Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
\Na. Neema Mathias- MAELEZO
Wachimbaji
wadogo wa dhahabu kutoka wilaya ya Kahama wanatarajia kutembea kwa
miguu kutoka Kahama mpaka Dar es salaam kwa ajili ya kumuunga mkono Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa juhudi zake
za kuijenga Tanzania mpya.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Young Human Rights Advocates
(TYHRA) Samwel Shami kwa niaba ya wachimbaji hao, alipokuwa akizungumza
na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam.
“Tumeamua kwa hiyari
yetu kutembea kwa miguu na baiskeli kutoka Kahama mpaka Dar es Salaam
kumpongeza Rais wetu mpendwa na tunaomba Watanzania wenzetu wanaoipenda
nchi yetu watuunge mkono”, alisema Bw. Shami.
Bw. Shami amesema
kuwa wachimbaji hao wamefurahishwa na juhudi za serikali ya awamu ya
tano pamoja na moyo wa utu wa Mhe. Raisi katika kuhakikisha rasilimali
za Tanzania zinawanufaisha Watanzania wote.
“Kuna wakati
tulijiona kama yatima kwenye nchi yetu, na tulianza kuamini kuwa dhahabu
yetu imegeuka laana badala ya baraka alizotupatia mwenyezi Mungu bure,
lakini sasa tunaiona nuru kubwa kupita Raisi wetu”, amesisitiza Bw.
Shami.
Aliendelea kusema kuwa mwaka 2008, Shirika la TYHRA kwa
kushirikiana na wachimbaji wadogo, wadau wa maendeleo na wafanyakazi wa
mgodi wa Bulyanhulu walianzisha harakati zilizojulikana kama ‘Native
Solidarity Movement’ kwa lengo la kudai haki zao za msingi katika migodi
lakini hazikuzaa matunda.
Hata hivyo Bw. Shami ameyaomba
mashirika mengine yasiyo ya kiserikali na yeyote anayeitazama Serikali
kwa jicho la maendeleo na mwenye mapenzi mema na nchi yake wajaribu
kutumia nguvu kubwa kuipongeza, kuishauri na kuitia moyo serikali kama
wanavyotumia nguvu kubwa kukosoa na kulaani mambo mbalimbali
yanayofanywa na Serikali.
Bw. Shami alifananisha matatizo na
changamoto za Watanzania sawa na kupewa tembo mkubwa kumla, jambo ambalo
linahitaji hatua kwa hatua, kipande kwa kipande, hivyo aliwataka
Watanzania wampe Rais muda wa kutatua changamoto zao kwani juhudi zake zimeonekana toka alipoingia madarakani.
Shirika
la Young Human Right Advocates linajihusisha na utetezi wa haki za
binadamu na wadau wa maendeleo. Shirika hilo linashirikiana na
wachimbaji wadogo wa wilaya ya Kahama kuchangia maendeleo ya kijamii,
kiuchumi na kisiasa na pia kukemea na kuelimisha jamii.
0 comments:
Post a Comment