Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (kulia) na
Mkandarasi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Reynolds, Bw. Dan Yzhak Shahn (kushoto)
wakibadilishana mkataba wa Sh. bilioni 101 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya
Kidatu – Ifakara yenye urefu wa Kilometa 66.9, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha
na Mipango Jijini Dar es Salaam leo Julai 28, 2017. (PICHA NA WFM)
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa pili
kulia) na Mkandarasi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Reynolds, Bw. Dan Yzhak
Shahn (kushoto) wakisaini mkataba wa Sh. Bilioni 101 kwa ajili ya ujenzi
wa Barabara ya Kidatu- Ifakara yenye urefu wa Kilometa 66.9, katika Ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto)
akizungumza kuhusu umuhimu wa barabara ya Kidatu – Ifakara kwa kiwango cha lami
kwa maendeleo ya Kilimo baada ya kutiliana saini mkandarasi atakayejenga
barabara hiyo, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango Jijini Dar es Salaam.
Balozi
wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Roeland van de Geer akizungumza kwa
niaba ya EU, UK-AID na USAID, kuhusu mpango wao wa kuendelea kuisaidia Tanzania
katika ujenzi wa miundombinu baada ya kuwekwa saini mkataba wa Sh. bilioni 101
kwa ajili ya Ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara, katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban.
Baadhi
ya wajumbe waliohudhuria hafla ya kuwekwa saini mkataba wa Sh. bilioni 101 kwa
ajili ya Ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara wakifuatilia nyaraka za mkataba
huo kabla ya kusainiwa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar
es Salaam.
-----------------------------------------------------------------------------
Benny
Mwaipaja, WFM
WIZARA ya Fedha na Mipango imetiliana saini na Kampuni ya
ujenzi wa barabara ya Reynolds kandarasi ya ujenzi wa barabara ya kutoka Kidatu
hadi Ifakara mkoani Morogoro, yenye urefu wa kilometa 67 kwa kiwango cha lami
utakaojengwa kwa shilingi bilioni 101, kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya,
Marekani na Uingereza.
Mkataba huo umesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Dan
Yzhak Shahn, Bw. Benjamin Arbit ambaye ni Mkandarasi kutoka Kampuni ya Ujenzi
ya Reynolds.
Kiasi hicho cha fedha ni sawa na
Euro milioni 40.4 ambapo Euro milioni 29.6 zimetolewa kwa
ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Misaada la Uingereza-UK-AID, huku
kiasi kinachobaki cha Euro milioni 10.8 kikitolewa na Shirika la Misaada
la watu wa Marekani- USAID.
Akizungumza mara baada ya kutiwa
saini kwa kandarasi hiyo, Bi. Amina Khamis Shaaban, amesema ujenzi wa barabara
hiyo utakaohusisha pia ujenzi wa daraja katika Mto Ruaha Mkuu, utasaidia
wakulima wadogo kupitia Program ya Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini
mwa Tanzania-SAGCOT, walioko katika Bonde la Mto Kilombero, kuyafikia masoko ya
uhakika ya mazao yao.
“Kuimarika
kwa kipande hiki cha barabara kutaongeza uzalishaji wa nafaka na bidhaa
nyingine hatimaye kupunguza gharama za chakula na umasikini wa wananchi”
aliongeza Bi. Shaaban
Bi Shaaban amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa msaada
huo utakao fungua milango ya kiuchumi kwa Watanzania kupitia Program hiyo ya
kuendeleza Kilimo katika Ukanda huo wa Kusini-SAGCOT, unaohusisha pia kuboresha
masuala ya nishati ya umeme.
“Ujenzi wa miundombinu unalengo la kuchochea maendeleo ya
kilimo cha kibiashara kwa kuwa itasaidia kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara
na wakulima”. Aliongeza Bi Shaaban.
Aidha amesema uboreshwaji wa miundombinu utachochea
uwekezaji ambao ndio chachu ya maendeleo ya biashara za watu wa chini, hivyo
kuinua kiwango cha maisha yao.
“Barabara ya Kidatu hadi Ifakara ndiyo inayounganisha Wilaya
za Kilombero na Ulanga na ni barabara kuu itokayo Bandari ya Dar es Salaam
kwenda Zambia, Malawi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hivyo
kuwa na tija katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi jambo ambalo ndio lengo
kubwa la Wahisani hao”. alifafanua Bi Shaaban.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini,
Roeland van de Geer ameahidi kuwa EU, UKAID na USAID, zitaendelea kushirikiana
kwa kiwango cha juu na Serikali ya Tanzania katika kuboresha Sekta ya ujenzi na
miundombinu kwa ujumla lakini pia atahakikisha wanachangia katika kupata soko
la uhakika la mazao ya kilimo.
Sekta ya kilimo ni muhimu kwa ukuaji
wa uchumi wa Tanzania mbapo zaidi asilimia 70 ya wakazi wake hutegemea kilimo
na kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza uzalishaji, kipato na kukuza ajira,
hususan kwa wanawake na vijana ikiwa miundombinu inayochangia ukuaji wa Sekta
hiyo itazidi kuimarika.
0 comments:
Post a Comment