Imeandikwa na Regina Mpogolo
MSICHANA wa miaka 19, Elizabeth Chengula anaelezea anavyoishi maisha
ya shida ambayo ni pamoja na kupata mtoto mwenye tatizo la utata wa
jinsi yake huku madaktari wakifafanua tatizo hilo kitaalamu.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Chengula alisema Agosti
mwaka jana alijifungua mtoto ambaye aliambiwa katika Zahanati ya Ifisi
iliyoko Mbalizi Mbeya Vijijini kuwa mtoto huyo ni wa kiume, lakini siku
zinavyozidi kwenda hajui ni wa jinsi gani baada ya maumbile yake ya siri
kuwa hayaeleweki ni ya kike au ya kiume. Chengula alisema alipompeleka
hospitali huko Mbeya aliambiwa kuwa tatizo hilo ni mpaka ampeleke
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini kutokana na hali yake ya
maisha kuwa duni, hakuwa na uwezo wa kufika Dar es Salaam iliko
hospitali hiyo.
“Hali hii ilinichanganya sana nikaenda kuomba msaada Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya, walinisaidia nikachangiwa pesa kwenye ofisi yao ikapatikana
laki mbili na orobaini, nikapewa kwa ajili ya safari pamoja na barua ya
rufaa, hata hivyo pesa hizo ziliibiwa zote pamoja na begi langu nikiwa
safarini kuja Dar es Salaam,” alieleza msichana huyo. Akielezea maisha
yake, alisema mama yake ni mlemavu wa mikono na miguu ambaye hawezi
kujishughulisha na kitu chochote na yeye na mama yake wanaishi kwa ndugu
yao ambaye anafanya vibarua vya kubeba mizigo ya watu sokoni Mbalizi.
“Maisha yangu ni ya shida sijui nitapataje msaada wa mtoto huyu
ambaye nimeambiwa Muhimbili anatakiwa kufanyiwa vipimo na baadaye
kufanyiwa upasuaji na mimi sina mtu yeyote wa kunisaidia,” alisema
Chengula kwa masikitiko. Aliongeza kuwa pamoja na kwamba hana uwezo wa
kumsaidia mtoto wake, lakini anaamini atapata msaada mtoto wake aweze
kuwa kama watoto wengine ingawa baba wa mtoto huyo alimkimbia baada ya
kuambiwa mtoto ana tatizo.
“Baba wa mtoto alisema hamtaki mtoto na nisimpe jina lake mtoto huyu
ni mkosi hataki kujihusisha naye, nahangaika peke yangu nikipata watu wa
kunisaidia nitashukuru kwa sababu mimi naamini sio mkosi na atapona,”
alieleza msichana huyo. Aidha, alisema katika kipindi chote hicho
amemlea mtoto wake kama wa kiume na alimpa jina la kiume ingawa hajui
jinsi yake.
“Kipindi chote hicho mimi namlea kama mtoto wa kiume kwa mavazi na
jina nimempa la kiume, sasa nikiambiwa ni wa kike sijui nitaenda
kuwaambia nini watu kule nyumbani, nadhani nitahama kabisa na sijui
nitaenda wapi maana hawatanielewa,” alibainisha. Watoto kuzaliwa na
jinsi mbili au isiyoeleweka Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa Watoto,
Zaituni Dkhary akizungumzia tatizo hilo, alisema mzazi yeyote anaweza
kupata mtoto wa namna hii na kwamba tatizo hilo sio mkosi.
Dk Dkhary alisema wazazi mwanzoni huwa wanachanganyikiwa kwa sababu
hawajui kama wataweza kuwa kawaida yaani wa jinsi moja walivyo watu
wengine au la, lakini tatizo hilo lina ufumbuzi. “Na hakuna kesi yoyote
ambayo tumeipata mzazi kurudi kulalamika kwamba kuna hali tofauti
imetokea baada ya kuwasaidia, hapa Muhimbili tunawafanyia upasuaji
vizuri kabisa kuwarekebishia maumbile na wanakuwa sawa kabisa,” alieleza
Dk Dkhary.
Alisema madaktari wanaofanya upasuaji huo ni madaktari bingwa wa
upasuaji wa watoto (Pediatric Surgeon) au madaktari bingwa wa upasuaj wa
njia ya mkojo (Urologist Surgeon) na kama kuna kesi ngumu wanaweza
kusaidiana lakini upasuaji huo ni wa kawaida kabisa. Daktari huyo
alisema watoto ambao wanazaliwa wakiwa na maumbile hayo ni vigumu
kuelewa jinsia yake kwa kumtazama kwa macho katika sehemu zake za siri
kwani wanakuwa na viungo vya jinsia ya kike na pia ya kiume.
“Watoto hawa kwa mzazi hata mzalishaji inakuwa ni vigumu kutambua kwa
kuangalia kwa sababu ukimuangalia mtoto sehemu zake za siri anakuwa na
kiungo cha kiume na pia maumbile ya kike na kwa chini anakuwa na tundu
la kukojolea,” alieleza. Anasema katika hospitali hiyo wanapokea watoto
waliozaliwa katika hali hiyo wengi ambapo karibu kila wiki wanawafanyia
upasuaji wa kurekebisha maumbile baada ya kuwafanyia vipimo mbalimbali
na kubaini jinsi yake.
“Kama ni mtoto wa kike utamfanya awe wa kike kwa kurekebisha maumbile
yake, na kama ni wa kiume hivyo hivyo, na ni lazima kufanya vipimo
kadhaa kwanza ili kuhakikisha jinsi ya mtoto,” alisema na kuongeza kuwa
hakuna sababu maalumu inayoweza kusababisha kupata mtoto mwenye tatizo
hilo.
Alitaja vipimo hivyo kuwa ni pamoja na vya damu kujua vinasaba vya
mtoto na pia kuchukua kijinyama kwenye mdomo wa mtoto kupima baada ya
kuiotesha pamoja na kipimo cha MRI kuona viungo vya ndani vya mtoto ni
vya jinsi gani.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment