elimu hiyo kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2017.
Aidha, shirika hilo limesema kuwa limejipanga kuendelea kuboresha
mipango ya kilimo kwenye wilaya mbalimbali kwa mwaka 2017/18 kupitia
mpango wa TANSHEP (Tanzania Small Holder Horticulture Empowerment
Promotion) pamoja na kumalizia ujenzi wa barabara za juu Tazara ikiwa ni
sehemu ya kukabili changamoto za maendeleo ya Tanzania kulingana na
mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano na matakwa ya utawala wa
Rais John Magufuli.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment