Imeandikwa na Matern Kayera
SERIKALI iko kwenye hatua za mwisho za kupeleka bungeni Muswada wa
Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kudhibiti matumizi mabaya ya
simu za mkononi, barua pepe na mitandao ya kijamii.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
jana, Edwin Ngonyani (pichani) wakati akifungua mkutano wa pamoja kati
ya Wachina na Watanzania uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa
Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Sheria hiyo ya kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii
itakuwa ya tatu baada ya Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao na Sheria ya
Miamala ya Kimtandao kupitishwa mwaka 2015.
Imeelezwa kuwa muswada huo wa sheria hautachukua zaidi ya mwaka mmoja
kupitishwa kuwa sheria na itakapokuwa sheria kamili itawapa fursa watu
watakaochafuliwa au kutendewa uhalifu wa kimtandao kudai fidia.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Ngonyani, watumiaji wa simu waliosajili
simu zao za mkononi imeongezeka kutoka 300,000 mwaka 2000 hadi kufikia
milioni 39 kwa sasa. Kuhusu idadi ya mitandao ya kijamii inayotumika
nchini, Ngonyani alisema kwamba ni vigumu kwa sasa kuidhibiti mitandao
hiyo kwa asilimia 100 kwa kuwa wanaoimiliki wako nje ya nchi na hasa
Marekani na siyo Watanzania.
Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi itasaidia kumjua mtu mahususi
atakayefanya uhalifu kupitia simu yake ya mkononi au hata kama atatumia
simu ya mtu mwingine, na hivyo hivyo kwenye mitandao ya kijamii na barua
pepe.
Naye Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema matumizi ya
mitandao ya kijamii yameimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na
China. Alisema ushirikiano kati ya Tanzania na China umekuwa na manufaa
katika nyanja mbalimbali kama vile kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, amani
na usalama, ushirikiano wa kimataifa na ushirikiano baina ya mtu na
mtu. Kuhusu maendeleo ya intaneti alisema kwamba kati ya kampuni 10
kubwa za intaneti duniani, kampuni nne zinatoka China.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment